Azam ambao wamepoteza mechi moja tu katika mashindano yote ya kimataifa waliyoshiriki msimu huu, wanapewa nafasi kubwa ya kutinga raundi ya pili ya michuano hiyo baada ya kushinda 3-0 katika mechi ya kwanza jijini Johannesburg, Afrika Kusini wiki iliyopita.
Wanalambalamba waliuanza msimu wa 2015/16 kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame bila kupoteza hata mechi moja, lakini wakatokewa mapema Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar kabla ya kutwaa ubingwa mashindano maalum ya timu nne nchini Zambia.
Kurejea kikosini mwa beki kisiki, Aggrey Morris aliyepona majeraha ya goti, kumekiimarisha zaidi kikosi cha Mwingereza Stewart Hall ambacho kinaendelea kutesa na washambuliaji Kipre Tchetche na John Bocco.
Beki wa pembeni Shomari Kapombe ambaye alikuwa mmoja wa wafungaji katika mechi ya kwanza jijini Johannesburg, anazidi kung'ra kwa kutupia magoli muhimu msimu huu. Mchezaji huyo wa zamani wa Simba na AS Cannes ya Ufaransa ametupia mara nane katika mechi 21 zilizopita za Ligi Kuu.
Azam FC pia wanapewa nafasi kubwa ya kuwatungua tena Bidvest kutokana na mechi hiyo kuchezwa mchana jua kali (kuanzia saa 9:15 alasiri), muda ambao si rafiki kwa timu hiyo ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) ambayo nyota wake wamezoea baridi la 'Sauzi'.
Mechi hiyo itachezeshwa na Gait Oting akisaidiwa na Abdallah Gassim na Casim Dehiya, huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Ariel James, wote kutoka Sudan Kusini










