Katika ngazi ya urais mwanamke mmoja alijitokeza kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku katika nafasi za ubunge na udiwani idadi ya wanawake na wenye ulemavu ikiwa ndogo.
Kwa waliojitokeza kuomba kuchaguliwa katika nafasi hizo walikutana na changamoto nyingi zikiwamo za kutokuwa na fedha za kuwafikia wapigakura na wengine wakikataliwa kwa sababu ni wanawake na walemavu.
Chama cha waandishi wa habari wanawake (Tamwa) kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Internews Tanzania, wamewakutanisha wadau wa habari na wagombea wa makundi hayo kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Singida, kujadili changamoto zilizojitokeza wakati wa uchaguzi huo.
Stella Jailos ambaye ni mlemavu aligombea nafasi ya viti maalum mkoa wa Dodoma kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), anasema changamoto kubwa aliyokutana nayo ni kutokuwa na fedha za kuwapa wapigakura, kuwatembelea na kutopewa kipaumbele.
“Ukigombea viti maalum unatakiwa kuzunguka mkoa mzima kuomba kura kwa wapiga kura wanawake, kila unakofika unaulizwa kuhusu nauli., lakini pia maeneo ya kwenda kijinadi kwenye ukumbi wa pamoja wa kupiga kura unawekwa nafasi za mwisho na unapewa dakita tano za kujieleza hali ya ulemavu jina likitajwa hadi ufike mbele umemaliza dakika tatu,” anasema.
Anasema kabla mgombea mwenye ulemavu hajamaliza kujieleza unaambiwa imetosha imetosha hatua ambayo anasema ni ishara kuwa hawataki kukusikiliza.
Anasema changamoto nyingine ni namna ya mtu kukuhakikishia kura wakati wa kuhesabu na kulazimika kuiamini meza jambo ambalo ni gumu sana na ambayo inaonyesha kuwa wenye ulemavu hawawezi kupata nafasi za uongozi.
Ndonge Said Ndonge, aligombea ubunge katika jimbo la Mbagala kwa chama cha AFP, anasema changamoto zilikuwa nyingi kama za vitambulisho vya wasioona kufanana na watu wengine na maeneo ya kupiga kura kutokuwa na miundombinu rafiki kwao.
“Unyanyapaa ulikuwa hadi ndani ya vyama kwani licha ya wenye ulemavu kuwa na sifa za kugombea hawakupewa nafasi inavyotakiwa, huku kukiwa hakuna maandishi maalum kwa wasioona kama nukta nundu na kukosekana wakalimani,” anasema.
Rehema Madusa aligombea viti maalum mkoa wa Singida na anasema, changamoto kubwa aliyokutana nayo ni ukosefu wa fedha.
“Wapiga kura wa mkoa wanajulikana mwenye fedha wanawafikia wote na kuwapa chochote ikiwamo vitenge, unapokwenda usiye na fedha hawakusikilizi na wakati mwingine wanakwambia uongee haraka uondoke kwa kuwa umesema huna fedha za kuwapa,” anabainisha.
Anasema kwa ujumla amejifunza kuwa ili uweze kufanikiwa katika nafasi ya kisiasa lazima uwe na uwezo wa kifedha na sifa nyingine zitafuata kwa kuwa wapigakura wengi wanapenda kupewa chochote ndipo wafanye maamuzi.
Lois Kibona aligombea ubunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chadema katika jimbo la Segerea jijini Dar es Salaam amegombea mara ya nne nafasi hiyo, lakini hajafanikiwa kupita.
Anasema katika uchaguzi wa jimbo walikuwa wagombe 12 kati ya hao wanawake walikuwa wawili na katika hatua ya awali alishinda.
“Rafiki wa mwanamke ni mwanamke lakini adui wa mwanamke ni mwanamke, katika chaguzi zote nimeona wanawake ndiyo wanashiriki kukuangusha,” anasema.
Zaina Manyanga ambaye aligombea udiwani katika kata ya Kimanga, jijini Dar es Salaam, anasema lugha za kashfa kwa wanawake ni kikwazo kikubwa.
Anasema mwanamke unaposimama jukwaani utafanywa kama jalala, utapewa majina yote na kashifa ambazo huzijui na hujawahi kuhusika nazo.
Aliyekuwa mgombea jimbo la Kilombero, Pamela Vigelo kupitia chama cha Chausta anasema changamoto kubwa ni kukosa fedha za kununua vifaa muhimu kama maturubai, viti na gari la kubeba muziki.
Neema Kabali ambaye ni Mkurugenzi wa Umoja wa Walimu Wanawake Tanzania, anasema mwanamke anaposimama kwenye jukwaa la kisiasa anapaswa kujiandaa kisaikolojia.
Anasema lazima ajue atakutana na lugha za matusi na maswali yenye lengo la kumdhalilisha hivyo anapaswa kujiandaa kukabiliana navyo na kuangalia lengo alilojiwekea.
Aidha, wagombea hao kwa pamoja walipongeza vyombo vya habari kwa namna vilivyoripoti uchaguzi huo ikiwamo kuwapa nafasi wanawake na walemavu na changamoto kubwa ilikuwa ni wagombea wa vyama viwili kupewa kipaumbele zaidi ya wagombea wengine.
Mkugenzi wa Internews Tanzania, Valeria Msoka, anasema wanawake wanapaswa kusimama imara na kuonyesha uwezo wao wa kuongoza katika nafasi yoyote na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.
Anasema vyombo vya habari vinapaswa kutoa nafasi sawa kwa wagombea wote na kuhakikisha habari za watu wenye ulemavu na wanawake zinapewa nafasi kwa kuwa wana mengi waliyoyafanya kwenye jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Edda Sanga, anasema utafiti uliofanywa na chama hicho umeonyesha vyanzo vya habari 2,577 vilivyotumika wakati wa uchaguzi mkuu mwaka jana, wanaume walikuwa 2,256 sawa na asilimia 88.
Utafiti huo uliolenga kuonyesha jinsi vyombo vya habari vilivyominya sauti za wanawake wakati wa uchaguzi, ilionyesha wanawake walikuwa 303 sawa na asilimia 11, huku vyanzo ambavyo havikujulikana kuwa ni mwanaume au mwanamke vilikuwa 18 ambavyo ni sawa ni asilimia moja.
Sanga anasema takwimu zinaonyesha kwamba wagombea katika ngazi ya ubunge walikuwa 1,218 kati ya hao wanawake walikuwa 233 sawa na asilimia 19.13 katika ngazi ya kata, kulikuwa na wagombea 10,879 kati yao wanawake walikuwa 679 sawa na asilimia 6,232.
MWISHO










