Migogoro hiyo ambayo chanzo chake ni kugombea ardhi, imekuwa ikiwahusisha wakulima na wafugaji katika maeneo mengi nchini.
Kibaya zaidi ni kwamba imekuwa ikitokea sambamba na mapigano baina ya makundi hayo mawili na matokeo yake ni kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.
Migogoro hiyo imekuwa ikitokea karibu kila mahali nchini, lakini kuna maeneo sugu ambayo imeathirika sana kutokana na mapigano yanayotokea kila uchao.
Baadhi ya maeneo hayo ni Kilosa, Mvomero, Kiteto, Rufiji na Chunya kwa kutaja baadhi.
Kimsingi, kila kundi limekuwa likidai kuwa ndilo lenye haki ya kumiliki eneo husika. Wafugaji wanasema ni maeneo yao ya kulisha mifugo wakati wakulima wakidai kuwa ni maeneo yao ya kulima.
Kutokana na hali hiyo, wafugaji wamekuwa wakiingiza mifugo na kula mazao ya wakulima na wakulima walipiza kisasi kwa kuua mifugo. Matokeo yake kuwa ni mapigano.
Kutokana na migogoro hiyo, serikali imekuwa ikitoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanamaliza migogoro hiyo. Rais John Magufuli wakati wa kuunda serikali yake aliwagiza viongozi hao pamoja na mambo mengine kushughulikia migogoro hiyo na kuipatia ufumbuzi.
Katika hali inayodhihirisha kuwa migogoro ya wakulima na wafugaji bado ni changamoto kubwa, Jumamosi iliyopita watu wawili waliuawa katika mapigano baina ya makundi hayo wilayani
Handeni, Mkoa wa Tanga.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, David Mnyambunga, matukio hayo yalitokea katika wilaya za
Handeni na Kilindi.
Mnyambunga alisema tukio la mauaji ya watu wawili lilitokea Novemba 16 saa 11: 30 jioni katika Kitongoji cha Tengwe Kijiji cha Manga wilayani Handeni baada ya kuzuka mapigano ya wakulima na wafugaji.
Mapigano hayo yalitokana na wafugaji jamii ya Wamang’ati katika Kijiji cha Ng’andu mkoani Pwani kuingiza mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima Handeni.
Mfugaji aliyeuawa alipigwa risasi na wakati mkulima aliuawa kwa kuchomwa mkuki mbavuni.
Tukio hili na mengine yanayotokana na mapigano ya kugombea ardhi nchini hayanabudi kutafutiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu kwa kuwa yanatishia usalama wa wananchi.
Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi kuchukua hatua mbalimbali za kukomesha migogoro ya ardhi, ikiwamo kugawa ardhi iliyotelekezwa na wawekezaji wakubwa kwa wananchi wenye mahitaji ya ardhi katika maeneo kadhaa, baada ya Rais kufuta hati za umiliki.
Aidha, ilishaunda kamati iliyochunguza migogoro ya ardhi mkoani Morogoro na kupendekeza utaratibu wa kupiga chapa mifugo, ingawa zoezi hili lilisimamishwa kutokana na malalamiko kutoka kwa wananchi.
Aidha, serikali kupitia kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ilichukua hatua ya kusimamia ujenzi wa mtaro wa kutenganisha maeneo ya wakulima na wafugaji wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro, lengo likiwa ni kudhibiti mapigano.
Tunaridhishwa na jitihada za serikali kuendelea kushughulikia migogoro ya ardhi, ikiwamo ya wakulima na wafugaji, lakini tunaishauri iendelee kubuni mikakati mipya na endelevu ili kuikomesha kabisa.










