BAADA YA KUACHA KULA UNGA: Asimulia yaliyojificha katika maisha yake

03Mar 2016
Fatma Amir
Dar
Nipashe
BAADA YA KUACHA KULA UNGA: Asimulia yaliyojificha katika maisha yake

DAWA za kulevya ni tatizo. Vijana wengi wanaharibikiwa, tatizo ambalo tafsiri yake ni ya kimataifa. Ni ‘jipu’ ambalo ulitumbuaji wake ni tatizo duniani kote.

Mvano Mjamzito baada ya kuacha kutumia madawa ya kulevya.

Kilevi hicho kina tafsiri pana, mojawapo ni iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Inaanzia na bangi, mirungi na zile ambazo ni tatizo kubwa zinazozalishwa viwandani na zinapatika katika aina mbalimbali kama vile Heroine, Cocaine, Iron na Mandrax.

Sehemu kubwa ya jamii na hasa vijana wanaojihusisha na matumizi yake huwa na afya dhaifu kimwili na kiakili na kuna dhana iliyotawala kwamba mtu anayebobea katika kutumia kilevi hicho, mwisho wake kimaisha si mzuri.

Pia inalezewa kuwa, mtumiaji anapata shida, kwani wengi wanaoamua kuingia katika ulevi huo hawaachi.

Kijana Mvano Mjamzito mwenye umri wa miaka 26, mkazi wa Mwananyamala Jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa waliopitia milima na mabonde ya ulevi wa dawa za kulevya.

Mvano anasema katika maisha yake, ameshiriki na kubobea katika kutumia dawa za kulevya, hasa Cocaine na Iron kwa wastani wa muongo mmoja.

ALIANZIA WAPI?
Mvano anasimulia alivyoanza kutumia dawa ya kulevya kwa simulizi ndefu ya safari ya maisha yake, kwamba alizaliwa katika Mtaa wa Mikanjuni Jijini Tanga, akiwa mtoto wa mwisho katika familia ya watoto saba.
Anasema orodha hiyo ni ya uzao wa mama yake, lakini wapo wengine sita katika watoto waliozaliwa na baba yake kwa mama tofauti.

Kijana huyo anasimulia safari ya maisha yake kwamba baada ya kumaliza elimu ya msingi katika shule ya Mikanjuni, mwaka 2005 alihamia Jijini Dar es Salaam baada ya mzazi wake kushindwa kumuendeleza kielimu.

Anasema alipofika Dar es Salaam, alifanya kazi ya kondakta wa daladala inayosafiri kati ya Buguruni na Mwananyamala.
Mvano anasema katika kipindi hicho alikuwa anatumia sigara, bangi na pombe. Hakuwahi kufikiri angetumia dawa zingine za kulevya maishani mwake.

Ilikuwaje akaingia katika kundi la watumiaji dawa za kulevya nyinginezo? Mvano anajibu akisema urafiki na watumiaji dawa hizo ndio uliomponza hata akajikuta anafafana nao kwa tabia.

Anasimulia kwa kina kuwa katika nyumba aliyokuwa akiishi, alikuwepo mtoto wa mwenye nyumba (jina tunalo) aliyemshawishi “kuvuta unga” wakiungana na marafiki zake wengine, waliokuwa wanatoka wote Tanga.
Mvano anasimulia kwamba, katika hatua ya kwanza alikuwa akimchanganyia dawa za kulevya katika sigara yake pasipo kujua.

APONZWA NA MPENZI
Anasimulia kwamba mshawishi mkuu katika kutumia dawa za kulevya alikuwa msichana mpenzi wake aliyekuwa akitumia dawa za kulevya.

Mvano anasema walikuwa wakikutana msichana huyo alikokutaja kuwa ‘kijiweni’ kunakouzwa bangi, ingawa katika sura ya pili ni kwamba hakuamini binti yule mrembo kama alikuwa mwathirika wa dawa za kulevya, kwani hata kiafya hakudhoofika.

Mvano anasema wakati huo ilikuwa bado kuanzishwa uhusiano wa kimapenzi baina yao.
Anasimulia kuwa siku moja wakiwa ‘kijiweni’ eneo la Kinondoni katika harakati za kuhitaji uhusiano wa kimapenzi, aliomba kuvuta bangi ya mwanamke huyo.

