Wanawake itumiemi siku yenu kujitathmini

08Mar 2016
Mhariri
Nipashe
Wanawake itumiemi siku yenu kujitathmini

LEO wanawake nchini wanaungana na wenzao duniani kuadhimisha siku ya Wamawake Duniani. Siku hiyo huadhimishwa Machi 8, kila mwaka kwa wanawake kuainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili na kueleza mikakati ya kuzitatua.

Wanawake na watoto wa kike wamekuwa wakikabiliwa na vitendo mbalimbali vya ukatili na udhalilishaji kama ukeketaji, vipigo, kutelekezwa, ubakaji, mimba na ndoa za utotoni, kutopewa nafasi katika vyombo vya maamuzi, kunyimwa fursa za elimu, kumiliki mali na kurithi mali kwa kutaja baadhi.

Hata hivyo, hatua zimekuwa zikichukuliwa zikiwamo mafunzo, uhamasishaji pamoja na ushauri nasaha kwa waathirika wa matukio ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa lengo la kuhakikisha kwamba vitendo hivyo vinapungua kama siyo kukomeshwa kabisa.

Asasi kadhaa pia zimekuwa zikifanya tafiti kubaini matukio ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia katika maeneo mbalimbali nchini na kuendesha kampeni za kupambana na vitendo hivyo.

Miongoni mwa jitihada zinazofanya na asasi na wanaharakati wa masuala ya wanawake nchini kwa miaka ya karibuni, ni kuhakikisha Tanzania inatekeleza mikataba mbalimbali ya kimataifa kuhusua haki za wanawake ambayo iliisaini na kuiridhia.

Mikataba hiyo ni ya kuongeza idadi ya wanawake katika vyombo vya maamuzi kama udiwani, ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi. Kwa mfano, baada ya maaazimio ya Mkutano wa Nne wa Dunia wa Wanawake uliofanyika Beijing, China mwaka 1995 na kuazimia kuwa nafasi za wanawake zifikie asilimia 25.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 maazimio hayo yalitekelezwa nchini na kufuatiwa na Mkataba wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) kwa kuongeza idadi ya wanawake katika vyombo hivyo vya maamuzi na kufikia asilimia 30 mwaka 2005.

Hivi sasa jitihada za wanawake nchini zinaendelea kushika kasi kutekeleza Mkataba wa Muungano wa Afrika (AU) wa Maputo wa kuwa na asilimia 50 kwa 50 kati ya wanaume na wanawake katika vyombo vya maamuzi kwa mana ya mabaraza ya madiwani, Bunge na Baraza la Wawakilishi ifikapo mwaka 2030.

Suala hili linapewa msukumo mkubwa huku kaulimbiu ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu ikiwa ni ’50 kwa 50 ifikapo 2030’.

Kimsingi, tunaridhishwa na hatua zinazofanywa na wanawake nchini za kudai usawa katika nafasi za uongozi na tunawatia moyo waendelee kuzidai ili taifa letu liwe la usawa wa kijinsia.

Tunawashauri wanawake watumie maadhimisho ya siku yao mwaka huu kujitathmini kuona mafanikio na mapungufu yao ili iwe rahisi kufikia lengo la 50 kwa 50 ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo, tunaamini kuwa lengo hilo linaweza kutimia kabla ya hapo ikiwa kutakuwa na umakini na maadalizi ya kutosha miongoni mwa wanawake wenye nia ya kugombea nafasi hizo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Sapoti iliyotolewa na asasi kadhaa zikiwamo TGNP na Tamwa kwa wagombea wa makundi maalum ikiwamo la wanawake katika uchaguzi uliopita kuanzia mwaka 2002, 2010 na 2015 imeonyesha mafanikio makubwa kutokana na idadi kubwa ya wanawake kuwa madiwani, wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Ni matarajio yetu kwamba asasi hizo na nyingine zitaendelea kuwawezesha wanawake kwa njia ya mafunzo na hata kwa rasilimali ili kuwajengea uwezo wa kujitokeza na kupambana kwenye kata na kwenye majimbo kugombea nafasi hizo. Bila shaka changamoto zinazowakwaza wanawake zitajadiliwa katika maaadhimisho ya leo.