Mfano wa matukio kama hayo, hujitokeza maeneo yenye mikusanyiko ya watu, kama sokoni, vituo vya mabasi na mengine kunakofanyika shughuli za kijamii.
Katika tukio ambalo nimewahi kulishuhudia ni la mama mmoja ambaye alidaiwa kuiba nguo katika duka moja eneo la Kariakoo. Mama huyo alikuwa amevuliwa nguo zake zote na kuachwa na nguo ya ndani pekee.
Mama huyo aliyekuwa na umri wa kati ya miaka 40 – 50, alikuwa amezongwa na kundi la wanaume, vijana kwa wazee, akizomewa na kudhalilishwa kwa kushikwa shikwa maungo yake.
Kabla ya kufahamu kilichokuwa kikiendelea, kulikuwa na kelele zilizotawala eneo zima la soko la Kariakoo, hali iliyofanya wateja waliokuwa wamekwenda kupata mahitaji katika soko hilo, kuingiwa na hofu.
Baadhi ya watu walidhani huenda majambazi wamevamia eneo hilo na wengine kudiriki kugeuza magari yao na kurudi walikotoka.
Hata hivyo, baada ya muda mchache, ndipo kundi hilo lililopoibuka huku likiwa limemuweka mwanamke huyo katikati na kumfanyia udhalilishaji wa kila aina.
Nilipojaribu kudadisi baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa pembeni ya tukio hilo, walisema kuwa ni tabia ya wafanyabiashara ndogo ndogo eneo hilo, wanaposikia mwanamke katuhumiwa kufanya wizi, kumvamia, na kumdhalilisha kwa kumvua nguo.
Nilipowauliza, wanampeleka wapi mama huyo ambaye alikuwa akipata hukumu hiyo bila kufikishwa mahakamani, walisema walikuwa wakimpeleka Kituo cha Polisi cha Msimbazi.
Binafsi kitendo kile hakikunifurahisha, kwa sababu aliyekuwa akidhalilishwa ni mwanamke mwenzangu, hata kama alikuwa amefanya kosa la wizi, hakustahili kupata adhabu hiyo ya kuvuliwa nguo hadharani na kufanyiwa udhalilishaji wa kushikwa maumbile yake na watu walistahili kumuita mama, dada au bibi.
Watu hao pia hudhalilisha wasichana wanaovaa nguo fupi kwa kuwachania na kuwaacha wakitembea utupu.
Sijawahi kuona mwanaume anayetuhumiwa wizi, au kuvaa nguo zinazoonyesha nguo zake za ndani, kufanyiwa udhalilishaji kama wanaofanyiwa wanawake.Kwa mujibu wa sheria, mahali pekee panapostahili kutoa hukumu ni mahakamani, si vinginevyo.
Tukio lingine lililoripotiwa kutokea wiki hii, maeneo ya kituo cha Mbuyuni, Barabara ya Bagamoyo, msichana mmoja alichaniwa nguo zake mpaka ya ndani na madereva wa bodoboda kwa madai kuwa alikuwa amevaa nguo fupi.
Imedaiwa kuwa msichana huyo licha ya kuvuliwa nguo, alifanyiwa kitendo cha kinyama cha kuingiliwa kimwili.
Mtu aliyemuingilia kimwili dada huyo haijulikani kama ni mzima kiafaya, au alikuwa na lengo la kusambaza ugonjwa wake. Hata kama si mgonjwa, hakufikiria hali ya mwanamke aliyemuingilia?
Madai ya waliofanya vitendo hivyo ni kuwa, eti wanatoa funzo kwa wasichana wengine wenye tabia ya kuvaa nguo fupi, wasipite eneo hilo.
Vitendo hivi vya unyanyasaji na ukatili wa wanaweke, ulisasababisha wanaharakati wa masuala ya wanawake na watoto, kushinikiza kuwapo na sheria zinazopiga vita vitendo hivyo.
Mwaka 1998, serikali kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilipitisha Sheria ya Makosa ya Kujamiiana, ili kuweka ulinzi kwa mwanamke na mtoto. Sheria hii ilirekebisha baadhi ya makosa kwa kuyafafanua zaidi katika Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya Juzuu iliyofanyiwa marekebisho 2002 na kuongeza mengine.
Katika Sheria hiyo imefafanua makosa ya kujamiiana na adhabu zake. Kwa mfano kosa la ubakaji; Mwanaume atakuwa ametenda kosa la kubaka kama atafanya tendo la ndoa bila ridhaa ya mwanamke.
Katika Sheria hiyo, adhabu anayostahili kupata mtu huyo ni kifungo cha maisha, au kifungo cha miaka isiyopungua 30 pamoja na viboko au pasipo viboko na faini.Mkosaji atatakiwa kulipa fidia kwa muathirika wa kosa au mlalamikaji.
Sheria hiyo pia imezungumzia ukatili wa kijinsia, ambapo kosa hili hufanyika na mwanaume kwa kitendo au vitendo au kwa maneno ya unyanyasaji anayotolewa mwanamke au msichana. (kwa mfano kumshika maziwa, makalio, kumbusu kwa lazima au matusi ya nguoni kwa mwanamke au sichana).
Mtu atakayepatikana na hatia ya kufanya kosa hilo, adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka mitano au faini isiyozidi Sh. 200,000 au vyote kwa pamoja. Mkosaji pia anaweza kuamriwa kutoa fidia kwa muathirika wa kosa.
Wanawake au wasichana wanaofanyiwa vitendo hivyo , ni lazima waelewe kuwa sheria inayowalinda ipo, hivyo wana wajibu wa kwenda kuripoti kwenye vyombo husika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Mtindo huo wa kudhalilisha wanawake, umekuwa ukifanywa zaidi na kundi la wahuni wanaojifanya kurekebisha tabia za wanawake.
Wanawake msikubali kudhalilishwa, chukueni hatua ili vitendo hivi vikomeshwe. Sidhani kama wahuni hao wanaweza kuwafanyia vitendo hivyo ndugu zao wa karibu.
bbandawe@hotmail.com: Simu 0774 466 571



.jpg?itok=nfwjwDzv)








