Viboko vilitumika katika shule za msingi, sekondari na baadhi ya vyuo. Waliosoma zamani walichapwa viboko na wengi hadi sasa wanakiri kwamba adhabu ya viboko iliwasaidia kupata mafanikio waliyonayo.
Hata hivyo, katika miaka ya karibuni sheria ilizuia adhabu hiyo na kuweka utaratibu maalum. Kwa kujibu wa mabadiliko hayo, viboko vinaongozwa na Sheria ya Elimu Sura ya 353, ambayo inaelekeza kuwa adhabu hiyo kutolewa kwa ruhusa ya mwalimu mkuu pekee ama kuwapo kwa ruhusa yake kwa wasaidizi wake huku ikielekeza kuwa idadi ya juu ya viboko ni vinne.
Uamuzi huo ulitokana na adhabu hiyo kutumiwa vibaya na baadhi ya walimu na kuwasababishia athari baadhi ya wanafunzi, hivyo wazazi, walezi na wadau wengine wa elimu kulalamika kisha Serikali ikasikia kilio chao.
Licha ya uamuzi huo, kuna baadhi ya wadau wa elimu ambao wamekuwa wakilalamikia kasi kubwa ya mmomonyoko wa maadili miongoni mwa wanafunzi unaochangiwa na mambo mbalimbali, yakiwamo malezi mabaya na utandawazi.
Hali hiyo imekuwa ikiwafanya waone umuhimu wa kurejeshwa kwa adhabu ya viboko shuleni. Hali hiyo inaonekana pia kumgusa sana Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, ambaye amewataka walimu na bodi za shule kutekeleza adhabu ya uchapaji viboko shuleni ili kudhibiti mmomonyoko wa maadili kwa wanafunzi.
Alitoa agizo hilo juzi wakati akifungua mdahalo wa wanafunzi kutoka shule mbalimbali za sekondari na msingi za jijini Dar es Salaam, kuhusu kampeni ya kitaifa na kukuza maadili kwa lengo la kukuza na kusimamia maadili kwa vijana.
Alisema serikali ilitoa waraka wa utoaji wa adhabu kwa wanafunzi wanaotenda makosa yaliyokatazwa na makosa ya jinai ili wanapobainika wachukuliwe hatua stahiki kwa lengo la kuwarekebisha tabia na kuwaandaa kuwa viongozi wa taifa lijalo.
Aliwaelekeza walimu na wakuu wa shule wahakikishe wanafuata waraka wa mwaka 2002 kwa kutoa adhabu kwa wanafunzi wanaobainika kuvunja sheria za shule.
Kwamba Serikali imebaini kuwapo malalamiko kutoka kwa baadhi ya walimu kuwa, bodi za shule zinasita kuchukua hatua stahiki na kutetea baadhi ya wanafunzi wakorofi wanaopelekewa na kuwaacha kuendelea na masomo.
Prof. Ndalichako alisema wakati huu si wa kulea ugonjwa wa mmomonyoko wa maadili kwa wanafunzi na bodi za shule ziache siasa kwa kuwa siku hizi kila kitu ni siasa.
Tunakubaliana na Prof. Ndalichako kuhusu urejeshaji wa viboko shuleni, lakini hofu yetu bado ni usimamizi katika utekelezaji wake.
Tunasema hivyo kutokana na matukio kadhaa ambayo yamekuwa yakitokea mara kadhaa. Kwa mfano, tukio la karibuni mkoani Mbeya ambalo walimu waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo walimpiga kupita kiasi mwanafunzi mmoja na kusababisha Serikali na vyombo vya dola kuingilia kati.
Hakuna mazazi au mlezi ambaye anapinga mtoto wake asipewe adhabu ya kiboko ili kumuweka sawa kimaadili na kitaaluma, lakini wanahofia walimu wasiofuata maadili ya taaluma yao na ya kijamii kuitumia fursa hiyo vibaya na kusababisha athari kubwa kwa wanafunzi.
Ushauri wetu ni kwamba uwepo mjadala wa kina kuhusiana na suala hilo kisha ziwekwe taratibu za kisheria na kikanuni za kusimamia vizuri utekelezaji wake, ili walimu wasikiuke.










