Vyombo vya habari vinapoangukiwa uchaguzi Zanzibar

24Feb 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Vyombo vya habari vinapoangukiwa uchaguzi Zanzibar

ZIKIWA zimebaki siku 25 kabla ya Wazanzibari kupiga kura katika uchaguzi wa marudio baada ya uchaguzi wa awali kufutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), mwaka jana.

Mkurugenzi wa Shirika la InterNews nchini Tanzania, Valarie Msoka.

ZEC imepiga marufuku kampeni za aina yoyote katika marudio ya uchaguzi huo, huku vyombo vya habari na waandishi wa habari pamoja na wananchi wanaotumia mitandao ya kijamii wametakiwa kuhamasisha amani ili uchaguzi huo usiwe chanzo cha kuleta machafuko.

Vyombo hivyo vya habari vikiwamo radio, magazeri, runinga pamoja na mitandao ya kijamii vimetakiwa kujikita katika kuandika taarifa zenye kuhamasisha na kuleta amani.

Wadau mbalimbali wanasema kuwa uchaguzi wa marudio unakazi kubwa katika kuhamasisha amani kuliko uchaguzi uliopita ambao Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha aliufuta kwa madai kwamba ulikuwa na kasoro mbalimbali.

Vyombo hivyo, vinaaswa kutoigawa jamii na kuwakumbusha waandishi wa habari kwa kutumia kalamu zao hasa wakati huu wa joto la wanasiasa na wanachama limepanda juu kuhusu hatima ya uchaguzi huo wa marudio.

Kwa kuliona hilo Shirika la Internews lenye makao makuu yake nchini Nairobi limetoa mafunzo kwa waandishi ili kuwajengea uwezo wa kuripoti habari za uchaguzi.

Akitoa mafunzo kwa wanahabari kutoka vyombo mbalimbali Mwanahabari mkongwe visiwani hapa, Salim Said Salim, aliwakumbusha wanahabari kutanguliza maslahi ya nchi kwanza kwa kuzitumia vyema kalamu zao.

Anasema wakati wa uchaguzi mara nyingi huwa kunajitokeza mambo mbalimbali hivyo, vyombo hivyo pamoja na wanahabari kuwa makini katika kutoa taarifa zao.

“Mnapokwenda kinyume na maadili ya taaluma yenu na kuegemea upande mmoja wa chama fulani mtakuwa hamuitendei haki jamii na mnaweza kuitia nchi katika matatizo makubwa,'' anasema Salim.

Salum alitolea mfano wa nchi ambazo zimeeingia katika machafuko ya kisiasa ambayo yalichangiwa kwa karibu sana na vyombo vya habari kuwa ni nchi jirani ya Kenya na Rwanda.

“Kama si vyombo vya habari Rwanda isingeingia katika mauaji ya halaiki, lakini vyombo vya habari vilichangia sana mauaji yale ya mwaka 1994,” anasema.

Anasema sasa nchi ya Rwanda inaendelea kuwa funzo kwa nchi jirani, katika Bara la Afrika na hata dunia nzima kutokana na kutokea mauaji makubwa ya watu wasio na hatia.

Akielezea hali ya machafuko ya kisiasa nchini Kenya, Salim anasema nchi hiyo ilijifunza ilipoingia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2012, baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Anasema licha ya mifano hiyo iliyotokea katika nchi jirani lakini, hivi sasa Zanzibar kumeanza kutokea viashiria vya uchochezi wa uvunjifu wa amani wakati Wazanzibari wanasubiri uchaguzi wa marudio.

“Kumekuwapo na uwandikaji wa mabango katika maskani za chama mabango ambayo huwa na ujumbe wa uvunjifu wa amani na hata katika vyombo vya habari vilivyopo Zanzibar huwekwa ujumbe wa sauti za viongozi mbalimbali ambao ni wa uchochezi,”anasema.

Anasema kuwa dalili kama hizo zinaweza kuwapa hamasa wanachama wa vyama vya siasa pamoja na wananchi kufanya vitendo vichafu vya kuleta machafuko.

Anasema kwa kuwa vyombo vya habari vina nguvu katika nchi yoyote ile vinaweza kuijenga jamii katika misingi mizuri hivyo ni vyema kuhakikisha Zanzibar inakuwa salama kipindi chote.

“Umma unaamini sana vyombo vya habari kama wanavyoaminiwa viongozi wa dini basi kwa kutumia kalamu zenu ipo haja ya uaminifu huu kuendelea na siyo kupoteza,”anasema.

Mkurugenzi wa Shirika la InterNews nchini Tanzania, Valarie Msoka anasema kwa makusudi wameamua kutoa mafunzo hayo ili kuhakikisha vyombo vya habari vinafanya vizuri katika kuripoti taarifa za uchaguzi wa marudio bila ya kupotosha jamii.

“Tumeona bado upo umuhimu wa kuvikumbusha vyombo vya habari na waandishi wa habari kutimiza wajibu wao, kwa kuwa hivi sasa wanachama na viongozi wa vyama vya siasa wana joto kubwa la kisiasa, kwani wapo wanaosema watashiriki uchaguzi, wako wanaosema kuwa hawatoshiriki haya ni mambo ya kuyaangalia zaidi tusipokuwa makini basi tutaifikisha nchi pahala pabaya,” anasema Valerine.

Kwa upande wake mkufunzi wa mambo ya habari kutoka nchini Kenya, Tole Nyatta, anasema bado vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuhubiri amani hasa katika kipindi hiki ambacho Wazanzibari wanasubiri uchaguzi wa marudio.

Akitolea mfano wa nchini kwao, Nyatta anasema ni wanahabari ndiyo waliofikisha nchi hiyo kuingia katika mapigano ya kikabila ya mwaka 2007.

“Kwa kweli hivi sasa nchini Kenya hakuna mwanahabari anayetaka kusikia juu ya kutoa taarifa za uchochezi tumekuwa ni kitu kimoja, kwa sababu wako wanahabari wamefikishwa ICC, tunajifunza kwa hilo,'' anasema.

Aidha, anasema Kenya ilifika pahala pabaya sana kwa kuwa wako waliopoteza ndugu, jamaa na wapendwa wao na wapo waliohama nchi yao, walipoteza mali zao jambo ambalo ni baya sana asingependa litokee tena.

Anasema ni wazi kuwa joto la kisiasa limepaa Zanzibar, hivyo ni lazima vyombo vya habari vitulize munkari huo na visiegemee upande mmoja.

Kwa upande wake mkufunzi wa mambo ya sheria katika Chuo Kikuu cha Tunguu Zanzibar, Ali Uki, anasema Katiba ya Zanzibar na ya Tanzania zimekuwa zikieleza utaratibu wa uchaguzi kwa wananchi na wagombea wa vyama vya siasa.

Uki anasema kuwachagua viongozi ni haki ya kila mtu ambaye atatimiza masharti ya kuchagua na kuchaguliwa na vyombo vya habari vina wajibu wa kuwaelimisha wananchi juu ya haki yao ya kuchagua na kuchaguliwa.

Muhadhiri huyo anavitahadharisha vyombo vya habari kuwa havina haki ya kutangaza matokeo katika uchaguzi na kwamba ni tume pekee ya uchaguzi ndio yenye mamlaka ya kufanya hivyo.