Ijue nguvu iliyo ndani ya mwanamke!

13Mar 2016
Flora Wingia
Nipashe Jumapili
Maisha Ndivyo Yalivyo
Ijue nguvu iliyo ndani ya mwanamke!

MPENZI msomaji, leo hebu tujuzane kwa mhutasari kuhusu baadhi ya nguvu waliyo nayo wanawake, kwamba tusiitizame tu katika duru la siasa, bali hata katika maandiko ya Mungu aliyeumba mbingu, nchi na vyote vijazavyo.

Wakati tukiwa bado katika vuguvugu la kuadhimisha Siku ya Mwanamke Duniani ambayo hufanyika Machi 8, kila mwaka, ni muhimu tukatafakari kwa makini nguvu iliyo ndani ya mwanamke kama ambavyo pia maandiko ya Mungu yanabainisha.

Nguvu iliyo ndani ya mwanamke ikitumika vizuri huleta faida au hasara kibiblia. Leo tuone faida chache. Nguvu ili ilete matokeo, lazima aliye nayo aijue, aitambue…..Ndani ya mwanamke iko nguvu kubwa sana. Na Mungu aliidhihirisha nguvu hiyo tokea mwanzo.

Lakini pia, ni ukweli usiopingika kuwa shetani naye anajua kuwa kama akifanikiwa kuteka jamii ya wanawake, basi ataitawala dunia. Ingawa wanawake wanachukuliwa kama viumbe dhaifu, lakini majukumu waliyopewa hayawezi kufananishwa na msingi wa neno hili.

Hata kama mwanaume akiwa mtu mkuu sana katika maisha yake, lazima ajue kuwa kuna wakati alikuwa kichanga katika tumbo la mwanamke. Shetani anajua kuwa mwanamke anatawala/anamiliki uzao(tumbo la uzazi), chimbuko(chanzo, asili) na pia anatawala jiko.

Ukitafakari maeneo hayo matatu, utagundua kuwa mwanamke anatawala ulimwengu. Dunia inatawaliwa na uzao(tumbo la uzazi), chimbuko(asili) na jiko.

Shetani pia anaufahamu ukweli kuwa akiwaachia wanawake wawe na bidii ya kumtafuta Mungu na wamiliki maeneo muhimu katika historia ya dunia, wanaweza kutikisa ufalme wake. Hivyo, wanawake wana vita kali ya kupigana na shetani; Naye huwa hawahurumii, huwapiga vibaya sana.

Tukiangalia katika mpango wa wokovu, kama ilivyofunuliwa katika sura ya tatu ya kitabu cha Mwanzo katika Biblia Takatifu, utagundua kuwa UADUI kati ya mwanamke na shetani una mizizi mirefu.

Mwanzo 3:15 imeandikwa; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino. Katika mpango wa Mungu kutukomboa, mbegu ya mwanamke ilitakiwa kumkanyanga shetani kichwani.

Hii haikumaanisha mbegu ya mwanaume, bali ya mwanamke. Hivyo ni dhahiri kabisa kuwa toka mwanzo wa dunia, wanawake wamekuwa wakimpa shetani wakati mgumu sana.

Kwa kufahamu kuwa kuna mbegu ya mwanamke ambayo imemkanyanga kichwani, shetani ameamua kushambulia kila mwanamke kwa sababu hajui ni mwanamke yupi anaweza kuzaa mbegu hatari kwake. Kwa hiyo alianza mipango yake dhidi ya wanawake kwa kupotosha, kuchafua, kuwashushia hadhi na kuwafanya wanawake wadharaulike katika jamii.

Kama wanawake wangejua wako katika vita kali, wangeacha kubaki katika hali ya ulimbukeni na kupanga mashambulizi dhidi ya adui yao shetani. Kila mwanamke anatakiwa kusimama katika nguvu na uweza wa Mungu kumiliki kilicho halali yake.

Ndio maana leo hii, wanawake ni wengi sana katika nyumba za ibada . Isitoshe, wanawake wanaweza kuomba kuliko wanaume, wanaongeza idadi ya watu kupitia watoto wao na mwanamke ni mzazi wa mwanaume.

Vile vile mwanamke ni mama wa kila kilicho hai. Hakuna kiumbe kilichozaliwa duniani bila kupitia kwa mwanamke, iwe ni wanyama, wadudu na binadamu. Wanawake hujenga nyumba.

Kitabu cha Mithali 14:1, “Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe”. Pia soma Mithali 31: 10-31 inazungumzia uhodari wa mwanamke.

Kwanini mwanamke ni muhimu? Yeye ndiye anayelea watoto katika hali ya uvumilivu , huhimili mateso(mfano manyanyaso ya mume, ndugu n.k. Mwanamke anahusika na jiko ambalo ni moja ya ofisi zake, kujali , upendo na mjasiriamali.
Jiko lisipokaa sawa wakati mwingine humpeperusha mwanaume. Chakula kitamu kimekuwa sumaku kwa kinababa wengi.

Njia ya kuupata moyo wa mwanaume ni kupitia chakula. Ndio maana jiko humpa mwanamke umuhimu mkubwa. Mithali 31:15, “Tena huamka, kabla haujaisha usiku, huwapa watu wa nyumbani kwake chakula; na wajakazi wake sehemu yao”.

Kwa ujumla, mwanamke anapaswa ajitambue, ajue kuwa bila kusimama imara kiimani hataweza kushinda hila ovu za shetani. Ni muhimu amtangulize Mungu mbele katika kila jambo alifanyalo ili kuzuia nguvu za adui.

Hebu angalia mstari huu; Ufunuo wa Yohana 12:17, “Joka (shetani) akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu…”

Shetani ana maajenti wake katika sura tofauti; aweza kuwa nduguyo, mzazi wako, rafiki yako, mchawi, mganga wa kienyeji. Wanawake wengi wamejikuta wakizongwa na mikosi, balaa, magonjwa, vikisababishwa na maajenti hao. Siyo kila unayemuona na kucheka, kula, kushirikiana naye ni mwema kwako.

Wengine ni maadui waliojificha wakijaribu kudhoofisha nguvu alizokuzokupa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafanikio yako. Lakini mwanamke ukisimama kwa kufunga na kuomba, maombi yako yatapata kibali mbele za muumba wetu.

Niishie hapa kwa leo, ukiwa na maoni kuwa huru kuwasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com au flora.wingia@guardian.co.tz