Hii inaitwa Roho ya Unafiki.
Makala iliyopita ilibeba kichwa cha maneno ‘Familia ya mke imechangia ndoa yangu kuvunjika!’ Kwa wale walioisoma wataona jinsi kijana alivyokuwa anasononeka namna ambavyo familia ya mkewe ilivyokuwa inashabikia mgogoro wa ndoa yake.
Ilianza pale mume aliposafiri kikazi miezi sita mkoani Kilimanjaro na aliporudi, muda mfupi tu vurugu zikaanza. Mke akatibuka na kuondoka kwao. Akamwachia mume watoto wawili.
Hata aliporudi kwa kubembelezwa na mume hakutulia hadi kufikishana ofisi ya mtendaji ambako ndugu za mke walijazana, hata kusababisha kikao kuvunjika.
Kijana huyu kuona purukshani zinazidi akaoa mwanamke mwingine awalee wanawe. Mkewe naye akaolewa mara mbili lakini akaachika.
Mpenzi msomaji, hapa ukiangalia kwa undani, wawili hao bado wangali wanapendana, hasa mume bado anampenda mkewe huyo anayehadaiwa na ndugu/familia yake.
Inavyoonekana, familia ya mke huyo imeghubikwa na Roho ya Unafiki. Yapo maneno ambayo wamekuwa wakimwambia bibie kuhusu mumewe tangu aliposafiri kwenda Kilimanjaro kikazi.
Maneno hayo ndiyo yamekuwa yakimhangaisha bibie, hata kuchukua maamuzi ya kuondoka mara kwa mara kwa mumewe.
Mpenzi msomaji, Unafiki ni roho isiyoonekana. Roho ni kitu kisichoonekana kwa macho lakini inamtawala mwanadamu. Wapo watu wanaodhani kuwa roho hii ya unafiki haina madhara, lakini ukweli ni kwamba siyo tu ina madhara kwa aliye nayo bali pia kwa watu waliyo karibu naye.
Mwenye roho hii huja kama rafiki ukadhani ni kweli kumbe anakutega. Unamwamini, unakula naye, unampeleka nyumbani kwako hadi chumbani, kumbe ni adui mkubwa!
Anaonyesha unyenyekevu kwa muonekano wa nje, kumbe ndani ya nafsi yake ameficha mambo mabaya sana. Anachoongea sicho kilicho rohoni mwake. Atakuletea zawadi kumbe anakutega, mwishoni anakuangamiza.
Unafiki upo mahakamani, maofisini ambako wafanyakazi wenzio wanakuchekea kumbe unafiki umeganda ndani ya nafsi zao. Baadhi wanatamani cheo chako, wanatamani ofisi yako, wanaona gere utendaji wako na kadhalika.
Watakuchekea lakini huku nyuma wanakusema kwa wakubwa zako, wanakuendea kwa waganga lakini hayo yote ni bure kwani kila mtu Mungu amempa fungu lake na hazina yake ipo pale ulipo moyo wake.
Hawa ni watu wabaya sana, wamesababisha watu wengine kufukuzwa kazi na hata wengine kufa kwa kihoro, kisa, wanafiki wachache. Inatupasa tujilinde nao kwani wako tayari kukufanyia kila kitu kumbe wanakutega. Kwa mfano, anakuchekea kwa nje kumbe anajirusha na mumeo au mkeo. Ni hatari sana roho hii ya Unafiki ambayo inatawala nafsi ya mtu.
Hata katika maandiko matakatifu, Bwana Yesu aliwatahadharisha waandishi na Mafarisayo kuhusu Unafiki. Angalia kitabu cha Mathayo 23:28 neno la Mungu linasema; Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi.
Yesu alifahamu hatari ya unafiki, akawaambia makutano; Jilindeni na chachu ya Mafarisayo ambayo ni Unafiki.
Mpenzi msomaji, huenda una marafiki wengi na ndani ulishajiachilia kwako. Ila jitahidi kujua ili usiangamie.
Pia Mungu ameshautambia kwamba maadui zetu hawako mbali, ni wale tunaokula nao na kuwashirikisha katika mambo mengi kwa karibu kabisa. Angalia Mika 7:6 imeandikwa; Adui za mtu ni watu wa nyumbani mwake mwenyewe.
Angalia pia Warumi 12:9 Neno la Mungu linasema; Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema.
Kumbuka, upo upendo wa mdomoni tu, kumbe ni mnafiki mkubwa! Mnacheka lakini baadaye anakuongea vibaya, anachukua siri zako kisha baadaye anazianika kwa wengine. Hatari sana mtu wa aina hii.
Msomaji wangu, wakati namalizia hebu nikupe madhara ya unafiki. Zaburi 12: 2-3 Neno linasema; Husemezana yasiyofaa kila mtu na mwenzie, Wenye midomo hujipendekeza, Husemezana kwa mioyo ya unafiki; BWANA ataikata midomo yote ya kujipendekeza, Nao ulimi unenao maneno ya kiburi.
Ndio maana katika kisa cha jamaa hapo juu, japo anampenda sana mkewe, lakini unafiki wa familia ya mke umesababisha ndoa kuvunjika. Sasa hakuna aliyefaidika, bibie anaolewa na kuachwa huku nduguze wanafiki wakichekelea.
Pengine ni wivu hawakutaka mwenzao atulizane kwa mume. Kisa ni roho ya unafiki iliyokuwa imesimama mbele ya ndoa hiyo. Ama kweli Maisha Ndivyo Yalivyo.
Msomaji wangu, je, unacho kituko cha kimaisha ungependa tujadili pamoja? Usikawie, ukiwa tayari kuwa huru
kuwasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com au flora.wingia@guardian.co.tz

.jpg?itok=nfwjwDzv)









