Azam yazipiga bao Yanga, Simba

12Mar 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Azam yazipiga bao Yanga, Simba

“ATANGULIAYE kufika huchagua pa kukaa,” walisema wahenga. Anayefika mahali mapema huweza kuchagua pa kukaa kabla ya wengine hawajafika. Ni methali inayotuhimiza tuwe na tabia ya kuwahi vitu mapema.

Kiumri, Azam FC ni kama mjukuu kwa Yanga na Simba. Yanga SC ilianzishwa mwaka 1935 na mwaka 1936 ikaundwa Sunderland inayoitwa sasa Simba SC.

Yanga na Simba zilipoanzishwa ziliandikishwa kuwa vilabu vya burudani mbalimbali, ikiwemo kandanda (sports). Ni kweli, kuna wakati klabu hizo zilikuwa na michezo mingine kama netiboli na hatimaye ndondi, lakini kadiri muda ulivyopita, michezo hiyo ilikufa vifo vya mende.

Ni wakati ambao Yanga na Simba zingepaswa kubadili majina yao kutoka Sports Club kuwa Football Club yaani Young Africans Football Club (YAFC) na Simba Football Club (SFC).

Hazikufanya hivyo na majina yao yameendelea kuwa kama yalivyo, tofauti na maudhui yake. Pamoja na hayo, bora zingekuwa na maendeleo mazuri katika soka lakini ni ubabaishaji mtupu na ushirikina usiokuwa na kikomo. Zingali kwenye enzi za zana za mawe (stone age)!

Ingawa Yanga na Simba zilitangulia kuwepo katika ulimwengu wa kandanda takriban miaka 80 na ushei iliyopita, zimeshindwa kabisa kujitafutia nafasi nzuri ya kujiendeleza. Zimethibitisha usemi wa “kutangulia sio kufika.”

Azam FC ya miaka takriban saba iliyopita imezifunga Yanga na Simba mabao ya kisigino na inaendelea kufanya hivyo karibu kila mwaka.

Yanga na Simba zaoneshwa njia lakini zingali kwenye mzubao (hali ya kuemewa inayozifanya zishindwe kufanya jambo upesi; bumbuazi) wa kutojua kinachoendelea wala cha kufanya!

Kuhusu usafiri, Azam FC imezitangulia Yanga na Simba kuwa na gari la kisasa la wachezaji. Imekuwa ya kwanza kuwa na viwanja vyake vya kisasa kwa ajili ya mazoezi na mechi.

Imezitangulia kuwa na mambo yote yanayohitajika kwa klabu – sehemu ya mazoezi ya viungo, bwawa la kuogelea, hosteli na zahanati ya wachezaji.

Majuzi, wachezaji walipokwenda Afrika Kusini kupambana na timu ya Bidvest Wits ya huko, suti walizovaa zilipendeza kuziona.

Ziliwakaa wachezaji na maofisa walioandamana nao kiasi cha kumsisimua yeyote aliyewaona wachezaji hao pale uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam. Yote hayo ni mabao ya kisigino dhidi ya Yanga na Simba.
Mara ngapi Yanga na Simba zimekwenda kucheza michezo ya kimataifa (kama zinavyojiita – ‘wa kimataifa’) lakini huenda kama watu waliookotezwa haraka haraka katika mitaa ya Kariakoo na Jangwani?

Nakumbuka Yanga walipokwenda Kigali, Rwanda, walimtembelea Rais Paul Kagame wa nchi hiyo lakini waliingia Ikulu kama watalii wakiwa wamevaa jezi (mavazi rasmi ya michezo yanayovaliwa na wachezaji wa timu).
Haikuwa fedheha (jambo la aibu) kwao tu bali hata kwa mwenyeji wao, Rais Kagame!

Wachezaji wa Yanga walipoalikwa Bungeni kule Dodoma kupongezwa kwa kutwaa Kombe la Kagame, badala ya kuvaa mavazi rasmi kwa kuliheshimu Bunge, waliingia kama wanavyoingia uwanja wa mpira wakiwa wamevalia jezi!

‘Mjukuu’ wa Yanga na Simba anayeitwa Azam SC ndiye anayewaongoza kwa kila jambo. Ingawa ‘mjukuu’ huyo anaongoza kwa vitendo.

Magari waliyo nayo wamepewa bure na wafadhili wao, Tanzania Breweries Limited (TBL). Kambi za timu hizo ni katika hoteli mbalimbali.

Azam inapojiandaa kwa mechi, huwa kwao Chamazi. Mababu zao wakiwa na mechi hukimbilia Zanzibar, Pemba, Bagamoyo au Morogoro wanakoingia gharama kubwa.

Hufuata kile wanachokiita ‘kachumbari.’ Twajua pilau hunoga inapokuwa na kachumbari ila ‘kachumbari’ ya uwanjani sijui huwaje. Ushirikina mtupu!

Viongozi wanavyojinadi wakati wa kuomba kura kwa wanachama na wanavyofanya baada ya kuingia madarakani ni tofauti kama maji na mafuta! Wanachama wa Yanga na Simba wataamka lini?

marobarnabas@yahoo.com
0715/0784 33 40 96