Taifa Stars isirudie makosa ya 2011 leo

28Mar 2016
Mhariri
Nipashe
Taifa Stars isirudie makosa ya 2011 leo

BAADA ya kutolewa kwa kipigo cha jumla ya mabao 9-2 dhidi ya Algeria katika mchakato wa kuwania kufuzu kushiriki michuano ijayo ya Kombe la Dunia, Taifa Stars ina nafasi nyingine ya kufuta makosa itakapowakabili wageni, timu ya taifa ya Chad leo.

Timu hizo zitachuana kwenye Uwanja wa Taifa leo jioni katika mechi ya marudiano ya Kundi G la kuwani kufuzu kushiriki fainali zijazo za Mataifa ya Afrika (Afcon).

Wakiwa mkiani mwa msimamo wa Kundi G, Chad (Les Sao), watakuwa na presha kubwa kusaka ushindi wakati watakapoikaribisha Stars katika mechi hiyo baada ya kufungwa bao 1-0 nyumbani wiki iliyopita.

Les Sao wanataka kutumia kila mbinu wawezayo ugenini kupata ushindi wa kwanza na kufufua matumaini ya kwenda Gabon mwakani baada ya kupoteza mechi zote tatu zilizopita dhidi ya Misri, Nigeria na wenyeji wao wa leo, Taifa Stars.

Walipoteza 5-1 dhidi ya vinara wa kundi, Misri na pia wakachapwa 2-0 nyumbani na Nigeria wanaoshika nafasi ya pili kabla ya kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Stars.

Mbali na matokeo hayo mabovu, Chad pia wamekosa nafasi ya kwenda Russia kushiriki fainali za Kombe la Dunia 2018 baada ya kuchapwa na Mafarao mabao 4-0 licha ya kushinda 1-0 nyumbani katika mechi ya kwanza.

Taifa Stars ambao wana pointi nne katika nafasi ya tatu ya Kundi G, nao wako kwenye presha kubwa kuhakikisha wanayaweka hai matumaini yao ya kwenda Gabon.

Wakiwa wameweka malengo ya kushinda mechi zote mbili dhidi ya Les Sao, Stars walio chini ya kocha mzawa Boniface Mkwasa, wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kufungwa bao 1-0 dhidi ya Chad katika mechi yao mwisho dhidi ya timu hiyo nchini.

Wakishinda mabao 2-1 ugenini Novemba 11, 2011, Taifa Stars walikubali kichapo cha bao 1-0 nyumbani dhidi ya Chad siku nne baadaye.

Kutokana na kumbukumbu hii mbaya, Nipashe tunatoa rai kwa nyota wa Taifa Stars na benchi lao la ufundi kuhakikisha hawarudii makosa yaliyoigharimu katika kipigo cha 2011.

Kama kweli Tanzania iliyopoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Misri kabla ya kutoka suluhu na Super Eagles kwenye Uwanja wa Taifa wamedhamiria kufuzu kwenda Gabon mwakani, tunaamini hawana budi kupata ushindi, tena mnono, dhidi ya Chad leo.

Tunaamini kikosi cha kocha Mahamat Omat Yaya, kimejipanga kulipa kisasi cha kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Stars na kujipoza baada ya kuwa na mwanzo mbaya katika michuano ya Afrika msimu huu.

Tanzania haijawahi kushiriki michuano mikubwa ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) tangu 1980 ilipofuzu kwa mara ya kwanza kushiriki michuano ya Mataifa Huru ya Afrika.

Tunaamini rekodi hii ni mbaya kwa soka la Tanzania na ushindi dhidi ya Chad leo huenda ukawa njia ya mafanikio na ufunguo wa maendeleo ya soka la Tanzania kwa kuwa Stars itakuwa na nafasi nzuri ya kuzipiku Misri na Nigeria katika mbio za kwenda Gabon.

Ni matumaini yetu kuwa Watanzania watakaoingia kwenye Uwanja wa Taifa leo, wataiunga mkono timu yao ya taifa kuhakikisha inaipiga Chad ‘nje-ndani’ kwa kuwa 'damu nzito kuliko maji'.
Kila la heri Taifa Stars!