Mwenyekiti huyo, Jecha Salum Jecha kwa niaba ya ZEC alifikia uamuzi huo kwa madai kwamba uchaguzi huo ulikuwa na kasoro ya kuwapo idadi kubwa ya wapigakura kuliko watu waliojiandikisha kupigakura katika vituo mbalimbali hususan kisiwani Pemba.
Uchaguzi huo na matokeo yake yaliyokuwa yameanza kutangazwa ulifutwa siku mbili baada ya kufanyika Oktoba 25 mwaka jana.
Kufuatia hatua hiyo ya ZEC mpaka sasa utata umezidi kuongezeka juu ya hatma ya visiwa vya Unguja na Pemba ikizingatiwa kuwa muda wa ukomo wa urais wa Dk. Ali Mohamed Shein ulikwisha Novemba 2, 2015.
Aidha, kipindi kinachotolewa kwa Rais aliyemaliza muda wake kukaa bila Baraza la Wawakilishi kwa mujibu wa ibara 28 (1), inayotoa kipindi cha mpito kwa Rais aliyemaliza muda wake kuendelea kuwepo madarakani hadi Rais anayefuatia atakapokula kiapo na kuitisha Baraza la Wawakilishi katika muda usiozidi siku 90 tangu lilipovujnwa nao umekwisha rasmi.
Ifikapo Januari 12, 2016 kipindi hicho kitakuwa kimekwisha na baada ya hapo Zanzibar itakuwa imerejea katika utawala wa amri (decree rule) wa miaka ya 1970.
Hakuna anayejua nini kitafanyika kuvinasua visiwa hivyo kutoka katika hali hiyo na lini?
Aidha, binafsi nakerwa sana na ukimya uliopo ndani ya Tanzania na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika (AU) juu ya hali inayoendelea Zanzibar.
Imefikia wakati nimejiuliza swali, je, tunasubiri mpaka damu imwagike ndipo tuanze kujitokeza kusaidia suluhu ya mgogoro wa kikatiba na kisiasa ndani ya Zanzibar?
Kwa sababu hiyo, makala hii ni mchango wangu kuanza kuhamasisha utafutaji suluhu ya kudumu kwa mgogoro wa Zanzibar.
Naanza kwa kujadili mambo sita ya utata kufuatia kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar!
Kwanza ni utata kisheria na kikatiba ambao unahoji ni uchaguzi gani umefutwa?
Sambamba na hilo ni sababu zipi zilizosababisha uchaguzi huo kufutwa.
Hapa pana shida kubwa sana kwa maoni yangu. Ingawa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ni Tume huru kwa masuala ya uchaguzi wa Zanzibar iliyoanzishwa chini ya ibara ya 119 katika sura ya Tisa ya Katiba ya Zanzibar, Tume hiyo hiyo kwa namna moja au nyingine ni wakala wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa masuala yahusuyo uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao husimamiwa na kuratibiwa ya NEC.
Kwa kuwa maelezo ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha, uchaguzi ulifutwa kutokana na kasoro lukuki zilizofanya uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015 usiwe huru wala wa haki kutokana na sababu tisa alizozieleza kuhalalisha ubatili wa uchaguzi huo, utata unaoibuka ni je, kasoro nyingi na hatari namna ile zilitokeaje?
Swali lingine la kujiuliza ni namna gani kasoro hizo hazikuathiri uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika kwa upande wa Zanzibar ambao ulifanya siku hiyo kwa kumchagua Rais wa Muungano.
Badala yake kasoro hizo zikajikita kwa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani pekee.
Utata huu ungeweza kutatuliwa kwa kutolewa maelezo ya kina kuhusu uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania visiwani Zanzibar kuwa labda tofauti ya kura zote za utata zilizompigia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokea Zanzibar hata zisipojumlishwa upande wa mshindi haziwezi kubadili matokeo.
Hii ni hoja nzito na imewahi kutumika hivyo katika baadhi ya nchi.
Hata hivyo, nusu ya utata unabaki kuhusu uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hawa kwa namna yoyote ile hawawezi kukwepa mtego wa kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wao kwa kutumia sababu zile zile tisa alizozitumia Jecha na kuamua kufuta uchaguzi wa Rais, Wawakilishi na Madiwani wa Zanzibar.
Swali kubwa ni moja kwa nini uchaguzi wa wabunge 54 kutoka Zanzibar umeonekana kukwepa madhambi yote tisa aliyoyaibua Jecha? Huo ni utata !
Aidha, utata mwingine ambao haujaonwa na kuzungumzwa na watu wengi ni ule unaohusu mamlaka iliyofuta uchaguzi wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Ibara ya 119, Tume ya uchaguzi ndicho chombo chenye mamlaka halali ya kuitisha, kuendesha na hata kufuta uchaguzi.
