Mechi kati ya Chad na Taifa Stars itafanyika Jumatano Machi 23 na marudiano Machi 28 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili jana, kocha mkuu wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa alisema kuwa uamuzi wa kuondoka kwa 'mafungu' umetokana na baadhi ya wachezaji walioitwa kwenye timu hiyo kuwa na majukumu ya klabu nje ya Dar es Salaam.
Mkwasa alisema kuwa wachezaji wanaocheza nje ya nchi nahodha Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wataungana na timu hiyo huko huko N'Djamena.
"Tumefanya hivi ili kupata nafasi angalau ya kufanya mazoezi kwa siku tatu tukiwa hukohuko," alisema Mkwasa.
Wakati huohuo, Twiga Stars (timu ya soka ya Taifa ya Wanawake) inatarajia kuwakabili wenyeji wao Zimbabwe (Mighty Warriors) katika mchezo wa marudiano wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AWC) utakaofanyika leo kwenye Uwanja wa Rufalo jijini Harare.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Machi 4 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam, Twiga Stars ililala mabao 2-1 dhidi ya wapinzani wao hao na leo inahitaji ushindi wa kuanzia 2-0 ili iweze kusonga mbele.
Kocha mkuu wa Twiga Stars, Nasra Juma, alisema kwamba kikosi chake kiko tayari kwa mapambano na wanataka kurudia mafanikio waliyopata 2010 kwa kushiriki fainali hizo zilizofanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini.