Mvano anasema tendo hilo lilimshangaza, kwani baada ya kutumia sigara hiyo iliyochanganywa na ‘unga’ aliona giza na alilala usingizi mzito hadi alipoamshwa na muuza bangi.

“Sikuwa na wasiwasi kwa kilichonitokea, kwa kuwa nilikuwa najua nini alichochanganyia katika bangi ile,” anasema Mvano na kuongeza:

“Kilichoniacha nishangae ni kuhusu aliyekuwa mpenzi wangu. Sikuwa najua kama ni mtumiaji “unga’’ zaidi ya kujua anatumia bangi na pombe.”

Mvano anasema kupitia hatua hiyo, alibaini mwanamke huyo ni mtumiaji “unga” na Mvano aliamini kuwa katika sura ya pili, mwanamke huyo angemkubali kimapenzi kwa imani angekuwa anamnunulia dawa za kulevya.

Anasema urafiki wao ulichukua sura mpya, kwa kuwa watumiaji wa dawa za kulevya zilizochanganywa na sigara. Siku za kwanza Mvano peke yake ndiye aliishia kusinzia.

Anasema siku aliyomtakia rasmi mwanamke huyo kumtaka uhusiano wa kimapenzi, alikubaliwa kwa sharti atumie dawa za kulevya katika utaratibu wa kujidunga sindano.

“Nilimekukubalia, lakini lazima uwe unajidunga ndio nitaweza kuwa na wewe. Kama utashindwa kufanya hivyo na kuishia kuvuta bangi, huku ukichanganya na unga sitoweza kuwa na wewe,” anatamka Mvano akinukuu jibu lenye sharti kutoka kwa mpenzi wake.

Mvano anasema mwanzoni kauli hiyo uilimshitusha sana, lakini baadaye aliridhia sharti iliyomfanya aingie katika maisha mapya ya kutumia dawa za kulevya kwa kujidunga sindano.

Anasema wakati huo akiwa na umri mdogo na mazoea ya kuiga katika maisha yake, aliridhia sharti katika siku ambayo hakumbuki ulikuwa mwezi gani, zaidi ya kuitaja:”ilikuwa Jumapili jioni mwaka 2006.”
Mvano anakumbuka tendo hilo lilimfanya alale usingizi mzito hadi saa 6.00 usiku katika makazi yake eneo la Mwananyamala.

Anasema wakiwa katika maisha ya mapenzi, mwanamke huyo alimtawala katika namna ya kutumia dawa za kulevya kwa staili mbalimbali, ikiwemo ile ya mwanzo ya kuchanganya na sigara.

“Sikuwa na jinsi ya kuacha utumiaji dawa hizo, kwani ilifika mahali siwezi kukaa bila ya kutumia “unga” (Cocaine). Alikuwa mwanamke ambaye anapenda tujidunge. Sikuwa najielewa tena wakati nikishalewa na “unga” huo.”
“Sikuweza tena kufanya kazi ya daladala, matokeo yake nilianza kujulikana katika “vijiwe” vyote wanakouzia “unga’ nikaanza kujiingiza katika wizi.

“Maisha ya mapenzi yalianza kubadilika kwa kuwa mwanamke huyo kabla ya kuwa naye, alikuwa anafanya biashara ya kujiuza, lakini sikuwahi kujua tangu awali.

“Nakumbuka mwaka 2008 kuna majambazi walidondosha fedha pale maeneo ya Ubungo. Mimi nilikuwa mmojawapo niliyebahatika kuokota hela zilizodondoka.

“Ilikuwa Sh. 700,000. Ilikuwa vurugu kati ya majambazi na Polisi wakati wa kujisalimisha. Majambazi hao ndio waliweza kudondosha fedha hizo,” anasimulia Mvano.

Anaongeza kuwa chanzo cha kuachana na mwanamke huyo ni kwamba alimuibia fedha Sh. 200,000 ikiwa sehemu ya pesa alizookota Ubungo.

