Kesi za mimba utotoni hazina mwenyewe?

19Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Kesi za mimba utotoni hazina mwenyewe?

“MABINTI shuleni na ndani ya jamii tunapewa mimba au kuolewa utotoni, hakuna ufumbuzi kwa vile hayupo mwenye jukumu la kusimamia kesi hizi zinapotokea.”

Agness Joseph.

Ni maneno ya muathirika Agness Joseph (16) aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha pili wa Sekondari ya Ilolangulu wilayani Uyui, ambaye ni mjamzito wa miezi mitano.

“Nimetimuliwa shuleni baada ya kupewa ujauzito na mwanaume aliyekuwa akinisaidia mambo mengi. Hata hivyo, baada ya mimba kugundulika mtuhumiwa ametoroka na sasa sina msaada licha ya kesi kufikishwa polisi hakuna wa kufuatilia.”Analalamika.

“Naona kesi hizo hazina wa kuzishughulikia ndiyo maana wakati mwingine tunaishia kuhangaika na wahusika hawabanwi wala kufikishwa mahakamani.”

Akiwa na uchungu anashauri kuwa iwapo mwanaume anayempa binti mimba atakimbia, wazazi wasakwe washitakiwe ili wamtafuta kijana wao.

Anataka manispaa au halmashauri kuandaa sheria ndogo za kuwabana wazazi na walezi ili wawajibike kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wanaowapa mimba wanafunzi.

“Kweli kesi hizi huishia ngazi za chini kwa vile hazina mwenye jukumu la ufuatiliaji,” Agness, analalamika.
Anasema hakuna wa kuwatafuta watuhumiwa na ushahidi, kuufikisha polisi wala wa kufuatilia mwenendo wa kesi mahakamani.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilolangulu Kusini, wilayani Uyui, Abdallah Willa, anakiri kuwapo upungufu, hakuna mamlaka inayohusika moja kwa moja na kesi hizo ndiyo maana mara nyingi utasikia mtuhumiwa hafahamiki au katoweka.

Wanatoa maoni hayo kwenye utafiti unaolenga kuibua vitendo vya unyanyasaji wanawake na watoto, uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) na Shirika Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), mkoani Tabora.

Japo hakuwa na takwimu kuthibitisha maelezo yake, Willa anasema, ujauzito utotoni ni changamoto, lakini hakuna mamlaka mahsusi kama viongozi wa kijiji waliopewa jukumu la kuzifuatilia na kuwezeshwa kuzishughulikia.
Anaeleza kuwa binti wa shule ya msingi akipata ujauzito kamati ya shule ikishajiridhisha inamfukuza shule na kumkabidhi kwa wazazi au mlezi.

“Kwa sekondari Bodi ya Shule inamfukuza na kumkabidhi kwa wazazi au walezi, lakini haishughuliki na kesi wala haifuatilii zaidi,” anaonya.

Anataka watendaji wa vijiji wapewe jukumu la ufuatiliaji na kuwezeshwa ili wafuatilie kesi hizo.

Willa anasema mimba ni nyingi kijijini hapo, lakini anapewa taarifa za ujauzito baada ya watoto kutimuliwa shuleni.
Faustine Bamboriki, Ofisa wa Maendeleo ya Jamii wilayani Urambo, anasema kuna upungufu.

“Awali nilikuwa mwalimu na mjumbe wa bodi ya shule kabla ya kuingia kwenye maendeleo ya jamii, nimeona mwanafunzi mjamzito anafukuzwa na kamati ya shule au bodi kwa shule za sekondari. Vyombo hivi huidhinisha kufukuzwa na kuwakabidhi kwa wazazi au walezi wanafunzi wajawazito.”

Bamboriki anasema huenda taratibu haziwaelekezi kufuatilia na kushughulikia kesi hizo mahakamani.
Ofisa Ofisa Elimu Taaluma wa Wilaya ya Urambo, akizungumzia madai kuwa kesi hizo hazina ‘mwenyewe’ anasema kuna upungufu.

Filipo Barugahale, anasema ni kweli kuna tatizo kwani haijulikani ni nani anayeshughulikia kesi hizo.

