Siasa hizo zimeshamiri na kushika kasi baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana kwa chama kikuu cha upinzani (CUF), kususia na kueleza kutoridhishwa na hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha, kufuta uchaguzi huo.
Kutokana na kuwapo kwa hali hiyo ya ubaguzi miongoni mwa Wazanzibari kutokana na itikadi za kisiasa, kumekuwepo na utoaji wa huduma za biashara kwa ubaguzi haswa kisiwani Pemba.
Hata hivyo, Serikali ya Zanzibar imetishia kuwanyang’anya leseni wafanyabiashara wanaotoa huduma hizo kwa ubaguzi kutokana na itikadi za kisiasa.
Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba, Omar Khamis Omar na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwajuma Majid Abdallah, wanasema tangu kumalizika kwa uchaguzi wa marudio Zanzibar kumekuwapo na ubaguzi wa utoaji huduma wa biashara na usafiri kisiwani Pemba.
omar anasema kutokana na hali hiyo, wamewapa agizo wafanyabiashara wote wenye maduka na vyombo vya usafiri kuacha kutoa huduma kwa ubaguzi au watawanyang’anya leseni za biashara zao.
Anasema wamekuwa wakipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuwa wanabaguliwa katika upatikanaji wa huduma hizo.
Anasema walikuwa wakienda dukani kununua bidhaa walikuwa wakiangaliwa vidole na wakibainika kuwa kidole kinawino ambao huwekwa baada ya kupiga kura huwa hawawapi huduma na wakati mwingine hushushwa katika vyombo vya usafiri kama gari za abiria,” anasema Omar.
Aidha, anasema kila mtu ana haki ya kuchagua chama chochote cha siasa na kupiga kura katika uchaguzi huo isiwe sababu ya kutengwa na kukoseshwa huduma muhimu.
“Haki ya kupiga kura ni ya kidemokrasia hivyo wale ambao waliitumia haki yao Machi 20 wasibughudhiwe na wale ambao hawakuitumia haki yao hiyo…wote wawe wanapewa haki na fursa sawa,” anasema Mawajuma Majid, RC wa Mkoa Kusini Pemba.
Nao Masheha ambao ni viongozi wa kata wa Sheia za Kojani na Makangale, kisiwani Pemba wanasema baada ya kujitokeza kwa hali hiyo tayari wameshawapa taarifa wafanyabiashara wote katika Shehia zao kuacha mara moja ubaguzi ambayo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Hamad Ali Jakani Sheha wa Shehia ya Kojani, anasema kisiwa cha Kojani kimezungukwa na bahari hivyo wananchi wake wanatumia usafiri wa majahazi kutoka eneo moja kwenda jingine, hivyo ilifika wakati wananchi ambao wanamrengo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walikuwa wakibaguliwa na kutopatiwa usafiri huo.
Aidha, anasema pia ubaguzi ulikuwapo katika utoaji wa huduma za mahitaji ya vyakula madukani na watu waliopiga kura kwenye uchaguzi wa marudio Machi 20, mwaka huu walikuwa wakinyimwa huduma hiyo licha ya kuwa wana fedha za kununulia bidhaa wanazozihitaji.
Hata hivyo, anasema hali hiyo kwa sasa imeanza kupungua ingawa baadhi ya wafanyabiashara wanafanya ubaguzi huo kimya kimya ili wasigundulike.
Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Makangale Mohammed Juma Ali, anasema katika Shehia yake kulikuwa na ubaguzi wa kutoendeana harusini kutokana na itikaddi za kisiasa zilizopo kisiwani Pemba.
“Ilifika wakati mwanachama wa CCM akiwa na harusi nyumbaani kwake akialika weziwe ambao ni CUF hata kama ni jamaa basi walikuwa wakiisusia harusi hiyo kisa uchaguzi,” anasema Shekha huyo.
Hali hiyo Kisiwani Pemba ambako ni ngome ya CUF kumezuka tabia hiyo ya ubaguzi kutokana na wafuasi wa CUF kutoridhishwa na uamuzi wa Jecha kufuta uchaguzi Oktoba mwaka jana.
