Oktoba 2014, Kamati ya Nidhamu ya TFF ilimfungia miaka saba kujihusisha na masuala ya soka mwanasheria huyo aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Klabu ya Simba.
Beki wa kati Juma Said, maarufu Nyosso' anakamata nafasi ya pili kwa kupewa adhabu kubwa na TFF ya Malinzi baada ya msimu huu kamati ya uendeshaji wa ligi ya shirikisho hilo kumpiga faini ya shilingi milioni mbili na kumfungia miaka miwili kucheza soka nahodha huyo wa Klabu ya Mbeya City kutokana na udhalilisha wa kupenyeza kidole katikati ya makalio ya mmoja wa nyota wa Azam FC wakiwa uwanjani.
Tukiwa wadau namba moja wa michezo nchini, Nipashe hatuungi mkono udhalilisha wa aina yoyote katika michezo ukiwamo uliofanywa na nahodha huyo wa City. Tunaamini adhabu aliyopewa ni funzo kwa wachezaji wengine wenye nia ya kutenda kadhia hiyo.
Hata hivyo, Nipashe hatuko tayari kupigia upatu kitendo cha TFF na kamati zake kumwadhibu Nyosso, kisha kuwaweka kiporo baadhi ya wachezaji wa klabu za soka zinazotajwa kuwa kubwa nchini.
Tunafahamu kwamba uongozi wa Klabu ya Simba umeshawasilisha malalamiko na ushahidi wa video na kuliomba shirikisho kuchukua hatua dhidi ya utovu wa nidhamu uliofanywa na baadhi ya nyota wa Yanga wakati wa mechi ya duru la kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Nipashe tunafahamu pia kuwa uongozi wa Klabu ya Mbeya City umewasilisha malalamiko na ushahidi wa video ya mechi yao ya ligi ya Bara msimu huu dhidi ya Simba ukiliomba shirikisho kuchukua hatua stahiki dhidi ya beki wa kati Juuko Murshid aliyempiga kiwiko bila mpira nyota wao kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Tunakumbusha pia Sekretarieti ya TFF ilimfungilia mashtaka kwenye Kamati ya Nidhamu mshambuliaji Amissi Tambwe wa Yanga baada ya kupatikana na hatia ya kumvuta sehemu nyeti Murshid wakati wa mechi ya timu zao kwenye Uwanja wa Taifa Machi 8, lakini mpaka sasa bado hatua hazijachukuliwa.
Nipashe tunasikitika zimebaki raundi 10 kabla ya kumalizika kwa msimu wa 2015/16 wa Ligi Kuu Tanzania Bara ilhali shirikisho linasita kuwaadhibu baadhi ya nyota wa baadhi ya klabu waliofanya makosa msimu uliopita, licha ya kutolewa kwa ushahidi wa vitendo vyao viovu wakiwa uwanjani.
Pia kutochukuliwa hatua kwa wachezaji waliofanya makosa mbalimbali viwanjani ni kinyume cha Kanuni za Ligi za TFF toleo la 2015 zinazoitaka kamati ya uendeshaji wa ligi kuyafanyia kazi malalamiko yanayofika mbele yake ndani ya saa 72.
Tunaamini mwenendo huu wa shirikisho kutofuata misingi ya kanuni na utawala wa sheria ni hatari kwa soka la Tanzania kwani mbali ya kuwa miongoni mwa mbinu chafu zinazotumika kupanga matokeo, pia unashusha hadhi ya mamlaka husika (TFF) na kuzuia ufadhili na udhamini wa soka nchini.
Kutokana na ukweli huo, tunatoa rai kwa watendaji wote wa shirikisho kujikita katika misingi ya kiuweledi kuhakikisha si tu kwamba haki inatendeka, bali ionekane inatendeka kwa timu zote ili kulinda udhamini uliopo na kuvutia wadhamini wengine.
Nipashe tunawashauri watendaji wa TFF kuweka kando mapenzi yao kwa baadhi ya klabu ili wasimamie bila upendeleo kanuni za ligi za shirikisho kwa kuwa tunaamini pasi na kufanya hivyo, soka la Tanzania halitapiga hatua.










