Eco Energy ilipewa hati miliki ya eneo hilo kwa ajili ya mradi wa miwa wenye ukubwa wa hekta 20,000, ambayo inalalamikiwa ilikuwa tayari inalimikiwa na hifadhi hiyo.
Kipande kinachomilikiwa na Hifadhi ya Saadan, ambacho Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilitoa kwa Ecoenergy, ina ukubwa wa hekta 3441 na ndicho kilichopo katika mgogoro huo.
Sambamba na hilo, wametaka ofisa aliyehusika na utoaji wa hati ya eneo hilo kwa mwekezaji, achukuliwe hatua za kisheria, ili kukomesha tatizo la watendaji wanaozua migogoro ya ardhi nchini.
Mwenyekiti wa Kamati,Atashasta Nditiye, alitoa maazimio ya kamati hiyo mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhandisi Ramo Makani, aliyeambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Meja Jenerali Gaudance Milanzi,
WABUNGE ZIARANI SAADANI
Nditiye, anasema haiwezekani mwekezaji kuuziwa eneo ambalo tayari ni hatimiliki ya hifadhi, kitendo kilichozua mvutano.
Ziara yao ya siku moja ilikuwa na lengo la kuipa kuielimisha kamati shughuli zinazofanywa na Shirika la Hifadhi za Taifa ya (TANAPA), kupitia Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Mwenyekiti huyo wa Kamati, anasema hakuona sababu ya serikali kutoa hatimiliki kwa kampuni ya Eco Energy kumiliki eneo, wakati tayari liko chini ya milki ya hifadhi.
“Suala hilo nitamuaambia Waziri (William) Lukuvi aangalie namna ya kulipatia ufumbuzi, lakini kubwa zaidi ni kufuta hatimiliki ya eneo hilo kwa sababu haiwekani mwekezaji akaingia ndani ya sehemu za hifadhi ambazo zipo kisheria,”anasema.
Pia anawataka watendaji wa serikali kuwa makini wakati wa kuuza maeneo yanayopakana na Hifadhi za Taifa, ili kuepusha mivutano isiyokuwa ya lazima, inayoweza kutokea na kuathiri shughuli za hifadhi nchini.
“Haiwezekani ofisa ardhi, kuuza eneo juu ya hati nyingine. Hivyo, tunaomba aliyehusika na sakata la uuzaji mara ya pili achukuliwe hatua, kwa sababu haiwezekani jambo hilo litokee na sisi kama kamati tunalifumbia macho,”anasema mwenyekiti.
Nditiye anaongeza:”Sisi kama kamati, tumuagize Waziri Lukuvi kuwachukulia hatua kali maofisa ardhi waliopo kwenye ofisi yake, waliohusika, kwa lengo la kukomesha tabia za wawekezaji kuvamia maeneo ya Hifadhi za Taifa.”
Hatua hiyo inatokana na kauli iliyotolewa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani,Dk.James Wakibara alyetaja changamoto inayowakabili ni kitendo cha mwekezaji wa shamba la miwa kupewa sehemu ya ardhi wanayoimiliki.
Mjumbe wa Kamati hiyo,Shabani Shekilindi, naye anaunga mkono kupinga hifadhi kuvamiwa na serikali nakaa kimya.
“Suala la mwekezaji kuvamia eneo la hifadhi kwa kupewa ridhaa ya kufanya shughuli zake, siyo kitendo cha kuvumiliwa.
“Hivyo, tunaomba waliohusika kutoa vibali washughulikiwe ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo,” anasema Shekilindi, ambaye ni Mbunge wa Lushoto.
UPEKEE WA SAADANI
Upekee wa Hifadhi ya Taifa Saadani, unatokana kupakana na sehemu ya bahari ya Hindi inayokutana na nchi kavu, huku kukiwepo viumbe na mimea adimu, ikiwemo misitu ya ukanda wa chini wa Pwani ya Bahari.
Hifadhi ya Taifa ya Saadani, ilianzishwa mwaka 2005na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali ambalo liliipandisha hadhi kutoka Pori la Akiba la Saadani kuwa Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Mchakato huo ulijumuisha kuongeza, mipaka inayowezesha wanyamapori kupata eneo kubwa zaidi la makazi na malisho.
Hifadhi hiyo ina upekee kutokana na kuwa na samaki aina ya Kamba Mti waliokuwa maarufu kama zao la biashara nje ya nchi na kulipatia Taifa fedha za kigeni kati ya mwaka 1988 na 2004.
Tangu mwaka 2004 hadi sasa, serikali imeufunga uvuvi wa kutumia m katika ukanda huo kwa sababu rasilimali ya kamba mti haijaongezeka kwa kiwango cha kuridhisha .
Eneo la Saadani ni muhimu kwa ajili ya uhifadhi wa viumbe baharini waliopo hatarini kutoweka, ikiwemo Kasa wa Kijani na katika ulinzi wao, Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia mkataba wa kimataifa.
Pia, eneo la Saadani ni muhimu kwa uhifadhi wa matumbawe ambayo ni makazi na mazalia ya samaki.
