Wanaume wanaweza kuepukana na jail hizi kwa kuwa waangalifu

09Mar 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Wanaume wanaweza kuepukana na jail hizi kwa kuwa waangalifu

KATIKA toleo letu la jana tulichapisha habari ikieleza jinsi ajali nyingi za barabarani zinavyowaathiri wanaume vikiwamo vifo na ulemavu.

Ilielezwa kwamba idadi ya wanaume inaweza kuendelea kushuka mwaka hadi mwaka kutokana asilimia 90 ya wanaopoteza maisha au kupata ulemavu kwenye ajali kuwa wa jinsia hiyo.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2011 na 2015, watu waliofariki dunia kutokana na ajali za barabarani ni 19,180, wanaume wakiwa 15,169 na wanawake 4,011.

Mwaka 2011, waliofariki walikuwa 3,981, wanaume wakiwa 3,125 na wanawake 856 huku majeruhi wakiwa 20,802 kati yao wanaume ni 15,750 na wanawake 5,052.

Mwaka 2012, vifo vilikuwa 3,969 kati yake wanaume wakiwa 3,129 na wanawake 840, huku majeruhi wakiwa 20,111 idadi ya wanaume ikiwa 15,088 na wanawake 5,023.

Kwa mwaka 2013, waliofariki walikuwa 4,002 wanaume wakiwa 3,197 na wanawake 805. Majeruhi walikuwa 20,689, kati yao wanaume 15,488 na wanawake 5,201. Mwaka 2014, waliofariki walikuwa 3,760, wanaume 2,965 na wanawake 795 na majeruhi 14,530 wanaume 10,686 na wanawake 3,844.

Mwaka 2015, watu waliofariki walikuwa 3,468 wanaume wakiwa 2,753 na wanawake 715 huku majeruhi wakiwa 9,383 kati yao wanaume 6,883 na wanawake 2,500.

Kadhalika, waliojeruhiwa kutokana na ajali hizo ni 85,515 wanaume wakiwa 63,895 na wanawake 21,620.

Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, kinabainisha sababu kadhaa zinazosababisha hali hiyo kwamba ni pamoja na wanaume wengi kuwa wazembe wanapotumia vyombo vya moto au barabara. Nyingine ni wanaume wengi kutumia kilevi zaidi ikilinganishwa na wanawake.

Kwamba wanawake ni waangalifu wanapotumia vyombo vya moto au kutumia barabara, idadi kubwa ya wanaume kuwa ndio madereva ilikinganishwa na wanawake na kwamba wanaume ndio wanaotafuta riziki ya familia ndio wengi, hivyo hujikuta wanatumia barabara au vyombo vya moto.

Inawezekana kuna sababu nyingine zinazochangia hali hiyo, lakini takwimu hizi zinatosha kueleza kwamba hali hiyo ni hatari, inatisha na inapaswa kutafutiwa ifimbuzi wa kudumu.

Sababu kubwa ambayo inasababisha wanaume kuwa waathirika wa ajali za barabarani ni ulevi. Dereva ambaye amepata mafunzo ya kutosha na anyeheshimu na kuzingatia sheria za usalama barabarani hawezi kuendesha gari akiwa ametumia kilevi.

Mtu aliyetumia kilevi kupita kiasi hawezi kufanya mamuzi yoyote ya maana, hivyo ni dhahiri kuwa anapotumia kilevi na kuendesha gari uwezekano wa kupata ajali ni mkubwa sana.

Kwa kuwa takwimu hizo zinaonyesha kwamba wanaume wanaongoza kwa kuathiriwa na ajali kuliko wanawake, ipo haja ya kuzifanyia kazi sababu ambazo zimebainishwa na Jeshi la Polisi kwamba ndizo zinazosababisha ajali hizo.

Wanaume wahakikishe wanakuwa makini wanapotumia vyombo vya moto barabarani badala ya kuendekeza uzembe ambao mwisho wake ni mauti kwao, lakini pia waachane na kuendesha vyombo vya moto wakiwa wametumia vileo.

Madai kwamba wanaume ndio watafutaji wa riziki katika familia sio sababu ya kuwafanya watumie vyombo vya moto barabarani na kusababisha ajali, bali huo ni uzembe na ukosefu wa umakini.

Tunasikitishwa na kuongezeka kwa ajali hizo ambazo zinapunguza nguvu kazi ya taifa, lakini ushauri wetu ni kuwa njia pekee ya kuziepuka ni kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani.