Katika hali isiyokuwa ya kawaida, tangu kumalizika kwa uchaguzi Lowassa amejitokeza mara chache kuzungumza na wanahabari. Ukimya huu ambao haukutarajiwa umetafsiriwa na baadhi ya wadau kwamba ni ishara ya kukosa uhuru katika kambi ya upinzani.
Ukweli juu ya ukimya wake haujathibitishwa na yeye mwenyewe wala chama chake. Hata hivyo watu wanaweza kuhisi kuwa ukimya huo unaashiria kukosa raha ndani ya upinzani kutokana na ukweli kwamba marafiki zake wengi wako CCM.
Siyo dhambi Lowassa akirudi CCM kwani ndiko alikopikwa na alikojipatia umaarufu wa kisiasa. Kubadilisha chama cha siasa ni hiari ya mtu, hakuna sheria inayomfunga ‘mwanampotevu’ asirudi kundini kwani anakumbatiwa na kusamehewa (Siasa siyo uadui).
Nimemtaja Lowassa kwa makusudi kwa sababu imeelezwa alichokuwa anakipigania kipindi cha kampeni katika kambi ya upinzani sasa kipo ndani ya CCM yaani kuleta mabadiliko ya kiuchumi. Na kwamba wawili hawa Rais John Magufuli na Lowassa walikuwa na mtizamo pacha hasa wa sera ya kuchukia umaskini.
Mfano, katika kipindi cha kampeni wagombea wote wawili walipata umaarufu kwa sababu ya kauli mbiu zilizokuwa zikifanana za kuleta mabadiliko.
Rais Magufuli alikuwa akisistiza “hapa kazi tu” kwa upande wake Lowassa alikuwa akisisitiza “mchaka mchaka” hivyo baada ya uchaguzi kumalizika na Rais Magufuli kuanza kazi, Lowassa ameridhishwa na utendaji wake hususani katika sera ya mabadiliko kivitendo.
Ipo desturi ndani ya CCM ya kuachiana uenyekiti wa chama tangu enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Hivyo upo uwezekano wa Rais Magufuli naye akaachiwa nafasi hiyo Juni mwaka huu na kutamfanya avae kofia mbili ya uenyekiti wa chama na Rais wa Tanzania.
Napenda kuweka wazi kuwa sina pingamizi lolote kwa Rais Magufuli kukabidhiwa uenyekiti wa chama. Isipokuwa, wasiwasi wangu ni kwamba kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja kutaathiri kasi yake ya kutumbua majipu. Wahafidhina wenye mizizi ndani ya chama watamfunga kidhibiti kasi au “spidi gavana”
Kwa mazingira hayo ya kuvaa kofia mbili, kutamlazimisha kusalimu amri yaani akubali kupunguza kasi ya kutumbua majipu kwasababu kwa vyovyote vile ataingiliwa kiutendaji na vikao vya chama. Rais Magufuli ni mtendaji na siyo mwanasiasa, hivyo anamhitaji Mwenyekiti wa CCM atakakwenda na kasi aliyoianzisha.
Nathubutu kusema kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu, kama anavyopenda kujipambanua yeye Rais Magufuli kwamba “Msema kweli ni mpenzi wa Mungu” nami niseme, nafasi ya uenyekiti wa CCM ingefaa apewe Lowassa ili amsaidie Rais katika upande wa chama.
Rais Magufuli abakie serikalini kutumbua majipu akisaidiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan. Kikosi kazi hiki kitaleta mabadiliko ya uchumi na kwa kasi pia.
Natamani kuwaona viongozi wane hawa wakipanda gari moja. Hakika hakuna ubishi nchi hii itapiga hatua kubwa kiuchumi.Rais Magufuli tayari ameonyesha dira ya serikali yake. Anatakiwa apate mtu wa aina yake atakayemsaidia kwenye chama ambaye ataendana na kasi yake. Watanzania wanachokisuburi ni kuona mabadiliko yaliyoanza kushika kasi yakiendelea bila kuingiliwa kisiasa.
Natambua kwamba hii ni zamu ya Rais Magufuli kuachiwa kiti hicho, kadhalika natambua utendaji wake tangua ashike urais. Sina shaka nafasi hiyo ataimudu, hata kuliko watangulizi wake.
Hata hivyo, wasiwasi wangu ni kwamba, atapata changamoto ambazo zitatokana na kuheshimu vikao vya chama atakapokalia kiti hicho. Kwani nijuavyo kwenye chama kuna msemo kuwa “chama kwanza mtu baadaye”
Kwa ushauri wangu ningependa Rais Magufuli abaki na nafasi ya urais huku nafasi ya unyekiti wa chama ukiongozwa na mtu mwingine. Kwa muktadha huo dhana ya mwingiliano wa vikao vya chama vitapungua na atapata muda mzuri wa kutumikia jamii.
Kama hayo hayatoshi, maagizo yake kiserikali yataheshimiwa tofauti na sasa ambapo baadhi ya viongozi wa upinzani wamekuwa wakitafsiri tamko la Rais kwa mtizamo wa kiitikadi.
Haya ni maoni binafsi yasiyofungamana na upande wowote, Watanzania wanaopenda nchi hii, watakubaliana nami kwamba kuvaa kofia mbili kutampunguzia Rais Magufuli kasi kwani itamlazimu afuate mamuzi ya vikao.
Mawasiliano: 0713 399 004/0767 399 004, jmkibasso@gmail.com










