Serikali iokoe wahanga sera ya elimu ya bure

28Feb 2016
Mhariri
Dar
Nipashe Jumapili
Serikali iokoe wahanga sera ya elimu ya bure

Rais wa Tano, John Magufuli, ameishi katika nyingi ya ahadi zake za wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, na elimu bure kuanzia shule ya awali mpaka kidato cha nne ni mojawapo.

Chini ya sera ya elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, serikali imefuta michango yote ya lazima kwa wazazi wa wanafunzi na matokeo yake idadi ya watoto walioanza shule mwaka huu imeweka rekodi.

Ni kiasi gani sera ya elimu bure imekuwa mkombozi kwa watanzania wengi wa hali ya chini kunawakilishwa kirahisi na uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Majimatitu, Mbagala, jijini Dar es salaam ambako walikuwa wamepokea zaidi ya watoto 1,066 mpaka kufikia katikati ya mwezi huu. Ikumbukukwe kuwa uandikishaji watoto kwa ajili ya elimu ya awali na darasa la kwanza utafika kilele mwezi unaoanza kesho.

Idadi hiyo ya watoto katika Shule ya Msingi Majimatitu, tunaona Nipashe, ni rekodi si tu nchini bali barani Afrika na duniani kwa ujumla kwa sababu wastani wa waanfunzi katika shule nyingi nchini ni watoto 450.

Hivyo kuandikisha idadi ya watoto wanaoweza kutosha shule tatu kwa mpigo, ni jambo la aina yake ambalo linahalalisha ujio wa sera ya elimu bure.

Aidha, haya ni matokeo ya kujivunia ya muda mfupi, Nipashe tunaona, hasa ukizingatia kuwa katika miezi miwili ya kwanza ya elimu bure hiyo serikali imetuma fedha za matumizi ya shule zote nchini, licha ya changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika mapato na matumizi ya fedha hizo.

Tunafahamu, Nipashe, bado kuna nafasi ya kuboresha kiwango cha fedha kinachotumwa kwenye shule kwa nia ya kuondoa kero ndogo ndogo zilizojitokeza, ikiwemo baadhi ya walimu wakuu kupewa fedha kiduchu.

Na tunafahamu pia, Nipashe, kwamba serikali haijapiga marufuku wazazi kujitoa kifedha kukabili changamoto ndogondogo zilizo mashuleni ambazo zinaathiri upatikanaji wa elimu hiyo moja kwa moja.

Lakini tungependa kuishauri serikali mapema, Nipashe, kuangalia upande wa pili wa sera ya elimu bure - athari kwa wadau wa elimu hiyo, wakiwemo walinzi wa shule.

Katika toleo letu leo, Nipashe, tuna habari ya mlinzi wa Shule ya Msingi Lyowa, Mtwara ambaye amelazimika kuomba chakula katika kila nyumba anayotoka mwanafunzi wa shule hiyo, kutokana na kukosa mshahara kwa miezi mitatu mfululizo.

Mlinzi huyo ambaye shule iliingia naye mkataba kwa ajili ya kuangalia usalama, ameingia kwenye hali hiyo mara baada ya serikali kuja na mpango wa kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari.

Ili kukabiliana na adha hiyo, mlinzi huyo ameelezwa kuwa hupita nyumba hadi nyumba kuomba kujumuika katika chakula cha wazazi wa mwanafunzi.

Mlinzi huyu, tunaamini Nipashe, ni punje tu katika 'gunia' la matatizo yanayowakabili wadau wa elimu ambao maisha yao kwa namna moja yalitegemea sana michango ya wazazi na walezi.
Wanasaidiwaje?