Chadema na mikakati ya kuifanya Iringa mjini kuwa jiji

06Jan 2016
Nipashe
Chadema na mikakati ya kuifanya Iringa mjini kuwa jiji

KILA unapofanyika Uchaguzi Mkuu, wanasiasa hutumia kipindi hicho kutoa ahadi mbalimbali kwa wananchi ambao ni wapigakura.

Mbunge wa Iringa mjini Chadema, Peter Msingwa

Wanasiasa hao ni madiwani, wabunge pamoja na wale wanaogombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia vyama mbalimbali vya siasa.Ni kipindi kizuri kama kila mwanasiasa atatimiza kile alichokiahidi kwa wananchi wakati akiomba kura.
Peter Msigwa ni miongoni mwa wanasiasa aliyetoa ahadi mbalimbali kwa wapigakura wake katika jimbo la Iringa mjini.
Msigwa amekuwa mbunge kwa kipindi cha pili sasa baada ya kile cha miaka mitano kilichoanzia mwaka 2010 kumalizika mwaka jana.
Mwaka jana katika Uchaguzi Mkuu, Msigwa ambaye alipeperusha bendera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alichaguliwa tena na kumshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Frederick Mwakalebela aliyegombea kupitia (CCM).
Ulikuwa ushindani mkali kati ya vyama viwili vya CCM na Chadema, kabla ya wananchi kuamua ni nani wangetaka awe mwakilishi wao bungeni kupitia nafasi ya Ubunge.
Miongoni mwa vipaumbele kwa wagombea wote wa udiwani, ubunge na urais vilikuwa ni pamoja na kuboresha elimu, kujenga viwanda, kuendeleza kilimo, kujenga miundombinu ya reli, barabara, kuzalisha umeme wa uhakika na kuboresha mfumo wa utawala na kusimamia sheria.
Mwanasiasa huyu anaamini kwamba ikiwa atatekeleza ahadi zake kwa wananchi wa Iringa mjini, maendeleo ya kweli yanaweza kupatikana katika kipindi cha miaka mitano.
Kwa bahati mbaya, Msigwa anasema wanasiasa wengine pengine kwa hofu ya kukosa kura za wananchi wanashindwa kuuuliza nafasi ya kila mwananchi mmoja mmoja katika kuchangia maeneo yake binafsi.
Anaamini kwamba kuna namna mbili za wananchi kupata maendeleo ya kweli, moja ni kwa kuchagua viongozi bora ambao wanasikiliza na kutatua shida zao na njia nyingine ni wao wenyewe kujituma.
Hii njia ya pili anaamini kwamba kila mwananchi anatakiwa kutumia vizuri fursa zinazomzunguka na kwamba ni makosa makubwa kufikiri kuwa ataletewa kila kitu na viongozi wa kisiasa.
Jitihada binafasi za mtu ni muhimu kuliko kusubiri ahadi za wanasiasa kwa kuwa bila kuunganisha vyote viwili ni vigumu mwananchi kufikia malengo yake.
Msigwa ambaye ni miongoni mwa wanasiasa waliolitikisa Bunge la 10 kwa hoja nzito, anasema Watanzania wengi hawafanikiwi maisha kwa sababu ya kupenda njia za mkato.
Lakini pia anasema watu wengi wanadhani kutokuwa na pesa ni tatizo, wakati ukweli ni kwamba tatizo kubwa ni kutokuwa na wazo la namna ya kupata pesa.
''Unapokuwa na wazo unakuwa na uwezo wa kuanzisha na hata kubadili kila kitu katika maisha,'' anasema .
“Taifa lolote ili liendelee linatakiwa kuwa na watu wenye uwezo kielimu, nidhamu, watafiti na kwamba vitu vipo, lakini tunashindwa kujua ni jinsi gani ya kutumia vipawa hivyo kwa ajili ya maendeleo yetu na ya taifa kwa ujumla na hivyo kubaki kulalamika tu,” anasema Msigwa.
Mbunge huyo anasema mtu akitaka kuwa mjasiriamali lazima asome vitabu vya ujasiriamali, akitaka kuwa mwanasiasa atafute vitabu vya siasa na ukitaka kubadilisha namna ya kufikiri anapaswa kusoma mambo yanayoweza kubadilisha fikra zake.
“Tusipende kuwa wafuasi bali tuwe wanafunzi, mfuasi hufuata lolote, liwe baya au jema, lakini mwanafunzi huchota taarifa na maarifa na kuzifanyia kazi kwa ajili ya kujijengea uwezo wa kufanya yawe na manufaa kwake,”anasema Msigwa.
Anasema kuwa watu wengi wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea bila ya kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa, wengi wamejikita katika kukuza vipato vyao vya kiuchumi badala ya kujiendeleza wao wenyewe ili wawe watu bora.
Kanuni ya tatu ni kujiwekea malengo ambayo yatamsaidia kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
“Watu wengi hawana malengo, malengo ni kama dira baharini imsaidiayo baharia kujua mwelekeo, mtu yeyote anayeishi pasipo malengo kamwe hawezi kujua anaelekea wapi,” anasema mwanasiasa huyo machachari.
Anabainisha kwamba kuna aina mbili za malengo yakiwamo ya muda mfupi na muda mrefu ambayo mtu anaweza kujiwekea ili kufikia mafanikio.
Katika uchaguzi uliopita, Msigwa alifanikiwa kutetea kiti chake huku chama chake cha Chadema kikipata madiwani 14 kati ya kata 18.
Kwa matokeo hayo Chadema kiliandika historia ya kuongoza halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Chadema kupitia kwa Meya wa mji wa Iringa, Alex Kimbe kimetangaza kupandisha pato lake la ndani kutoka shilingi bilioni mbili kwa sasa hadi kufikia shilingi bilioni saba ili kupata fedha za kuboresha huduma muhimu za kijamii.
Kimbe anasema Chadema kimeanza kazi rasmi na kinalenga kuujenga mji wa Iringa ili ufikie hadhi ya kuwa jiji.