Yanga, Azam wanahitaji maandalizi ya kweli Afrika

23Mar 2016
Mhariri
Lete Raha
Yanga, Azam wanahitaji maandalizi ya kweli Afrika

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Afrika, Yanga na Azam, wote wamefanikiwa kuingia Raundi za Pili za michuano hiyo baada ya kuwatoa wapinzani wao mwishoni mwa wiki.

Yanga walianza kuwatoa APR ya Rwanda katika Ligi ya Mabingwa Afrika Jumamosi baada ya sare ya 1-1 wakitoka kushinda 2-1 ugenini mjini Kigali wiki iliyotangulia na Azam FC wakafuatia Jumapili kwa kuwatoa Bidvest Wits ya Afrika Kusini baada ya ushindi wa mabao 4-3 wakitoka kushinda 3-0 ugenini mjini Johannesburg.

Maana yake, Yanga imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-2 na sasa itamenyana na Al Ahly ya Misri mwezi ujao, wakati Azam FC imefuzu kwa ushindi wa jumla wa 7-3 na sasa itamenyana na Esperance ya Tunisia, pia mwezi ujao.

Mechi za kwanza zinatarajiwa kuchezwa kati ya Aprili 8 na 10, wakati marudiano yatakuwa kati ya Aprili 18 na 20 na timu zote za Tanzania zitaanzia nyumbani.

Al Ahly (National) na Esperance zote ni timu bora na miaka yote wamekuwa washindani wa mataji ya Afrika – hii inamaanisha timu zetu sasa zinaingia kwenye mtihani mgumu na zinahitaji maandalizi ya kina.

Tayari miongoni mwetu tumekwishahukumu kwamba mwisho wa safari za Yanga na Azam kwenye michuano ya Afrika umewadia, tu kwa sababu tunajua ubora na umakini wa hali ya juu wa Ahly na Esperance katika michuano hiyo.

Na hii pekee ni sababu tosha kwamba, Azam na Yanga zinahitaji maandalizi mazuri. Kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya timu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara juu ya kuahirishwa kwa mechi za Azam na Yanga kwa ajili ya mechi za Afrika, Simba SC wakiongoza kelele hizo.

Simba wanataka Azam na Yanga waendelee na ligi huku wakicheza michuano ya Afrika pia – si vibaya, lakini Lete Raha tunaona ipo haja ya kulitazama mara mbili suala hilo.

Mshambuliaji tegemeo la mabao wa Yanga, Amissi Tambwe, ameshindwa kucheza vizuri mechi zote dhidi ya APR kwa sababu aliumia katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya African Sports siku tatu kabla ya mchezo wa kwanza na APR mjini Kigali.

Ni kweli Yanga na Azam zote zimesajili zaidi ya wachezaji 25, lakini lazima tukubali kwamba kati ya hao kuna wachezaji muhimu, ndiyo maana hata Barcelona pamoja na kuwa na wigo mpana wa wachezaji kuanzia wa kikosi cha kwanza, akiba na hata katika akademi yake, lakini bado utaona kuanzia mashindano ya nyumbani hadi Ulaya wanacheza wale wale kina Lionel Messi, Neymar, Luis Suarez na wenzao.

Usipomuona mmoja kati ya wachezaji unaowajua wa kikosi cha kwanza cha Barca, basi jua atakuwa anaumwa au anatumikia adhabu. Huo ndiyo ukweli. Wakati Yanga na Azam wanatarajiwa kucheza na wapinzani wao wa Kaskazini mwa Afrika Aprili 9 na 10 Dar es Salaam, kabla ya hapo watakuwa na mechi mbili za mashindano ya nyumbani, Kombe la TFF na Ligi Kuu.

Lete Raha tunaona kabisa huku ni kuzitengenezea mazingira mabaya timu hizo kuelekea kwenye mechi hizo ngumu za michuano ya Afrika – na ndiyo maana leo tunawashauri Bodi ya Ligi na TFF watumie hekima wawezavyo ili kuziwezesha Azam na Yanga kupata fursa nzuri ya maandalizi kabla ya mechi zao na Ahly na Esperance.