Saleh Ahmada Juma( 28 ) amejiajiri kwa kufanya biashara ya kupika sambusa na udi kisha kuziuza katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar na kujipatia mapato ya kuendesha maisha yake.
Hatua hiyo inamfanya avuke kizingiti kilichobuniwa na baadhi ya watu kwamba baadhi ya kazi au biashara wanazigawa katika makundi ya za wanawake na wanaume hata kuwafanya baadhi ya vijana kuzidharau kwamba hawezi kuzifanya.
Saleh alichukua uamuzi huo baada ya kuona ajira ni chache katika sekta rasmi na kuamua kuendeleza ujuzi alioupata kutoka kwa wazazi wake ambao sasa wamefariki kitambo .
Akizungumza na mwandishi wa makala haya katika eneo lake la biashara mtaa wa Mwanakwerekwe,Zanzibar ambapo ndipo anaishi alisema kuwa biashara hiyo ilikuwa ikifanywa na wazazi wake kabla hawajafariki yaani walipika, kuuza sambusa na udi.
Sambusa ni kitafunwa maarufu Zanzibar hata nje na hutumika pia katika sherehe mbalimbali zikiwemo harusi.
Kijana huyo kwa sasa ndiye msimamizi mkuu wa biashara hiyo inayompatia kipato cha kuendesha familia.
“Tangu niwe msimamizi mkuu wa biashara hii ni muda wa miaka sita sasa. Awali biashara hii walikuwa wakifanya wazazi wangu lakini baada ya kuugua na kufariki mwaka jana nikaamua kuiendeleza kikamilifu,” alisema Saleh.
Sambausa anazopika na kuuza ni za aina tatu miongoni mwa huzo ni za viazi mbatata ambazo ni maalum kwa wananfunzi wa shule ambao huwauzia sh.100 kwa sambusa moja.
Pia anapika sambusa nyingine za viazi mbatata na vitunguu maji ambazo huuza katika migahawa .Bei yake ni sh. 250 kwa kila sambusa moja. Sambusa nyingine ni za nyama ambazo hupokea tenda kwa watu mbalimbali haswa wenye shughuli maalum ambazo huziuza sh. 400 kwa moja.
Mapato yanayotokana na mauzo ya sambusa hizo kwa jumla na rejareja huyatumia kwa mahitaji ya kununulia chakula nyumbani na kukamilisha mahitaji mengineyo yanapohitajika.
Biashara hiyo ya sambusa ina faida haswa kipindi cha harusi nyingi soko lake huwa zuri zaidi kwa wateja wake wengi kuzihitaji kwa ajili ya shughuli hizo.
Wakati mwingine hupokea tenda nyingi za kupika sambusa hata kulazimika kuzikataa kwa sababu ya muda kuwa sio rafiki wa kuweza kuchukuwa tenda za watu wengi zaidi na kuzitekeleza kwa wakati.
Kuhusu changamoto anazokabiliana nazo katika biashara hiyo ni kwamba, baadhi ya wateja sio waaminifu.
“Baadhi ya wateja hunipigia simu na kuniagiza niwatengenezee sambusa 100.Kwa kawaida huwa nagharamia kila kitu kwa kununua mahitaji ya kutengeneza sambusa kwa makubaliano kuwa nitalipwa baada ya kukamilisha kazi hiyo.Lakini cha ajabu anakuja anachukua sambusa lakini malipo yanakuwa ni shida sana au wakati mwingine haji kuuchukua mzigo baada ya kuutayarisha hivyo naingia hasara,”alisema Saleh.
Baadhi ya mahitaji ambayo hutumika kwa ajili ya utengenezaji wa sambusa ni nyama ya ng’ombe iliyosagwa, unga wa ngano, mafuta ya kula, viazi mbatata, vitunguu maji na viungo mbalimbali.
Biashara hiyo alisema kuwa ina kazi kubwa kuikamilisha kwani humlazimu kuifanya kuanzia saa kumi za alfajiri ili kuhakikisha kuwa analiwahi soko lake nyakati za asubuhi.
Matarajio yake Saleh anasema kuwa ni kuiboresha zaidi biashara hiyo ili awe anapata tenda ya kupeleka katika mahoteli makubwa ya kitalii hivyo kumfanya apate faida zaidi.
“Siwezi kukuambia kwa mwezi naingiza kiasi gani kwa sababu fedha ninayoipata mara nyingi nailekeza katika mahitaji ya chakula cha kila siku hapa nyumbani hivyo inakuwa vigumu kujuwa kipato ninachokipata.Lakini nashukuru napata fedha ambazo zinanisaidia kuihudumia familia yangu”alisema.
Kama hiyo haitoshi, Saleh pia anafanya biashara ya kupika udi na kuuza,na kwamba biashara hiyo imekuwa ikimpatia ujira na kuondokana na hali ya utegemezi kutoka katika familia yake.
Udi ni aina ya urembo wenye harufu nzuri ambao huchomwa kisha harufu yake husambaa ndani ya nyumba au kwenye nguo na harufu yake hutoa msisimko wa haiba nzuri katika nyumba.
Alisema udi anaoupika huuza kwa jumla na rejareja. Wateja wake huwa ni kutoka Zanzibar na Tanzania bara. Plasitiki huuza kati ya sh. 500 na 1,000 kwa kuwekwa katika vikopo maalum.
Miongoni mwa zana zinazotumika kwa ajili ya utengenezaji wa udi ni sukari guru,mchanganyiko wa mafuta mazuri na liwa.
Kwa sasa alisema, malighafi ya liwa imekuwa adimu kupatikana Zanzibar kwa sababu miti mengi inayotoa liwa inatoweka kwa sababu ya ukataji wa miti ovyo. Mazingira hayo yanalazimisha malighafi hiyo kuagizwa kutoka Tanga- Tanzania bara.
Saleh ana elimu ya kidato cha nne aliyohitimu mwaka 2008 katika Shule ya Sekondari Tumekuja mjini Zanzibar. Alisema anachukizwa na tabia ya baadhi ya vijana kuchagua na kudharau kazi kama biashara anazozifanya sasa baadhi ya vijana wanazichukulia kuwa ni za wanawake.
Aliwataka vijana wenzake waachane na mawazo hayo mgando na badala yake wasichague kazi na kujiajiri ili waweze kujiepusha kufanya mambo yasiyofaa ambayo hayana faida kwao.
Alisema baada ya kumaliza kidato cha nne alama alizopata hazikumuwezesha kuendelea na elimu ya juu licha ya kutamani sana kuendelea na elimu.Kikwazo kingine ni wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kifedha pia walikuwa wagonjwa wasiojimudu.
Saleh siku si nyingi zijazo anatarajia kufunga ndoa na kuishi maisha mapya ya ndoa.










