Mwita alishinda nafasi hiyo kwa kupata kura 84 dhidi ya mpinzani wake, Yusuph Yenga, wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyepata kura 67. Uchaguzi huo umefanyika kutokana na busara za Rais Dk. John Magufuli, baada ya kutoa maelekezo kwamba uchaguzi huo ufanyike bila kujali ni chama gani cha siasa kimeshinda na mshindi atangazwe.
Itakumbukwa kuwa uchaguzi huo uliahirishwa mara kadhaa kutokana na baadhi ya makada wa CCM kuweka pingamizi mahakamani, hali iliyozua mvutano mkali kati ya chama tawala na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Kufanyika kwa uchaguzi huo kumemaliza mvutano ambao haukuwa na tija yoyote, hivyo kuwafungulia milango Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam kuanza kuchapa kazi za kuwaletea maendeleo wananchi.
Tunampongeza Mwita kwa ushindi huo ambao tunaamini kuwa umetokana na imani waliyonayo kwake madiwani wenzake; kwamba anazo sifa za kuliongoza Jiji na kuwaletea maendeleo wakazi wake.
Hata hivyo, Jiji la Dar es Salaam lina changamoto nyingi ambazo zitampasa afanye kazi kwa bidii na kujituma kwa kushirikiana na madiwani wa vyama vyote bila kujali tofauti za kiitikadi.
Jiji hilo ndilo linaloongoza nchini kwa kuwa na idadi kubwa ya watu, hivyo kukabiliwa pia na changamoto hizo ikiwamo miundombinu ya barabara katika manispaa zake za Ilala, Temeke na Kinondoni. Manispaa hizo zina barabara ambazo hazijafanyiwa ukarabati kwa kipindi kirefu na kusababisha zipitike kwa taabu.
Uhaba wa maji pia ni tatizo sugu kwa wakazi wengi, hivyo, uongozi wa Jiji haunabudi kubuni miradi mingi ya maji na kuisimamia ili kupunguza kero hiyo. Zipo pia changamoto za elimu hususan elimu bure kwa shule za msingi na sekondari. Kinachotakiwa ni Jiji kwa kushirikiana na manispaa hizo kubuni mikakati ya kuhakikisha shule hizo zinapata madawati na vyumba vya madarasa kukidhi ongezeko la wanafunzi.
Manispaa za Jiji Dar es Salaam zinakabiliwa na tatizo sugu la migogoro ya viwanja. Viwanja vingi vya wazi vimeuzwa au pamoja na migogoro mingine inayowahusu watu binafsu na taasisi.
Jiji hilo lina vyanzo vingi vya mapato ikiwamo miradi kadhaa, lakini jambo la kushangaza ni kuwa fedha zinazopatikana ni kidogo kulingana na vyanzo hivyo, na mikataba ya miradi mingine inalinyonya Jiji kwa kulikosesha mapato.
Baadhi ya changamoto tulizozitaja na nyingine ndizo zinazotakiwa kushughulikiwa na Meya Mwita kwa kushirikiana na madiwani wa manispaa zote tatu zinazounda Jiji la Dar es Salaan.
Ni matarajio yetu kwamba madiwani wote wanaounda Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam watafanya kazi kwa uzalendo, uadilifu, bidii na kwa kushirikiana ili kubadili sura ya jiji hilo na kuwaletea wananchi maendeleo. Wanapaswa kukumbuka kuwa muda mwingi umepotea katika malumbano ya kumpata meya, hivyo waanze haraka kuchapa kazi kwa kasi.