“Kwa sasa yapo maelekezo kuwa kesi hizo zifikishwe kwa Mkuu wa Wilaya. Lakini kisheria si bodi wala kamati inayomshitaki mbakaji.”

Anaeleza kuwa hata inapotokea jitihada zimefanywa kumkamata na kumfikisha polisi na baadaye mahakamani, suala la nani mwenye jukumu la kumshitaki mtuhumiwa halijawekwa wazi.

Anakiri kuwa kukosekana anayewajibika moja kwa moja na kesi hizo imekuwa vigumu kufuatilia kikamilifu kesi hizo na kwamba athari mojawapo ni kesi nyingi kutoripotiwa ama wazazi wanamalizana nje ya mahakama.

POLISI
Suala kwamba kesi hizi hazina mwenyewe, linajadiliwa na Kamanda Sarah Nyoni, Mkuu wa Dawati la Polisi la Kuzuia Ukatili wa Kijinsia dhidi ya watoto na wanawake, mkoani Tabora.

Anasema kesi hizo zinafahamika na kushughulikiwa, lakini zinakwama kwa kukosa ushirikiano baina ya polisi, wazazi na wananchi.

Sarah anasema wahusika wanafikishwa mahakamani, lakini baada ya kupewa dhamana hutokomea. Kwa vile si wazazi, kamati ya wananchi wanaojihusisha nazo, wakati mwingine hata nyaraka mfano barua za utambulisho wa serikali za mitaa zinazofikishwa mahakamani ili kutoa dhamana ni feki.

“ Yote haya huwanufaisha washtakiwa ambao huruka dhamana na kutoroka.”

MATOKEO HASI
Kesi hizi zinapokosa mwenyewe wazazi na walezi hushirikiana na watuhumiwa kumaliza kesi hizo kabla ya kufikishwa mahakamani.

Hali hii inasababisha wazazi kupokea rushwa ya ng’ombe au fedha kuwalinda watuhumiwa na wakati mwingine polisi na hata walimu hudaiwa kuhusika pia.

Utafiti umegundua kuwa wazazi hupewa ng’ombe wengi na fedha ili kupoteza ushahidi na hili limedhihirika mara nyingi kwani mabinti wanapopelekwa mahakamani huwakana wanaume waliodaiwa kuwapa ujauzito.

Wanadai hawawafahamu waliowapa ujauzito wakidai walikutana nao minadani, hivyo mtuhumiwa huachiwa huru baada ya binti kumkana.

Mathalani Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Urambo, wilayani humo Nassoro Ndege, akizungumzia suala hilo, anasema baadhi ya wazazi wamekuwa mstari wa mbele kuficha ushahidi.

Anasema wakibaini kuwa watoto wana ujauzito wanawaombea mabinti uhamisho kumbe wanaficha mimba.

“Anapopewa uhamisho huondoka bila taarifa za mimba kufahamika, baadaye binti anaonekana ana mtoto mchanga ama ameolewa eneo jirani,” anafafanua Mwalimu Ndege.

Anasema wazazi wengine wakipanga mpango wa kuwaoza mapema au wakijua watoto wao wana mimba, huwaondoa shuleni wakipelekwa maeneo mengine ili wafukuzwe shule kwa utoro sugu, lakini kilichofanyika ni kuwaoza au kuficha mimba.

CHANZO CHA MIMBA
Makabila ya wafugaji hasa wakulima wanaamini kuwa binti anaolewa akiwa mdogo chini ya miaka 13 na iwapo ataachwa kuwa mkubwa mwenye miaka 18 huonekana mzee asiyeoleka.

Mfumo dume huu unaoendelea miongoni mwa Wasukuma unamchukulia msichana kama chombo cha kumstarehesha mwanaume hivyo kuwekwa tayari kuolewa muda wote.

“Wapo baadhi wanalipiwa mahari wakiwa na miaka sita hivyo anapofikia miaka 12, anaweza kuozeshwa bila kujali kuwa anaachishwa masomo, ” anasema Ofisa Maendeleo ya Jamii wilayani Urambo, Paul Kahumbi.