CHANGAMOTO
Changamoto zinazoikabili Hifadhi ya Taifa Saadani, ni Ikolojia ya muundo wa hifadhi hiyo, kwani eneo lake kiikolojia inalaezwa imekaa vibaya, kwani ni dogo.
Ina eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,100, hali inayolazimu idadi kubwa ya wanyamapori kuwa nje ya eneo la hifadhi kwa muda mrefu, kwa sababu mahitaji yao muhimu na hasa malisho yanapatikana huko.
Mtawanyiko wa wanyamapori kwenda nje ya hifadhi inaleta changamoto ya ulinzi wa wanyamapori, wakiwamo tembo jike, ambao hutumia miezi sita kwa mwaka kupata malisho.
Hiyo zaidi huwa katika vipindi vya masika ambavyo wanyamapori wengine kama vile Swala wakitumia maeneo hayo wakati wa kiangazi.
Pia mtawanyiko huo wa wanyamapori, unasababisha ongezeko la migongano ya wananchi na wanyamapori kama tembo na Simba ambao, hula mifugo na kuhatarisha usalama wa maisha ya watu.
ENEO LA MGOGORO
Eneo lenye mgogoro ni asilimia 10 ya eneo lote la Hifadhi ya Taifa ya Saadani. Mgogoro huo baina ya hifadhi na mwekezaji wa Eco Energy, ana lengo la kuanzisha shughuli za kilimo cha miwa, ili kuzalisha nishati ya umeme na kuzalisha sukari.
Eeno hilo limeenda sambamba na ukanda wa chini wa Mto Wami ambao ni mhimili na uhai wa hifadhi, kwani katika majira yote, wanyama hupata makazi na malisho kutokana na uoto wa asili kwenye eneo hilo, ambalo ni mfumo wa asili wa kiikolojia.
Eneo hilo ni maalum kutokana na mdomo wa mto Wami kuingia katika ardhi oevu, ambayo ni muhimu kwa ustawi wa mimea mbalimbali.
Aidha, mwingiliano wa maji ya bahari na mto Wami hutengeneza muungano wa tabia ya ujumla ya mazingira ya kipekee na kufanya makazi na mazalia ya viumbe maalum ikiwemo Kamba Mti.
Kuanzishwa kilimo cha Miwa, kunaelezwa kutatoa mwanya wa kuvutia ongezeko la hatari ya shughuli za binadamu na uvamizi wa ujenzi wa makazi ya watu ikiwemo nyumba za biashara.
Eneo hilo linaelezwa kuwa muhimu kwa mtawanyiko wa wanyamapori, mazalia na mapito ya wanyama.
MALENGO YA HIFADHI
Lengo kuu lilikuwa kuhifadhi maeneo muhimu kwa mtawanyiko wa wanyamapori, eneo la mazalia na mapito ya wanyama, kuhifadhi eneo la mazalia ya Kasa Kijani .
Pia maeneo hayo yanaelekeza kulinda na kuuhifadhi Mto Wami, ambao ni mazalia ya samaki na malisho ya ndege wanaohama.
Malengo mengine ni kulinda na kuhifadhi Tembo wanaohama kutoka hifadhi jirani za Selous, Mikumi, Wami na Mbiki.
Pia inalinda na kuhifadhi matumbawe na kuongeza ulinzi wa mimea aina ya Acacia Zanzibarica ambayo ni makazi muhimu ya Mbega Mweusi na Mweupe.
UMUHIMU KATIKA UTALII
Kwa mujibu wa Mpango wa Menejimenti ya Shirik la Hifadji ya Taifa(TANAPA) - 2010-2020, Hifadhi ya Taifa Saadani imepanga kuongeza vitanda vya wageni kutoka 315 vya sasa hadi 690.
Idadi ya watalii wanaotembelea Saadani imeongezeka kutoka 3,540 katika msimu wa mwaka 2007/08 hadi watalii 15,855 mwaka 2013/14.
Pia, mapato yameongezeka kutoka Sh. milioni 116.4 mwaka 2007/8 hadi Sh. milioni 653.8 mwaka 2013/14.
Hiyo ni ongezeko la asilimia 462 ndani ya kipindi huku katika dira ya kuelekea mwaka 2025, watalii wanaotarajiwa kuzuru Sadani wataongezeka maradufu na kufikia 100,000 kwa mwaka.
Taarifa ya hifadhi inaeleza kuwa mapato yatokanayo na huduma za kitalii hutumika kusimamia shughuli za uhifadhi, ikiwamo kudhibiti ujangili na kutekeleza miradi ya ujirani mwema na jamii inayozunguka hifadhi.
Hifadhi pia inachangia miradi ya kuondoa umaskini, hasa kwenye vijiji vinavyoizunguka hifadhi kupitia mikakati ya ujirani mwema.
Kupitia mikakati hiyo, miradi imejenga miundombinu kama vile shule ya sekondari, jengo la utawala la kijiji, pampu ya umwagiliaji maji kwa kikundi cha kinamama cha kijiji cha Matipwili.
Pia kumefanyika ujenzi wa nyumba mbili za matabibu na nyumba moja ya mwalikatika kijiji cha Saadani.