Nikiamini maneno ya Jecha, Tume katika dakika za mwisho ilivunjika na kuparanganyika kama chombo wakati na baada ya kuacha kufanya kazi kama Tume na kuvua mashati na kuanza kupigana.
Kwa maelezo haya, Tume iliacha kufanya kazi kama chombo chenye mamlaka na kuingia katika mgogoro ambao mpaka le haujaisha na wala hauelekei kuisha.
Swali kuu hapa ni je, nani alifuta uchaguzi wa Zanzibar? Kama ni Tume ya Uchaguzi Zanzibar, ilipaswa tujulishwe ni kwa azimio lipi, la kikao kipi kilichoketi lini na wapi?
Kama ni Jecha aliyefuta uchaguzi, nataka kuamini kuwa hana mamlaka hayo kikatiba na kama kuna kifungu cha sheria ya uchaguzi kinachomruhusu kufuta uchaguzi akiwa peke yake kama Jecha, uhalali wa kifungu hicho ni vema ukapimwa ili kujiridhisha kama si batili kikatiba.
Nijuavyo mimi, mwenyekiti angeweza kuchukua hatua kadhaa yeye mwenyewe kuhusu nidhamu ya Makamishna wa Tume, lakini kamwe asingeweza kuruhusiwa kuchukua maamuzi ya kufuta uchaguzi yeye mwenyewe kama mtu pasipo maamuzi yoyote ya vikao halali vyenye akidi vya Tume ya uchaguzi Zanzibar.
Kwa vyovyote ilivyokuwa, hapa kuna utata mkubwa juu ya nani hasa aliyefuta uchaguzi wa Zanzibar.
Mbaya zaidi, kuna suala lingine lenye utata kuhusu maelezo ya sababu za kufutwa kwa uchaguzi yaliyotolewa na Jecha.
Kwa mdomo wake, Jecha alisema kuwa baadhi ya Makamishna waliamua kuacha kuwa wajumbe wa Tume na kuwa wawakilishi wa vyama vya siasa.
Swali hapa ni je, nini hasa walichokifanya mpaka kuwafanya wapoteze sifa ya kuwa wajumbe wa ZEC kikatiba?
Nimkumbushe Jecha kuwa kufuatana na Katiba ya Zanzibar ibara ya 119 (1) (b) na ( c), wajumbe wa Tume wanne watapatikana kwa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar kutokana na mapendekezo ya chama tawala na chama kikuu cha upinzani katika baraza la wawakilishi.
Swali hapa ni je, ubatili wa wajumbe hawa wanne ulitokana na matendo yao maovu ndani ya Tume au kwa kuwa wanatokana na vyama vya Siasa?
Kama ni lile la kwanza, walifanya nini kiovu kuwafanya wawe na ubatili wa kiwango alichoeleza Jecha na je, ubatili huo usingetosha kuwachukulia hatua ndani ya Tume na kuokoa uchaguzi wa Zanzibar?
Utata huu na ule mwingine unaofanana nao wa kwamba fomu nyingi za matokeo hasa kutoka Pemba zilionekana kuchezewa kwa nambari zake kufutwa na kubadilishwa nyingine unaonesha jinsi Tume ya Uchaguzi Zanzibar ilivyokosa uongozi na uwezo wa kuendesha zoezi la uchaguzi na kwamba inaonekana ingepaswa Tume ndiyo iwajibike kwa kukosa uwezo wa kiutendaji badala ya kuwajibisha Zanzibar nzima kwa kufuta uchaguzi? Hapa pana utata mkubwa sana !
Zaidi ya hayo, kuna masuala mengine matatu ya utata. Kwanza, suala la baadhi ya watu walioripotiwa na Jecha kupiga kura huku vitambulisho vyao vikiwa mikononi mwa ZEC lina utata mwingi.
Watanzania wanakumbuka kuwa kwa mfumo wa BVR, zoezi la kujiandikisha lilikuwa linafanywa na kukamilika kituoni pale pale na kila mtu kukabidhiwa kadi yake ya mpiga kura.
Sasa swali ni je, vitambulisho alivyovielezea Jecha na kwa wingi alioueleza vilibaki vipi ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar?
Ni uzembe gani ulitokea kwa Tume ya uchaguzi Zanzibar mpaka kushindwa kuwakabidhi Wazanzibari wengi kiasi hicho vitambulisho vyao? Je, watu hao waliweza vipi kupiga kura kama hawana vitambulisho au ruhusa ya ZEC kuwa wapige kura? Je, majina yao yalikuwamo au hayakuwemo katika daftari? Je, huu wote ni uzembe wa nani?
Huu ni uzembe wa watumishi wa Tume ya Uchaguzi au wananchi wapigakura wa Zanzibar?
