Huduma ziboreshwe hospitali za rufani, mikoa

10Mar 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Huduma ziboreshwe hospitali za rufani, mikoa

KATIKA toleo letu la jana tulichapisha habari ikieleza kuwa hali ya huduma katika hospitali za rufani na za mikoa ni mbaya.

Habari hiyo chanzo chake ni uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti hili katika hospitali kubwa za mikoa na rufaa, ukionyesha kuwa hali ni mbaya kutokana na kukosekana kwa huduma ya vipimo muhimu, wauguzi, madaktari na madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali.

Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo kuna ukosefu wa watumishi na vipimo muhimu. Ina daktari mmoja wa magonjwa ya wanawake sambamba na upungufu wa wauguzi wakunga zaidi ya 40, hali inayosababisha muuguzi mkunga mmoja kuhudumia wastani wa wa wanawake zaidi ya 24 kwa akiwa zamu ya saa nane.

Hospitali ya Rufani Kitete mkoani Tabora, ina ukosefu wa dawa na vifaa tiba na huku wajawazito wakilala wawili kwenye kitanda kimoja pamoja na watoto wao baada ya kujifungua na wengine kulazimika kujifungulia chini. Hospitali ya rufani ya Mkoa wa Dodoma haina kipimo cha X-ray kutokana na kuharibika, hivyo wagonjwa kwenda hospitali ya nje.

Pia hakuna vipimo vya MRI wala CT-Scan sambamba na upungufu wa watumishi 108 wakiwamo madaktari bingwa saba.

Katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya baadhi ya vipimo havipo zikiwamo mashine za CT-Scan na MRI.

Hospitali ya Rufani ya KCMC ya Moshi haina MRI, CT-Scan na X-ray zinafanya kazi kwa kiwango kidogo kutokana na kuzeeka pamoja na kuwa na vitanda 585, ambavyo havitoshelezi mahitaji ya wagonjwa. Pia ina upungufu wa wauguzi 230, madaktari 102 na haijawai kuwa na mashine ya MRI huku ST-Scan zake tatu muda wake wa matumizi umeisha.

Hosptali Teule ya Rufani ya Tumbi, Mkoa wa Pwani, ambayo inazotegemewa sana nchini kwa kuhudumia majeruhi wa ajali zinazotokea mara kwa mara katika Barabara ya Morogoro, chumba chake cha maiti kimezidiwa na kuharibika kwa majokofu.

Matatizo yanayoikabili Hospitali ya Rufani ya Mnazi Mmoja Zanzibar
yanafanana na ya hospitali za mikoa na rufani za Bara kama kuharibika kwa X-ray muda mrefu, uhaba wa waunguzi na udogo wa chumba cha kuhifadhia maiti ambacho pia hakina barafu ya kutosha kuhifadhi maiti zaidi ya mbili.

Hiyo ndiyo hali halisi katika hospitali zetu za mikoa na rufami. Ukweli wa habari yetu ya uchunguzi kuhusu hali hiyo mbaya ulithibitishwa na mamlaka husika wakiwamo watumishi, madaktari na menejimenti za hospitali hizo, hivyo ni wajibu wa serikali kuhakikisha kwamba matatizo hayo yanapatiwa ufumbuzi haraka.

Moja ya ahadi za serikali ya awamu ya tano ni kuboresha huduma katika sekta ya afya, hivyo ni matumaini yetu kwamba Rais John Magufuli atakuwa ameyabaini matatizo yanayozikabili hospitali hizo na athari wanazozipata Watanzania wanaokwenda kupata matibabu.

Katika siku zake za mwanzoni baada ya kuapishwa, Rais Magufuli alionyesha kuwa anayo nia ya dhati ya kuboresha mazingira na huduma katika hospitali za serikali.

Itakumbukwa jinsi Rais Magufuli alivyoanza kwa kuhakikisha mashine ya ST-Scan, MRI, vitanda, magodoro pamoja na mashuka vinapatikana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Ni matumaini yetu kwamba serikali itachukua hatua za kupeleka dawa za kutosha, vifaa tiba, kuongeza idadi ya madaktari na wauguzi, kukarabati majengo na kuwapa motisha watumishi wa sekta ya afya ili kiwe kichocheo cha kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.