RAIS wa Palestina, Mahmoud Abbas, hatimaye amejikuta akiweka bayana kwamba anafanyia kazi uwezekano wa kuzuia mashambulizi ya visu ya Wapalestina na machafuko mengine ya mitaani dhidi ya Israel.
Kiongozi huyo kadhalika alitoa ofa ya kukutana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kurudisha tena juhudi za kupatikana kwa amani.
Kauli zake hizo zimeonekana kuwa juhudi za Abbas anayeungwa mkono na Magharibi kuigeuzia kibao Israel, ambayo imekuwa ikimuelezea kama anayehusika na mkwamo wa kidiplomasia kwenye eneo hilo na ongezeko la umwagaji damu.
Akizungumza juzi na Televisheni ya Channel 2 ya Israel, Abbas alitoa maelezo nadra kusikika kuhusiana na mikakati ya usalama wa ndani, suala nyeti ambalo Wapalestina wengi wanachukulia hatua kama hiyo ni kushirikiana na adui.
"Majeshi yetu ya usalama yanakwenda kwenye shule na kupekua mikoba ya wanafunzi na kuona kama wana visu. Nyie hamjui hilo," alisema juzi.
"Kwenye shule moja, tulikuta wavulana na wasichana waliokuwa wamebeba visu. Tulichukua visu hivyo na kuzungumza nao na kusema: 'Hili ni kosa. Hatutaki wewe uue au uuawe. Tunataka uishi na upande mwingine waishi vile vile.'"
Utawala wa Abbas na Israel wanaratibu suala la usalama kwenye maeneo yanayokaliwa ya Ukingo wa Magharibi pamoja na kukwama miaka miwili iliyopita kwa majadiliano yaliyokuwa yanafadhiliwa na Marekani juu ya taifa la Palestina.
Netanyahu anasema yuko tayari kuanza tena mazungumzo na kwamba Abbas ndiye ambaye amekuwa akikwepa suala hilo huku akichochea machafuko kwa kauli zake dhidi ya Israel.
Lakini Abbas aliieleza Channel 2 kwamba jukumu lilikuwa kwa Netanyahu.
"Nitakutana naye, wakati wowote. Na kwa hali hiyo, napendekeza kwake kukutana," kiongozi huyo wa Palestina alisema.
Alipoulizwa nini kilichotokea kwenye pendekezo hilo, Abbas alisema: "Hapana, hapana – ni siri. Anaweza kukueleza wewe kuhusiana na hilo."
Hata hivyo, ofisi ya Netanyahu haikuwa na jibu la mara moja kuhusiana na hilo.
Tangu Oktoba mwaka jana, matukio ya Wapalestina kuchoma visu, kugonga na magari na kuvizia kwa risasi yameshauaWaisrael 28 na Wamarekani wawili.
Wakati huo huo, Wapalestina takriban 190, kati yao wakiwemo 129 ambao Israel inasema walikuwa wanafanya mashambulizi, wameshauliwa na majeshi yake. Wengi wao wakiwa wamepigwa risasi kwenye mapambano.
Mamlaka ya Palestina ya Abbas inaendesha utawala wake yenyewe kwenye Ukingo wa Magharibi chini ya makubaliano ya muda ya amani ya mwaka 1993.
Majeshi ya Israel hivi sasa yako huru kufanya shughuli kwenye maeneo ya mamlaka ya Palestina. Na Abbas anasema yuko tayari kuchukua hatua dhidi ya Wapalestina ambao intelijinsia ya Israel inawachukulia kuwa tishio.
"Kama yeye (Netanyahu) ananipa jukumu na kuniambia kwamba anaamini kwenye suluhisho la uwepo wa mataifa mawili na tunakaa kuzunguka meza na kuzungumzia kuhusu suluhisho la mataifa mawili, hilo litawapa watu wangu tumaini, na hakuna ambaye atathubutu kwenda na kumchoma mtu kisu au kumpiga risasi au kufanya chochote hapa au pale," Abbas alisema.
Netanyahu ameshasema atapendelea kuundwa kwa taifa la Palestina iwapo tu masharti ya Israel yatatekelezwa kama vile mahitaji ya usalama wake.
Suala la kama Abbas anaweza kuingiza Ukanda wa Gaza ni la kutilia mashaka, kwa vile upande huo uko chini ya udhibiti wa wapiganaji wa Kiislamu wa Hamas ambao wanapinga kabisa uwepo wa Israel.
Na kwa upande wake, Netanyahu hajaweka wazi kama ataondoa makazi ya Wayahudi huko Ukingo wa Magharibi kuwapisha Wapalestina.