Na je, suluhu ya matatizo ya uchaguzi yanayotokana na makosa ya Tume na watendaji wake yanapaswa kubatilisha uchaguzi wa nchi nzima kama ilivyotokea kwa Zanzibar?
Je, kama kuna maeneo ambako kasoro hizo zilitokea, kwa nini uchaguzi usingerudiwa katika maeneo hayo machache pekee?
Pia, Jecha anasema baadhi ya vyama vilionekana kuingilia kazi na majukumu ya Tume ikiwamo kujitangazia ushindi na kuleta malalamiko na mashinikizo kutoka vyama vingine na wapiga kura kwa Tume.
Mashinikizo hayo ndiyo yaliyochangia kufutwa kwa uchaguzi?
Kwa kuwa jibu ni ndiyo, je, uhuru wa Tume uko wapi katika kuandaa, kusimamia na kuratibu uchaguzi? Je, sheria inasemaje juu ya wanaovunja sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi?
Nani amechukuliwa hatua kwa kuvunja sheria na maadili hayo? Je, kuna utata wa kisheria au kikatiba juu ya wanaovunja sheria na maadili ya uchaguzi? Je, kwa kukubali kupokea mashinikizo hadi kufuta uchaguzi Tume inajiona kuwa bado ina nguvu ya kisheria na kikatiba kuendelea kuandaa uchaguzi mwingine wa marudio ikiwa haijatatua tatizo lililotokea ndani yake? Je, matatizo yaliyotokea katika uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba yataepukika vipi katika uchaguzi wa marudio siku yoyote utakapopangwa kufanyika? Je, vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi vitakubali vipi kurudiwa kwa uchaguzi wakati wasimamizi ni wale wale?
Mwisho, kuna suala lenye utata juu ya nini kinapaswa kufanyika kwa hatua hii Zanzibar ilipofikia.
Kwa sasa nchi ipo katika mgawanyiko kati ya wanaosema uchaguzi unapaswa kurudiwa na wanaosema haurudiwi uchaguzi bali uhakiki wa matokeo ukamilishwe katika majimbo 23 yaliyokuwa yamesalia mpaka Jecha anatangaza kufutwa kwa uchaguzi.
Wakati anatangaza kufuta matokeo na uchaguzi wote majimbo 31 tayari yalikuwa yamehakikiwa.
Suluhisho la haya ni kukamilisha zoezi hili na kutangaza matokeo ya uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba ili Baraza la Wawakilishi lianze kazi kama katiba ya Zanzibar inavyotaka.
Swali kubwa linabaki ni nani anayeweza kufanya haya ikizingatiwa kuwa Tume ya uchaguzi hivi sasa ipo vipande vipande na muda wa mtu mwenye mamlaka ya kuteua Tume ambaye ni Rais wa Zanzibar umekwisha kikatiba?
Ndiyo maana nadhani suala hili nalo lina utata mkubwa kiasi kwamba ufumbuzi wake hauwezi kukwepa kuhusisha Jumuiya ya Kimataifa.
Ninavyoona mimi Zanzibar ilipofikia hivi leo ni hali kama ya wakati kulipohitajika usuluhishi wa Kimataifa ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Chief Emeka Anyaouku.
Kinachonishangaza ni kwa nini Watanzania na Wazanzibari wote bado tuna usingizi wa kudhani kuwa mgogoro huu ni mdogo na tutaumaliza.
Hivi ni kweli mazungumzo yanayohusisha CUF na CCM yakishirikisha Maalim Seif Sherrif Hamad na Dk. Ali Mohamed Shein na kuratibiwa na Rais msaafu Jakaya Mrisho Kikwete na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan yatazaa matunda?
Matunda yenyewe yatakuwa ni matunda ama sumu? Naona kama tunajidanganya na kujichelewesha bure huku kila upande ukiwa na malengo yake.
CUF kwa sasa wanasubiri matokeo yatangazwe, CCM wanasubiri uchaguzi urudiwe chini ya ulinzi mkali wa Polisi na Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Hapa kwa utaalamu wangu wa usuluhishi wa migogoro hapatatokea suluhu yoyote mpaka watu ambao si sehemu ya mgogoro huu waweze kushika hatamu za usuluhishi.
Masuala mengine ya utata wa kiutawala na jinsi ambavyo Zanzibar sasa inapaswa kuwa katika mpito wenye serikali ya uangalizi.
Suala hili linaweza kumalizwa pia na Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kutoa tafsiri za kisheria juu ya kinachotokea Zanzibar.
Wiki ijayo nitaendelea kujadili suala hili ili mwisho wa siku Watanzania wafahamu ukweli kuhusu sakata la Zanzibar.









