Kauli ya serikali inahitajika kwa watoto, wazee , wanawake, wafanyakazi na umma wa wanafunzi unaosota barabarani kwenda shuleni au vyuoni, kwa vile wengi kama Rais alivyosema maisha yao ni kama ya ‘mashetani, wanaoteseka na moto wa jehenamu.
Inauma mno wauguzi wakifikiria kuwa wanaoingia kazini saa 2:00 asubuhi hadi saa 9:00 jioni kila siku na pia hufanyakazi zamu za usiku wakishinda wamesimama kutwa na kukesha usiku kuhudumia wagonjwa lakini mwisho wa mwezi mshahara haufiki hata Shilingi 1,000,000.
Hawa hawana pesa za vocha, nauli, posho ya pango, chakula wala safari ya kwenda mkoani ama motisha nyingine mbali na kuchoma sindano, kufunga vidonga, kutoa dawa na kuambukizwa magonjwa kama kifua kikuu, VVU, homa ya ini hata ebola na dengue wakati mwingine. Wanatamani sana kauli ya serikali kuwalipa mishahara minono.
Wako ‘mashetani wengine wa vichwa saba na jicho moja’ ni polisi. Wanafanyakazi katika maeneo hatarishi, kulinda benki, kukesha kwenye nyumba za viongozi, kuweka doria usiku wa manane huku wakiwindwa na majambazi kwa kila namna ili wachukue silaha zao. Wangetamani kulipwa kwa Dola ili Shilingi ikiyumba wasiathirike.
Hawa mishahara yao ni ‘kuduchu’ ndiyo waliostahili kulipwa milioni 40. Polisi wangapi waliuawa na hakuna kinachoendelea? Wakurugenzi wangapi na watendaji wakuu wa mashirika walishawahi kupigwa shaba? Inakuwaje polisi wanaosota kiasi hiki juani waambulie chenji? Huku wakurugenzi wanaowalinda wakila milioni 40 ndani ya viyoyozi?Inaamaanisha kuwa kila mwaka wanakomba milioni 500 usawa wa nusu bilioni! Hakika ni malaika walio peponi.
Kwa taarifa yao wakurugenzi wengine ni mbumbumbu walipewa vyeo kwa urafiki hawafahamu lolote, hawaendeshi shirika wala kampuni kwa bongo zao lakini wanaondoka na milioni 40 , pamoja nazo wana vocha karibu Shilingi 1,000,000, posho ya kukarimu (entertainment) , wanatumia magari ya shirika na kugarimiwa kila kitu.
Wanaishi nyumba za shirika ambazo hugaramia chakula, ulinzi, wahudumu na juu ya hayo ana safari za ng’ambo kwa ajili ya mapumziko na faragha.
Hana muda wa kuingia kazini anaweza kuonekana ama asionekane. Hana kazi za usiku kama wauguzi, halazimika kushiriki paredi ya kukabidhi silaha na risasi. Kwa ujumla ana washauri wengi na kazi zake si nyingi kama ilivyo kwa wauguzi, walimu, polisi na mahakimu.
Wakati watu wanapotafakari malipo ya Shilingi milioni 40 kwa wakurugenzi na watendaji wakuu wa asasi za umma, hivi ndivyo hali ilivyo kwani wapo baadhi ya wanaotaka kupata hata Shilingi 10,000 kwa siku lakini wanatoka tupu nao ni Wamachinga.
Siyo siri wanashinda kwenye vumbi, jua linawawakia kuanzia utosini hadi mguuni. Wanauza maji barabarani, korosho, karanga, soda, kila gari linalopita Ubungo ni wa kwanza kuliona. Mabasi yanayokwenda mikoani yanapoingia Chalinze, Morogoro, Dodoma na Arusha ndiyo wanaowakaribisha abiria.
Si hao tu wapo wanafunzi wanaotembea barabarani vumbi linawafunika machoni, miguuni na mapafuni wanapiga chafya muda wote ni kwa sababu hawana usafiri.
Kazi yao ni kusoma magari ya wenzao wa shule za ‘academy’gari lile ni la Queens Land School Bus, Cherub School Bus, hakuna gari lililoandikwa Mzimuni au Darajani ama Mawenzi School Bus. Hawa ndiyo wanafunzi wa Tanzania mvua ikinyesha matope yanawaremba. Yanarushwa na waendesha bodaboda, magari na baiskeli hii ni mahususi kwa wanaoishi mijini na majijini.
Kwa walioko vijijini wanaoga kwenye utelezi, kulowana tope na maji wanapovuka mito na makorongo yanayozunguka shule. Hawa ndiyo wasomi watakaoleta mapinduzi kama yale yanayoendelea China na kuipaisha kuwa taifa lenye nguvu ya uchumi mkubwa duniani pamoja na teknolojia katika karne ya 21.
Polisi wa usalama barabarani wanasubiri serikali itamke neno la kuwabariki. Hawana sehemu ya kujificha kukwepa mionzi ya jua inayoelezwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa kuwa inatisha kwani joto limeongezeka. Kwa taarifa yao watarajie kuwa na magonjwa yanayoletwa na sumu za moshi wa injini mbalimbali kuanzia bodaboda , magari hadi baiskeli.
