Nini hutokea mwilini wakati wa mzunguko wa hedhi?
Mzunguko wa hedhi huendeshwa na homoni mbalimbali za mwili. Wakati wa mzunguko wa hedhi, sehemu za kwenye ubongo ziitwazo ‘hypothalamus’ na ‘pituitary gland’ hupeleka taarifa za homoni kwenda kwenye ovari na kurudi kwenye ubongo. Taarifa hizi huziweka ovari na mfuko wa uzazi tayari kwa ajili ya kubeba mimba.
Kwanza pituitary gland hutoa homoni iitwayo Follicle Stimulating Hormone-FSH ambayo huenda kusababisha kukomaa kwa yai ndani ya ovari. Baada ya hapo homoni ya estrogen hutolewa ambayo huenda kusaidia ujenzi wa ukuta wa mfuko wa uzazi kwa ajili ya maandalizi ya mimba inayoweza kutokea (kwenye ukuta huu ndipo mimba hujishika, kupata virutubisho na kukua).
Wakati kiwango cha estrogen kimepanda mwilini, hali hii husababisha utolewaji wa homoni nyingine iitwayo Gonadotropin-Releasing Hormaone-GnRH kutoka kwenye sehemu ya ubongo. Uwepo wa homoni ya GnRH husababisha pituitary gland kusababisha ongezeko la homoni ya lutenizing (LH). Baadaye LH husababisha uachiliwaji wa yai kutoka kwenye ovari, kitendo kinachojulikana kitaalamu kama ‘ovulation’.
Baada ya yai kutolewa kutoka kwenye ovari, husogezwa karibu na mfuko wa uzazi ‘uterus’ kusubiri kuungana na mbegu za mwanamme, na endapo litakutana nazo basi mimba hutungwa. Kama hakutatokea muunganiko kati ya yai na mbegu (kitaalamu huitwa ‘fertilization’) basi yai humeguka na kufa ndani ya masaa 6 hadi 24.
Dalili za yai kutoka/kuachiliwa
Muda mfupi kabla ya yai kuachiliwa kutoka kwenye ovari mwanamke hutokwa na ute katika mlango wa uzazi ambao huwa katika hali ya kuteleza na usio na rangi; ni kama sehemu ya nje ya yai bichi (isiyokuwa kiini). Ute huu huvutika sana pia. Mwanamke anapokuwa katika hali hii huweza kupata ujauzito iwapo atagusana na mbegu za kiume. Ute huu husaidia kurutubisha mbegu za kiume pindi zinaposafiri kupita mlango wa uzazi ‘cervix’.
Iwapo mwanamke hayupo katika kipindi hiki cha yai kuachiliwa, ute wa kwenye mlango wa uzazi ‘cervical mucus’ huwa na rangi tofauti na katika hali ya tofauti. Ute huu huweza kuwa unanata, mweupe kama maziwa, ukiwa na muonekano kama losheni ya kujipaka au kuwa na rangi ya njano. Ute huu huwa hauvutiki na huwa na harufu kali kidogo.
Aidha, nafasi ya mlango wa uzazi nayo hubadilika wakati wote wa mzunguko wa hedhi. Wakati wa yai kuachiliwa kutoka kwenye ovari, mlango wa uzazi husogea juu kidogo na njia hutanuka kidogo zaidi. Baadhi ya wanawake huhisi hali ya maumivu wakati wa yai kuachiliwa. Maumivu haya hutofautiana na huweza kuwa ya kuvuta au ya jumla katika sehemu ya tumbo, au maumivu ya kukata upande mmoja wa tumbo ambao ndio yai huachiliwa.
Ni siku gani yai huachiliwa (ovulation)?
Mara nyingi wanawake huamini kuwa yai huachiliwa katikati ya mzunguko wa hedhi. Ukweli ni kwamba yai huachiliwa siku 12 hadi 16 kabla ya mzunguko unaofuata kuanza. Kwahiyo, japokuwa kwa mwanamke mwenye mzunguko wa siku 28 yai lake laweza kuachiliwa katikati ya hedhi (kati ya siku ya 12 na 16), mwanamke mwenye mzunguko wa hedhi wenye siku 36 yai lake huachiliwa kati ya siku 20 na 24. Kwa wanawake wenye mizinguko isiyobadilika sana, njia nzuri ya kukadiria siku ya yai kuachiliwa ni kutoa 16 kutoka kwenye jumla ya siku za mzunguko wake wote na baada ya kupata jibu, ajumlishe jawabu hilo na 4. Hii itampa siku ambayo yai huweza kuachiliwa. Kwa mfano, mwanamke mwenye mzunguko wenye siku 22 mara nyingi yai lake huachiliwa kati ya siku ya 6 hadi 10 ya mzunguko wake (22-16=6, halafu 6+4=10).
Mabadiliko ya siku kwa siku
Siku 1–5: Wakati wa hedhi
Dalili mbaya za hedhi huwa zimeshakwisha. Kiwango cha homoni za estrogen na progesterone huwa kimeshuka. Mwanamke husikia hali ya misuli kukaza. Hii husababishwa na kemikali ziitwazo ‘prostaglandins’ ambayo mwili huzitoa kusaidia ukazaji wa misuli ili ukuta wa mfuko wa uzazi umeguke. Kwa baadhi ya wanawake, kemikali hii husababisha kusikia kichefuchefu, kuhara au kutapika.
Siku ya 6–13: Hali nzuri
Kiwango cha homoni ya estrogen huanza kupanda tena wakati ambapo mayai huanza kukomaa. Hali hii hupelekea ongezeko la kemikali nyingine za ubongo kama serotonin na dopamine ambazo humfanya mwanamke kujisikia vizuri sana na huongeza kiasi cha damu kinachopita kwenye ubongo. Mwanamke hua vizuri sana kiakili na kimwili kwa ujumla.
Siku ya 14-15: Hali ya hatari
Hamu ya kujamiiana huwa kubwa wakati huu siku chache kabla ya yai kuachiwa. Wakati huu mwanamke hupata ujauzito endapo atajamiiana na mwanamme. Baadhi ya wanawake huweza kuhisi wakati yai linapoachiliwa kutoka kwenye ovari.
Siku ya 16–28: Maandalizi ya dalili za hedhi
Wakati huu mwili hutumia kiasi kikubwa cha nguvu zake na kuhisi njaa mara kwa mara. Huwa ni hali ya kawaida. Kuongezeka kwa homoni ya progesterone huweza kusababisha ngozi kuzalisha mafuta kwa wingi hali ambayo husababisha kutokwa chunusi. Mwanamke anapokaribia hedhi, kiwango cha homoni za progesterone na estrogen hushuka na kusababisha mabadiliko ya ukimwa ‘mood’ na kupungua kwa hali ya kutulia ‘concentration’.
Wiki ijayo tutajadili jinsi ya kufahamu siku za hatari katika mzuguko wa hedhi.
No: 0784 865 616


.jpg?itok=nfwjwDzv)