Kwa upande wa wavulana nao huozeshwa katika umri mdogo ili kuwazuia wasihame nyumbani wabaki kuchunga mifugo.
Wanafunzi wa kiume wa Shule za Azimio na Urambo, wanasema mfumo dume unawashinikiza vijana kuoa mapema ili kupata heshima na kupewa nafasi ya kuchangamana na jamaa wengine kwenye jamii.

Wanasema wavulana wenye umri chini ya miaka 18 ambao hawana wanawake, hulala mazizini, lakini wanapoona wanawake huishi kwenye boma na kuheshimika hivyo kuoa utotoni ni njia ya kuwajengea heshima kwenye familia zao na kuwadhibiti wasihamie mijini.

UDHIBITI
Baadhi ya shule wilayani Uyui zina kamati za nidhamu zinazoundwa na wazazi wenye watoto wanaosoma sekondari, walimu na wadau kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbola wilayani humo Aloyce Shija, anasema.
Shija aliyewahi kuwa mjumbe wa kamati hiyo, anasema licha ya kamati hizo kuwapo hazina fedha za kufanyiakazi badala yake wanajitolea.

Anaeleza kuwa pamoja na nia njema ya kufuatilia wakati mwingine watuhumiwa wana fedha kiasi cha kutishia maisha ya wanakamati.

ATHARI
Kalekwa Shabani, kutoka wilaya ya Uyui, aliyepata mimba akiwa na miaka 15 wakati huo akiwa mwanafunzi wa darasa la sita akizungumzia athari alizopata anasema ni pamoja na kujifungua akiwa na umri mdogo na kuumia kisaikolojia na kimwili.
Pia ni amejisikia kujuta na kuhuzunika hasa kwa vile hakukuwa na huduma muhimu kwa ajili yake na mwanae. Anasema wapo baadhi wanapata fistula na ulemavu.

Anasema athari nyingine zinazowapata mabinti wanapozaa utotoni watoto wao kuhangaika ikiwa ni pamoja na kushindwa kusoma.

Kalekwa anasema, watoto hulazimika kuingizwa kwenye biashara ndogo ndogo za kuuza karanga na matunda ya misimu mitaani, na wakati mwingine wanakuwa waathirika wa unyanyasaji watoto.

“Wakati mwingine watoto wanaingia kwenye uhalifu mapema wanapelekwa mahabusu au jela hutokea wengine wakauawa kwa udokozi,” anasema.

Anasema kutokana na mabinti wengi kutokusoma, hata idadi ya watumishi wa umma na wa asasi za kiraia wanaofanya kazi mkoani humo wanatoka nje ya Tabora, hivyo kuwanyima wazawa mapato na kuongeza umaskini miongoni mwa jamii zao.

UFUMBUZI
Kamati nyingi za shule na bodi hazina fedha, wananchi wanataka ziwezeshwe kwa kutumia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ili zihamasishe na kupunguza mimba shuleni.

Mfuko huo matumizi yake yashirikishe wadau wengi zaidi ili kupunguza ndoa mashuleni.

Kamati hiyo ina wajumbe wachache ambao ni Mkurugenzi wa Maendeleo wa Halmashauri, Mbunge (Mwenyekiti), wajumbe wengine ni maofisa mipango. Wananchi hao wanataka kuwe na wadau kutoka asasi za kirai, wawakilishi wa elimu na makundi ya wanyonge kama wenye VVU, walemavu na wajane.

Kadhalika mahakama zisikilize kwa kasi kesi za udhalilishaji watoto na kupunguza milolongo inayowakatisha tamaa walalamikaji kwa vile hukaa muda mrefu kabla ya hukumu, lakini pia ikitumia gharama nyingi.

Wazazi, shule na walimu waanzishe kamati na klabu za kuwalinda mabinti ikiwa ni pamoja na kuzungumza nao kuhusu watu wanaowahadaa kimapenzi.

Klabu hizo ikiwezekana zifuatilie mabinti wanaohamishwa na ikibidi kushinikiza kuwapima mimba kwanza ili kujua chanzo cha uhamisho shuleni.