Taarifa ya Ikulu haikueleza kwa undani yaliyomo katika ripoti hiyo, zaidi ya kusema kuwa Rais Magufuli alipokea taarifa hiyo yenye ripoti tano, ukiwa ni utaratibu wa kikatiba unaomtaka CAG kukabidhi kwa Rais taarifa ya ukaguzi kabla ya mwisho wa Machi.
Kwa mujibu wa taratibu, baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli ataikabidhi ripoti hiyo kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano katika siku saba za mwanzo za Mkutano wa Tatu wa Bunge hilo utakachofanyika mjini Dodoma.
Tunampongeza CAG Profesa Assad na timu yake kwa kuikamilisha kazi ya kuandaa taarifa hiyo na kuiwasilisha kwa Rais kwa ajili ya utekelezaji.
Tunachokisubiri sasa ni kwa Rais kulikabidhi Bunge taarifa hiyo ambayo tunaamini kuwa itajadiliwa kwa kina na Wabunge kisha kutoa mapendekezo huhusiana na hatua za kuchukua dhidi ya mambo yatakayobainika katika ripoti hiyo.
Katika miaka ya karibuni, taarifa ya CAG imekuwa ikifuatiliwa kwa hamu na kwa ukaribu na wananchi wengi, kutokana na kuibua madudu na uozo kuhusu wizi, ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha na mali za umma katika Serikali Kuu, mashirika ya umma, Halmashauri, idara na wakala za serikali.
Taarifa hiyo pia imekuwa ikiibua mianya ya ukwepaji kodi za serikali, misamaha ya kodi pamoja na, kutowajibika na matumizi ya madaraka miongoni mwa viongozi wa umma. Mwaka 2012 taarifa iliibu a mjadala mkali bungeni kuhusiana na kashfa mbalimbali na kuwahusisha mawaziri kadhaa na mwishowe mawaziri sita waliondolewa katika nafasi zao.
Mawaziri waliong’olewa ni Mustafa Mkulo (Fedha), William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk. Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Omar Nundu (Uchukuzi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Dk. Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii). Pia walikuwamo manaibu mawaziri ambao ni Dk. Lucy Nkya (Afya) na Dk. Athuman Mfutakamba (Uchukuzi).
Katika siku za karibuni, baadhi ya watendaji na viongozi wa umma wameonyesha dalili za kutotaka taarifa ya CAG kujadiliwa bungeni, pengine kwa kuogopa kuwajibishwa.
Hata hivyo, hatutarajii kama kuna mtu au kikundi cha watu ambao wanaweza kulinyang’anya Bunge mamlaka yake ya kupokea na kujadili taarifa ya CAG kila mwaka, kwa maslahi yao binafsi.
Ni matarajio yetu kwamba ofisi ya CAG itaaachwa iendelee kutekeleza majukumu yake kwa uhuru likiwamo la kuibua na kuweka hadharani vitendo vya wizi, ubadhirifu na matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Tunashauri kwamba baada ya Bunge kuipokea taarifa hiyo kutoka kwa Rais, litenge muda wa kutosha kwa ajili ya Wabunge kuijadili kwa kina kisha serikali itekeleze mapendekezo yao kwa lengo la kudhibiti vitendo vya ufisadi.
Rais Magufuli kwa miezi minne tangu aingie madarakani, ajijipambanua kwamba ajenda yake kubwa ni kupiga vita rushwa na ufisadi, hivyo ni imani yetu kwamba taarifa ya CAG atakuwa anaitumia kama silaha kwa kuwa ina ushahidi ambao hauna shaka na unakubalika kisheria.
Tunasubiri kuona serikali yake ikiitumia ripoti aliyokabidhiwa jana kutumbua majipu yote ambayo yamebainishwa ndani yake bila kupoteza muda wa kufanya uchunguzi wa vyombo vya dola.










