Hivi ndivyo rangi ya kijivu inavyopendezesha makazi

02Apr 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Hivi ndivyo rangi ya kijivu inavyopendezesha makazi

PENGINE ni mmoja wa wale wanaodharau rangi ya kijivu ikichukuliwa kuwa si mali kitu , ni ile inayopakwa kwenye maeneo kama kuta za viwandani, mahospitalini, shuleni na zile sehemu ambazo hazina sababu ya kuzipendezesha.

Umekosea. Kwa taarifa yako hii moja ya rangi ‘bomba’ na kama unafahamu namna ya kuitumia hakika utaipenda.

Wengi hawafikirii kuwa rangi hii inaweza kupamba nyumba na ikavutia mno. Aghalabu kijivu kinaendana na mazingira na kuna njia nyingi unazoweza ukaitumia kupendezesha nyumba bila kuzidisha au kuigeuza kama eneo lililofifia. Vilevile rangi hii ni murua kupakwa nje na ndani ya nyumba.

Rangi ya kijivu ina jamii kadhaa ndani yake, unaweza kuamua unayotaka kuna nyingine zinaelekea kufanana na moshi wa taka zinazochomwa, ipo inayoweza kuchosha na pia kuwa na muonekano wa maeneo ya biashara zaidi kuliko nyumbani. Fikiria chumba chenye kuta za rangi ya kijivu kinakuwa kama stoo au gereji ambako mvuto sio kigezo muhimu mahali hapo.

Habari njema ni kwamba kuna jamii nyingi za rangi ya kijivu ambazo zinakuja kwa kasi na zina muonekano wa kuvutia mno. Kijivu chepesi ukutani kwa mfano, ni rangi ambayo haiwezi kupitwa na wakati. Ukiipaka unaweza kuweka vifaa au samani zenye kijivu kizito mathalani zulia au sofa ili kuleta mchanyato wa kupendeza kati ya rangi mbili hizi za kijivu.

Kijivu chepesi pia kinaendana na rangi nzito kama vile rangi za kahawia, njano ya dhahabu na damu ya mzee ambayo pia inaitwa burgundy. Rangi hizi zinashirikiana kwa uzuri na kijivu chepesi na unaweza kuzitumia kwenye pazia na vitupio vya mapambo kama vile, mito, michoro ya ukutani na fremu za picha.

Kero na raha za rangi hii ni kwamba inapendeza zaidi ikikaa kama background na pia ikionekana kwa wingi. Kwa hivyo kama kuna samani au kitu unachotaka kiwe kvutia chumba basi paka ukuta kijivu chepesi au kuwa na zulia la kijivu nzito. Vile vitu vikubwa vikubwa vipe rangi ya kijivu, kwa mfano sofa ziwe za kijivu. Rangi hii ni nyepesi kutazama machoni na hufunika rangi nyingine. Kwa hivyo endapo una vitu unavyotaka viwe vya kukifanya chumba kivutie paka kuta kijivu ili zionekane kirahisi.

Kwa hivyo kama unataka kutumia rangi hii lakini hupendi nyumba yako ionekane kama godown au chumba cha daktari tumia kile chepesi ukutani ukichanganya na vitupio vyenye rangi nzito. Huku ukiambatanisha kijivu kizito kwenye zulia.

Kwenye rangi za jamii ya kijivu unaweza kupata yoyote kuanzia nyepesi inayokaribia na nyeupe hadi nzito inayoelekea kwenye weusi.
Ukijipanga utagundua kuwa kijivu ni rangi yenye mvuto kwa kupendezesha nyumba yoyote ile. Kumbuka kuwa usizidishe na tumia pamoja na rangi nyingine pia.
Mawasiliano: Tembelea www.vivimachange.blogspot.com,0755 200023.