Utulivu utawale Z’bar kuelekea uchaguzi wa marudio Jumapili

16Mar 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Utulivu utawale Z’bar kuelekea uchaguzi wa marudio Jumapili

UCHAGUZI wa marudio Zanzibar wa rais, wawakilishi na madiwani, unatarajiwa kufanyika Jumapili ijayo.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, kufuta uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, kwa madai kuwa kulikuwapo na dosari kadhaa.

Hata hivyo, uchaguzi huo utakihusisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vidogo kadhaa kutokana na Chama cha wananchi (CUF) na vyama vingine kususia uchaguzi huo kwa hoja kuwa hapakuwapo na haja ya kuitisha uchaguzi wa maruduo kwani wa mwaka jana ulikuwa huru na haki, badala yake kinachotakiwa ni kutangazwa kwa washindi na kuwaapisha.

Pamoja na Zec kuendelea na maandalizi ya uchaguzi wa marudio, kuna taarifa mbalimbali za kuwapo kwa amtukio yanayotishia usalama wa raia na mali zao katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Kuna malalamiko Unguja kwamba kuna makundi ya wahuni ambao wanawavamia watu, kuwapina na hata kuharibu au kupora mali zao na kwamba matukio hayo yamekuwapo tangu Jecha alipofuta matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana.

Inadaiwa kwamba vitendo hivyo vinafanywa na makundi hayo yaliwalenga watu wenye itikadi tofauti na ya kwao.

Kwa upande mwingine, CUF kimedai kwamba baadhi ya wanachama wake kisiwani Pemba wameanza kukimbilia msituni na wengine kutaka kukimbilia Kenya kwa ajili ya kuomba hifadhi. Chama hicho kimedai kuwa wananchi hao wanakimbia operesheni za kamatakamata zinazoendelea kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio.

Chama hicho kimelalamika kuwa tangu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, kumekuwapo na uingizwaji wa askari, vifaa na zana nzito za kivita katika visiwa vya Unguja na Pemba sambamba na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanaoranda randa mitaani wakiwa na silaha za kivita.

Mmoja wa viongozi wa kitaifa wa chama hicho, amedai kuwa kinachoonekana hivi sasa kitarejesha historia ya mwaka 2001. Mwaka huo mamia ya wafuasi wa chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania Visiwani walikimbia Pemba na kuomba hifadhi ya ukimbizi nchini Kenya, baada ya kutokea machafuko kutokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.

Hatukusudii kutuhumu wala kutetea chama au kundi lolote, isipokuwa kutahadharisha kwamba wakati huu wa kuelekea siku ya uchaguzi Jumapili ijayo, Zanzibar inahitaji amani na utulivu.

Vitendo vinavyolalamikiwa ni kichocheo kikuu cha kuharibu amani na utulivu wa visiwa hivyo. Jambo la msingi ni kwa vyombo nyenye dhamana ya ulinzi na usalama vikawajibika bila kugemea upande wowote wa itikadi na vikayachukulia hatua makundi yanayojihusisha na vitendo hivyo.

Historia inaonyesha kuwa uchaguzi umekuwa kichocheo kikuu cha vurugu Zanzibar, lakini suala hilo linaweza kumalizwa ikiwa kila Mzanzibari kwa nafasi yake atatanguliza maslahi ya taifa; kwamba Zanzibar kwanza chama chake cha siasa baadaye.

Itakuwa aibu kwa Tanzania kama kutakuwapo vurugu na matumizi makubwa ya vyombo vya dola kwa kuzingatia kwamba nchi yetu kwa miaka mingi na hadi sasa ni msuluhishi wa migogoro mingi katika nchi zingine.

Tunawashauri Wazanzibari kutambua kwamba uchaguzi ni kitu cha kupita, lakini Zanzibar itaendelea kuwapo.

Tunasisitiza kwamba amani na utulivu vitawale Zanzibar kuelekea uchaguzi wa marudio wa Jumapili.