Mwenyekiti huyo alifuta uchaguzi huo kwa madai kuwa haukua huru na haki kisha kutangaza tarehe ya marudio ya uchaguzi huo ambao ulifanyika Machi 20 mwaka huu.
Uchaguzi huo wa Machi 20 Chama kikuu cha upinzani Zanzibar CUF kilisusia uchaguzi huo ambapo licha ya kutoshiriki kwake, lakini kilipa kura 6,076 sawa na asilimia 1.3.
katika uchaguzi huo, Dk. Ali Mohammed Shein, ambaye alitangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi kwa kupata kura 299,982 sawa na asilimia 91.4.
Licha ya ushindi wa urais, lakini CCM ilipata ushidi kwa majimbo yote 54 ya Zanzibar, ikiwa ni mara ya kwanza tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.
Wakati hali ikiwa hivyo, Pemba, kisiwani Unguja, na hususani Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja, matukio ya uchomaji moto ya nyumba za makazi ya wananchi yamekuwa wakitokea mara kwa mara.
Hali hiyo inatokana na siasa za chuki na uhasama kati ya wafuasi wa vyama vikuu vyenye upinzani mkali CCM na CUF.
Kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana zaidi ya matukio manane ya uchomaji moto wa nyumba za makazi ya wananchi katika kisiwa hicho yametoke na kuripotiwa Polisi.
Kwa mfano kijiji cha Tumbatu Gomani ni ngombe ya CCM na Tumbatu Chwaka ni ngome ya CUF na hujitokeza hitilafu mbalimbali za uvunjifu wa amani katika vijiji hivyo kutokana na siasa za chuki na uhasama kwa wananchi hao kulipizana visasi.
Hivi karibuni baada ya uchaguzi wa Machi 20, nyumba nne zilichomwa moto na mbili kubomolewa na watu wasiojulikana katika kisiwa Tumbatu Chwaka.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa Tumbatu wanasema kuwa vitendo hivyo vinaendelea kujitokeza kutokana na kutochukuliwa hatua kali kwa wahusika wa matukio hayo.
Wanasema endapo jeshi la polisi litafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kulinda raia na mali zake itasaidia kuondoa matukio hayo ambayo yamekuwa yakileta athari kwa wananchi.
“Tunaliomba jeshi la polisi lisifanye kazi kwa upendeleo na lihakikishe linafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria bila ya kuegemea upande wowote wa chama,” anasema Machano Haji, ambaye nyumba yake imechomwa moto hivi karibuni.
Aidha, wananchi hao wanasema kuwa wahusika wa matukio ya ubomoaji nyumba, uchomaji moto kwa nyumba za wananchi, maskani za vyama pamoja na utiaji alama ya x kwa nyumba katika kijiji hicho yanazidi kuwatia hofu na kuishi kwa wasiwasi.
Kamanda wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Hassan Msangi, anasema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini wahusika wa matukio hayo na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, Machi 31 majira ya saa saba usiku nyumba nne zilitiwa moto na watu wasiojulikana katika kijiji cha Tumbatu Chwaka shehia ya Tumbatu Gomani na nyumba mbili zimebomolewa na watu wasiojulikana.
Aidha, anasema jeshi hilo halifanyi kazi kwa upendeleo na linafanya kazi kwa mujibu wa sheria hivyo aliwataka wananchi kuishi kwa upendo na kutii sheria bila ya kushurutishwa.
Anawataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi katika kuwafichua wahalifu wa matukio mbalimbali ili jeshi hilo liweze kufanyakazi zake kwa ufanisi.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Omar Makame anasema Zanzibar ipo shwari na hali ya amani na usalama imezidi kuimarika na wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaeleza uhasama na chuki kurejea visiwani humo, licha ya kwamba makaratasi ya ZEC yanaonyesha CCM inakubalika kwa asilimia 90.