Wakati yanazungumzwa maghorofa na majumba ya kisasa wanayomiliki wakurugenzi na maofisa wakuu watendaji mathalani kinatajwa kijiji cha kiongozi wa umma mwenye nyumba 72 , huko Kanda ya Ziwa wanawake wazee tena wagonjwa wanachinjwa kama kuku.
Maskini hawa hawana mahala pa kujificha kwa vile hawana nyumba. Wakisingiziwa uchawi ni rahisi kuwachomoa kwenye vibanda vya tembe ama vya matope vilivyoezekwa na nyasi na kuwapiga mapanga kwa vile hawana tofauti na wanyama kwani hata wao huishi nje ni kama ndama zizini hakuna wa kuwatetea.
Wako wazazi na watoto wachanga wanaozaIiwa kwa mwanga wa tochi za simu hakuna dakatri kwenye kituo cha afya wala kwenye zahanati. Lakini , kikali zaidi wanalala chini ya au kwenye kitanda chenye godolo chafu lisilokuwa na shuka . Wanajifunika na vitenge na kanga zao. Huko hakuna chandarua.
Mbu wanauma ngozi zao dhaifu na kujichana kwa damu za mama na watoto ambao wanaumwa ‘anemia’ kwa kuwa asilimia kubwa ya vifo vya wazazi na watoto nchini inaletwa na upungufu wa damu. Khee mbu anawaongezea malaria ambayo imewatesa na mtoto mgeni aliyeingia kwa mara ya kwanza duniani, analakiwa na malaria.
Serikali inaonyesha vipi kuwajali hawa mafukara? Taifa linaonyeshaje mshikamano na watu maskini? Walio kwenye lindi la njaa, magonjwa na kifo kikiwanyemelea muda wote? Linashikamanaje na watoto ambao hawatakua kwa utimilifu kwa kimo wala kwa akili hawa ni wale ambao wamedumaa?
Watoto ambao mifupa yao itaharibika au kitaalamu itakuwa ‘deformed’ kwa sababu ya utapiamlo, ambao hatma yao imeporwa na njaa, uchaji wa akili zao umetoweka na wataishia kuwa punguani, hata wakiwa darasani hawataelewa kitu hata kama ni kuandika na kusoma majina yao?
Wapo wanaohoji uko wapi mshikamano wa serikali na wale ambao maisha yao yanapotea wakiwa wadogo kwa kukosa maji wakaishia kufa kwa magonjwa ambayo yanatibika kama kuhara damu, kipindupindu, kichomi (naimonia) na maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), hawa taifa linashikamanaje nao?
Taifa litaonyeshaje mshikamano kwa wanawake wanaoshindwa kuwazika watoto wao kwa sababu ya udhaifu walio nao kwani wana Virusi Vya Ukimwi (VVU) na hawajapata dawa za kupunguza makali ya virusi za ARVs na kibaya zaidi hawana chakula wala msaada?
Serikali inabebaje jukumu la kuwasaidia wanaoishi kwenye mazingira magumu, kama yatima, wale wanaolala mitaani, wasiosoma, mabinti wanadhalilishwa kingono na wazazi na jamaa zao, wasichana wa shule wanaoozwa na kuzaa utotoni?
Watanzania karibu wote wanaishi kama ‘mashetani’, japo wapo wanaosema kukata mshahara wa mtu ni kosa kisheria, kuna uwezekano kuwa maagizo yakitolewa na Rais kuwa watapunguziwa mishahara ni sahihi kwa vile ndiye muajiri wao.
Rais kama mwajiri anayo mamlaka ya kuwafukuza na kuajiri wengine ambao anaweza kuwalipa fedha zinazolingana na hali halisi badala ya kuendelea kutengeneza pengo kubwa la maskini na matajiri wa kupindukia ndani ya taifa fukara kama hili. Cha kusikitisha pengo la mafukara na mabilioni linapanuliwa na mapato ya utumishi wa umma.
Watanzania wengi wanalia hali ni mbaya, lakini sasa wanaanza kufurahia na wana kila sababu ya kusherehekea ahadi ya kupunguza mishahara minono ya milioni 40 kwa mwezi wanayokula watendaji wakuu na wakurugenzi. Wanachekelea kibano cha wafanyakazi hewa ambacho kitaokoa mabilioni.
Wanafurahia kugawana mabilioni ya fedha za kigeni yanayoliwa kwa safari za ng’ambo yakibakia hazina ili kugawana na wengine ambao ni ‘mashetani’ wanaowalisha malaika.Kauli za kuwajali wasio nacho zinaonyesha mshikamano wa kujali na kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.
Ikiwezekana Rais aendelee kuangalia maeneo mengine hata ikibidi kutembelea mishahara ya wabunge, mabalozi, majaji na hata viongozi wastafu.