Analikumbuka kuwa jambo lililomkera, ikiongeza katika kasoro nyingine aliyobaini kwamba mpenzi wake huyo alikuwa anafanya biashara ya kujiuza.

AKUTANA NA WASANII
Safari ya Mvano ilimuelekeza katika maisha mapya, kwani alikutana na wasanii wa muziki wa kizazi kipya na alijenga urafiki nao baada ya kutambuana wote ni watumiaji dawa za kulevya.

Anasema wasanii waliokuwa na makazi katika eneo la Kinondoni, Dar es Salaam, walijenga mazoea ya kumtuma kununua dawa za kulevya anazozitaja za aina ya Cocaine na Iron na walitumia pamoja.

Mvano anasema wakati huo alikuwa na kipato duni, hivyo aliwategemea wasanii kumnunulia dawa hizo.
Anasimulia kuwa mwaka 2010 ulikuwa wa majuto kwake na hawezi kuusahau, kwani ndio alitiwa mbaroni na Polisi akiwa na dawa za kulevya aina ya Iron.

Mvano anasema sakata hilo lilimfikisha hadi katika gereza la Segerea jijini Dar es Salaam alikokaa rumande kwa miezi tisa.

Kijana huyo anasema, baada ya kutoka gerezani hakuacha kutumia dawa za kulevya, lakini kiuchumi aliingia katika maisha mapya ya kuokota chupa za plastiki na kuziuza.

ALIVYOACHA ‘UNGA’
Mvano anasema siku moja akiwa harakati zake za kuokota makopo ya plastiki eneo la Kigamboni, Dar es Salaam alipita katika saluni moja ya nywele ya kike na mmoja wa wateja alimuuliza “wewe ni Teja?” akakubali.

Alimhoji kama anahitaji kuacha dawa za kulevya na alipokubali, mteja huyo wa saluni alimuachia namba ya simu na ndipo ukaanza mchakato wa kumpeleka katika kituo maalum cha kumbadilisha.

Mvano anasema aliifikisha wazo hilo kwa dada yake ambaye ni mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam, (hakumtaja jina) na watu hao wawili walishirikiana kupitia kituo husika na hatimaye wakafanikiwa Mvano kuacha dawa za kulevya.

Mvano anasema katika kipindi chote cha miezi sita, alikuwa akiishi kituoni hapo na wenzake na sasa ana miezi miwili tangu atoke huko akiwa si mtumiaji wa dawa za kulevya.

DAKTARI BINGWA ANENA
Nipashe lilifanya mazungumzo na bingwa wa tiba ya akili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Cassian Nyandindi, anayesema kuwa watumiaji wa dawa za kulevya nchini hivi sasa wanaongezeka maradufu idadi ikifikia 500,000.

Pia anasema asilimia kubwa ya watumiaji wa dawa hizo ni wagonjwa wa maradhi mbalimbali, ikiwemo Ukimwi
“Kati ya watumiaji watano wa dawa za kulevya, mmoja ni mwanamke na yeye ndiyo anayeongoza katika kuambukiza maradhi ya Ukimwi,” anasema Dk. Nyandindi.

Anaainisha umri wa watumiaji wakubwa wa dawa hizo kuwa ni kati ya miaka 12 na 59, ingawaje vinara ni wenye umri kati ya miaka 20 na 38.

Dk.Nyandidi anataja mambo yanayochangia utumiaji dawa za kulevya ni pamoja na familia zinazohusishwa na kuenea kwake.

“Familia nyingi haziko na pamoja na watoto wao kuhusiana na utaratibu waliojiwekea kwa kwenye nyumba zao,” anasema Dk. Nyandindi.

Anatoa sababu zingine kuwa ni ugumu wa maisha, ukosefu wa elimu, tamaa na vishawishi.

“Vijana wengi wamekuwa na tamaa ya kutaka vitu vikubwa kwa haraka, bila ya kujali watajiingiza katika matatizo yatakayohatarisha maisha yao,” anasema.

Wito wa Dk. Nyandindi ni vijana wawe makini katika maisha yao na watafute shughuli za kiuchumi ambazo zinazowafaa.