Wiki iliyopita mtaalamu alianza kuelezea maana ya vidonda vya tumbo na jinsi vinavyomshambulia mgonjwa.
Alikumbusha kuwa vidonda hivi vina maumivu makali na vinatokea kwenye ukuta wa ndani wa tumbo la chakula au sehemu ya mwanzo ya utumbo mdogo (duodenum). Vidonda hivi huanza pale sehemu ya ukuta wa ndani wa tumbo wenye ute na ambao hulilinda tumbo dhidi ya asidi au tindikali ya kumeng’enya chakula unapounguzwa na kusababisha asidi kuchubua na kuharibu sehemu ya ukuta huo. Vidonda vya tumbo hutibika kwa urahisi lakini ni hatari sana visipopatiwa matibabu haraka.
Alikumbusha kuwa chanzo ni asidi inayomwagwa kwa ajili ya kumeng’enya chakula. Asidi hii ni kali na isipodhibitiwa tumboni huleta madhara. Katika hali ya kawaida tumbo lina ukuta wa ndani ambao umejaa ute mzito unaozuia asidi isiunguze au kuharibu ukuta huo. Pia bacteria wa H.Pilori husababisha tatizo hilo Endelea na tiba…
MATIBABU
Matibabu hutofautiana kulingana na chanzo cha vidonda. Mara nyingi tiba hufanywa kwa kuandikiwa dawa na daktari lakini mara chache upasuaji unaweza kuhitajika. Ni muhimu kutibu vidonda vya tumbo mara tu vinapogunduliwa Kama una vidonda vinavyotoka damu kwa kawaida hali hii hulazimisha mgonjwa kulazwa kwa matibabu zaidi kwani muathirika anaweza kuhitaji kuongezewa damu.
Iwapo sababu ya vidonda vya tumbo itabainika kuwa ni bacteria wa H. pylori dawa ya kuangamiza bakteria hao ambayo ni ‘antibiotic’ hutumika.
Kwa vidonda vya tumbo vya kawaida daktari hutoa dawa zifuatazo; H2 blockers ambazo huzuia tumbo kuzalisha kiwango kikubwa cha asidi. Nyingine ni Proton pump inhibitors hutolewa kwa lengo la kusaidia kuzuia chembe hai zinazozalisha asidi.
Kadhalika wagonjwa hupewa Antacids ili kuwasaidia kuweka mazingira ya tumbo vizuri kwa kupunguza ukali wa asidi zinazozalishwa wakati wa kumeng’enya vyakula.
Wakati mwingine dalili za vidonda zinaweza kupotea mapema mara tu baada ya kuanza matibabu lakini, hata baada ya dalili hizo kutoweka mgonjwa anapaswa kuendelea kutumia dawa alizopangiwa na daktari.
MUHIMU
Hii ni muhimu sana kuzingatia iwapo chanzo cha vidonda kinakuwa ni bakteria. Daktari pia anamshauri mgonjwa aliye katika matibabu kutokutumia pombe, sigara, dawa au chakula chochote kinachoweza kuamsha dalili za vidonda. Vyakula hivyo ni pamoja na vile vyenye pilipili , vyenye uchachu kama ndimu na hata vinavyoungwa na nyanya nyingi.
MATIBABU YA UPASUAJI
Hutokea wakati mwingine vidonda vya tumbo vyenye hali ya hatari vikahitaji upasuaji. Kawaida operesheni hufanyika iwapo vidonda vinarudia mara kwa mara au haviponi, vinatoa damu, vinasababisha utumbo kulika kwa kukwangua ukuta wa tumbo au utumbo mdogo.
Upasuaji huhusisha mambo kadhaa kati ya yafuatayo; uondoaji wa kidonda chote, au kuondoa nyama sehemu nyingine ya utumbo na kuziba eneo lenye kidonda, na wakati mwingine kukata mawasiliano ya fahamu ya tumbo ili kupunguza uzalishaji wa asidi inayoleta athari hizo.
ATHARI
Ni muhimu kupata matibabu ya mapema iwezekanavyo mara tu baada ya kugundulika kuwa na tatizo la vidonda vya tumbo. Kadri vidonda vinavyoachwa na kukomaa bila kutibiwa ndivyo ambavyo huleta madhara makubwa zaidi baadaye.
Unapaswa kumtafuta daktari mara baada ya kupata mojawapo ya dalili zifuatazo; maumivu ya ghafla yanayokata ambayo hayakomi tumboni, kupata choo chenye rangi nyeusi au kilichochanganyikana na damu, kutapika damu au kutapika kitu kinachofanana na mbegu.
Dalili hizi mara nyingi ni kiashiria kikubwa kuwa kidonda kimemega sehemu ya ukuta wa tumbo au mshipa wa damu. Kupata ngozi ya kovu kwenye ukuta wa tumbo kunaweza kuwa tatizo jingine. Nyama hii inaweza kuzuia chakula kusogea kutoka tumboni kwenda kwenye utumbo mdogo. Hali zote hizi ni lazima zipate matibabu makubwa na mara nyingi mgonjwa anatakiwa kwenda hospitalini.
JINSI YA KUZUIA
Kikubwa ni kuzuia usambaaji wa bakteria na kupunguza uwezekano wa kuwapata. Hakikisha unanawa mikono kwa sabuni mara kwa mara. Halikadhalika kula chakula kisafi ambacho kimepikwa vizuri na kwa usafi kila mara.
Kuzuia vidonda vinavyosababishwa na matumizi ya dawa za kundi la NSAID,kama aspirin au ibuprofen au naproxen achana nazo au punguza matumizi yake. Kama unalazimika kuzitumia hakikisha unafuata na kuzingatia namna ulivyoelekezwa na daktari na epuka matumizi ya pombe wakati wa kutumia dawa hizi.
Baadhi ya tabia za kimaisha huweza kuzuia vidonda vya tumbo kutokea. Mambo haya ni kama matumizi ya pombe, sigara, bidhaa za sigara, pamoja na kuepuka msongo wa mawazo.Mambo yote haya husaidia kujenga ukuta wa tumbo imara na wenye afya pamoja na hivyo kuondoa uwezekano wa kupata tena vidonda vya tumbo.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








