Yanga iliyoshinda 1-0 Mauritius na 2-0 Dar es Salaam ndani ya wiki mbili, kwa mara nyingine itaanzia ugenini dhidi ya APR, ambayo katika Raundi ya Awali iliitoa Mbabane Swallows ya Swaziland kwa jumla ya mabao 4-1, ikifungwa 1-0 ugenini na kushinda 4-1 Kigali.
Mchezo wa kwanza kati ya Yanga na APR unatarajiwa kuchezwa kati ya Machi 11 kwenye Uwanja wa Amahoro mjini Kigali, wakati mchezo wa marudiano utachezwa wiki moja baadaye mjini Dar es Salaam.
Mapema tu Desemba mwaka jana baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutoa ratiba ya awali ya michuano yake, Watanzania waliipokea kana kwamba Yanga ina mechi mbili nyepesi kabla ya kuanza kukutana na mikiki haswa ya Ligi ya Mabingwa katika Raundi ya Pili, ambako kama itafuzu itakutana na mshindi kati ya Recreativo de Libolo ya Angola na Al Ahly ya Misri.
Lakini ukweli wa mambo sivyo kama inavyozungumzwa kwamba Yanga imepata mchekea mbele ya APR – kwani timu hiyo ya Jeshi la Rwanda ni imara katika nyanja zote na ina misingi mizuri zaidi kiuwekezaji kisoka kuliko timu ya Jangwani, Dar es Salaam.
APR kwa sasa ndiyo inaongoza kutoa wachezaji wengi timu za taifa za Rwanda kuanzia za vijana, timu ya wachezaji wa nyumbani ambayo hivi karibuni ilicheza michuano ya CHAN na kuishia Robo Fainali, ambako ilitolewa na DRC walioibuka mabingwa baadaye.
Miongoni mwao, ni beki wa kati, Abdul Rwatubyaye mwenye umri wa miaka 28, ambaye alifunga mabao matatu peke yake (hat trick) katika ushindi wa 4-0 nyumbani dhidi ya Mbabane Swallows mjini Kigali na kiungo Patrick Sibomana aliyefunga lingine.
Ni APR imara ambayo baada tu ya kufuzu Raundi ya Kwanza, imefanya mabadiliko ya benchi la Ufundi, ikiingia Mkataba na kocha Nizar Khanfir, raia wa Tunisia.
APR imekuwa chini ya kocha wa akademi yake, Emmanuel Rubona tangu kuondoka kwaLjupko Petrovic aliyefuatiwa na Msaidizi wake, Mserbia mwenzake, Dusan Dule wakihamia PFC Litex Lovech ya Bulgaria.
Lakini APR kama Yanga ni miongoni mwa timu bora kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kipindi chote za kuwapo kwao. APR pia imekuwa timu inayoonyesha upinzani mkali kwa Yanga kila zinapokutana.
Katika michuano hii ya Ligi ya Mabingwa Afrika, safari hii inakuwa mara ya pili Yanga kukutana na APR, tena katika hatua hii hii, Raundi ya Kwanza.
Awali, zilikutana mwaka 1996 na Yanga ikatolewa kwa jumla ya mabao 3-1, ikishinda 1-0 nyumbani Dar es Salaam, kabla ya kwenda kufungwa 3-0 Kigali.
Hii inatosha kutoa picha kwamba, APR si timu ya kubeza na inaweza kurudia ilichokifanya miaka 20 iliyopita, iwapo Yanga watashikilia dhana wamepata mchekea na kuacha kuwekeza katika maandalizi mazuri.
Ndiyo maana ya leo, Lete Raha tunawaambia Yanga kwamba; APR si timu ya kubeza, wajiandae kikamilifu, vinginevyo Rwanda Air itakuwa ndege yao ya mwisho kupanda mwaka huu.










