Aliwataka viongozi hao kuwekeza muda mwingi kufanya kazi zenye tija kwa maendeleo ya michezo na kuepuka kuwa sehemu ya migogoro ya uongozi, ambayo moja kiini cha michezo kudidimia.
Lakini pia alizungumzia na kuukemea utamaduni mbaya wa baadhi ya mashabiki wachache wa michezo, hasa soka kuharibu mali za umma kwa kivuli cha ushabiki.
Alizungumza hayo kutokana na utumwa wa baadhi ya mashabiki wa timu kubwa nchini kufanya uharibifu wa kung’oa viti mara kwa mara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Siyo tu uharibu wa kung’oa viti, bali hata mali nyingine za umma kwenye uwanja huyo mkubwa na wenye hadhi ya kimataifa.
Aliwaonya mashabiki wa aina hiyo na kuzitaka mamlaka husika zinazosimamia michezo kuhakikisha kuchukua hatua za kinidhamu dhidi yao.
Hata hivyo, tunasikitia kuona onyo la Waziri Majaliwa limekuwa sehemu ya kuchochea uharibifu kwenye uwanja huo, badala ya kuzuia.
Katika mchezo wa Ligi Kuu Bara mwishoni mwa wiki iliyopita kati ya Yanga na Azam kwenye uwanja huo, mashabiki wasiokuwa na uchungu wa mali za umma, walifanya kile ambacho Waziri Majaliwa alikemea.
Bila aibu, mashabiki hao, waliamua kung’oa viti vya uwanja na kuvitumia kama sehemu ya kujiami baada ya kuzuka vurugu kati yao.Sisi kama wapenda michezo, tunasikitishwa na aina hii ya ushabiki usio na nidhamu wala uchungu na mali za umma.
Serikali imetumia fedha nyingi kujenga uwanja huo wa kisasa. Ikumbukwe pia, Timu ya Taifa ya Brazil ilikuja nchini na kucheza kwenye uwanja huo wakati ikijiandaa na fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
Kwa timu kama Brazil kuja kucheza Tanzania ni historia, lakini iliwezekana kutokana na kuukubali uwanja huo, ambao sisi leo tunaona si lolote na kufanya uharibifu.
Kabla hata tamko la Waziri Majaliwa kuhusiana na kuutunza uwanja huo, viongozi wengine kadhaa wa kitaifa akiwamo Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete wamewahi kutoa matamko ya kukaripia uharibifu kwenye uwanja huo.
Isitoshe, hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wameshazipiga faini baadhi ya timu kutokana na mashabiki wao kufanya uharibifu wa mali za uwanja.
Kuendelea kwa tabia hii, maana yake adhabu zinazotolewa kwa klabu hazisaidii kukomesha uharibu.
Tunachukua nafasi hii kuziomba mamlaka husika kuchukua hatua kali kwa klabu ambazo mashabiki wake watabainika kuharibu mali za umma.
Lakini pia, adhabu kali zitolewa kwa mashabiki wakatakonaswa wakifanya uharibu huo, ikiwa ni pamoja kulipa gharama za uharibifu na kupelekwa mahakamani.
Tunaamini, kuharibu mali za umma ni sawa na kuhujumu uchumi wa nchi, hivyo mashabiki wa aina hii wachukuliwe kuwa ni wahujumu.
Bila kuweka adhabu kali dhidi ya mashabiki wa aina hiyo, uharibifu hautakoma kwenye uwanja huo. Tuwakumbushe mashabiki wa soka kwamba, toka enzi na enzi, tafsiri ya mchezo huu ni furaha, amani na upendo. Mchezo wa soka haujawahi kuzaa uadui wa kuharibu mali au kutishiana maisha.
Katika mazingira ya sasa, ambayo michezo imekuwa mhimili wa ajira na pato kwa taifa, tusingependa kukuona mashabiki wa aina hii.Ushabiki unaolenga kuleta vurugu au aina yoyote ya kuhatarisha amani, unapaswa kukemewa kwa nguvu zote.










