Katika kudhihirisha kuwa agizo hilo limepata mwitikio chanya, Rais Dk. John Magufuli, juzi alihakiki silaha anazozimiliki Ikulu kwa maofisa wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam wakiongozwa na Kamanda wake, Kamishna Simon Sirro.
Makonda alitoa agizo hilo hivi karibuni baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo, ukiwa miongoni mwa mikakati yake ya kupambana na matukio ya ujambazi yaliyoshamiri katika jiji hilo.
Hatua ya Rais Magufuli ya kuhakiki silaha zake inamaanisha kwamba suala la kuhakiki silaha sasa sio la Mkoa wa Dar es Salaam pekee, bali ni la nchi nzima kwa sababu kuhakiki mkoa mmoja sio njia ya kudhibiti umiliki wa silaha haramu.
Matukio mengi ya uhalifu yanayofanyika nchini yamekuwa yakiwahusisha wahalifu kutoka maeneo mengine mbalimbali. Mathalani, matukio yanayofanyika Dar es Salaam, utakuta waliohusika wanatoka mikoa ya jirani kama Pwani.
Lingine ni kuwa silaha nyingi zinazotumika katika uhalifu ni zile ambazo hazijasajiliwa na Jeshi la Polisi na zimekuwapo taarifa kuwa silaha nyingi haramu zilizoko nchini zimeingizwa kimyemela kutoka nchi jirani.
Sababu kubwa inayochangia ni kuingia nchini kwa baadhi ya wageni wanaokimbia machafuko ya kisiasa hususan kutoka nchi za Maziwa Mkuu ambazo hazina amani na utulivu. Mikoa ambayo kwa kiwango kikubwa imekuwa ikiathiriwa na ujio wa wageni hao ni Kagera, Kigoma, Geita, Tabora, Rukwa na Katavi.
Kutapakaa kwa silaha haramu katika mikoa hiyo, kulisababisha majambazi kuzitumia kuteka magari na kuwapora abiria na wakati mwingine kuwaua au kuwajeruhi, hali iliyosababisha Jeshi la Polisi kuwapa askari wake jukumu la kusindikiza magari.
Inawezekana kwamba silaha hizo pia ndizo zinazotumiwa na wahalifu kufanya vitendo vya uhalifu katika maeneo mengine ya nchi. Kutokana na hali hiyo ndiyo maana tunashauri agizo la uhakiki wa silaha liwe la nchi nzima.
Ni wajibu sasa wa kamati za ulinzi na usalama za mikoa kuagiza wamiliki wote wa silaha kuzihakiki pamoja na kuhakikisha kwamba inasimamia kikamilifu.
Tunategemea kwamba kama uhakiki wa silaha unafanyika kwa umakini na unakuwa endelevu, matukio ya ujambazi yaliyoshamiri yatapungua kama siyo kumalizwa kabisa.
Tunapaswa kukubali kuwa kuna tatizo kubwa kutokana na wahalifu kufikia hatua ya kuvamia vituo vya polisi wakiwa na silaha na hata kuwapora silala polisi na kuwaua. Inapofikia hatua askari polisi akauawa na kuporwa silaha lazima tujiulize hiyo silaha imepelekwa wapi na kwa malengo yapi?
Pamoja na uhakiki wa silaha, tunashauri kwamba ipo haja kwa vyombo vya ulinzi na usalama kufanya oparesheni ya pamoja ya kusaka silaha zote haramu nchi nzima, ambayo itasaidia kuzipata hata silaha ambazo wameporwa askari katika baadhi ya matukio.
Tunasisitiza kwamba uhakiki wa silaha ni jambo muhimu sana na tunawahimiza wamiliki wote kuhakikisha wanakwenda kuzihakiki kwa kufuata utaratibu utakaopangwa.
Kama mkuu wa nchi amehakiki silaha zake kwa hiyari yake, hatutarajii kama atakuwapo mmiliki atakayekaidi. Vinginevyo, tunasisitiza kwamba uhakiki wa silaha ufanyike nchi nzima bila mzaha.










