Kazimoto ataka ubondia badala ya kandanda?

13Feb 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kazimoto ataka ubondia badala ya kandanda?

LICHA ya Mahakama kuwa chombo cha kisheria kinachosimamia mashitaka, na kuyatolea hukumu, pia ni moja ya mihimili mitatu ya nchi, mingine ikiwa Bunge na Serikali.

Mahakama ni kimbilio (pahali pa kupata nusura au msaada) la mtu yeyote anayedhani katukanwa, kaonewa au kadhulumiwa. Mtu anapojichukulia sheria mkononi ni mhalifu anayestahili kushitakiwa mahakamani.

Jumatano wiki hii kule Shinyanga, mchezaji Mwinyi Kazimoto wa Simba aliripotiwa kumpiga mwandishi wa gazeti la Mwananchi aitwaye Mwanahiba Richard baada ya mazoezi ya timu hiyo.

Yadaiwa kuwa Kazimoto alimpiga makofi, ngumi na mateke Mwanahiba kwenye uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga majira ya asubuhi baada ya mazoezi ya Simba. Sababu za Kazimoto kumpiga mwandishi ni kwamba eti aliambiwa na washikaji wake kuwa mwandishi alimwandika vibaya mwaka jana!

Bado Kazimoto alikuwa na kinyongo (hali ya mtu kutokuwa na moyo wa kusamehe au kusahau maudhi aliyofanyiwa; mfundo). Jambo hili huwaletea watu matatizo ya moyo hata kufupisha maisha yao.
Sijui kama Kazimoto anatambua hilo.

‘Kuandikwa vibaya,’ tena mwaka jana, ndio iwe sababu ya kumpiga mwandishi akiwa kazini kutimiza wajibu aliotumwa na gazeti lake? Kazimoto asidhani yeye ni tofauti na watu wengine nchini.

Kama viongozi wakubwa huandikwa na kukoaolewa wanapokengeuka, sembuse Kazimoto? Yeye ni nani hata asikosolewe anapokosa?

Yadaiwa pia Mwanahiba amekuwa akipigiwa simu za matusi na Kazimoto huku akimpa siku saba amwambie mtu aliyemweleza habari alizoandika dhidi yake. Mtu mmoja anakuwa mlalamikaji na hakimu sawia! Mahakama zimewekwa kufanya kazi gani?

Mwanahiba anadai kuwa wakati akishambuliwa, Kazimoto alimwambia aende kokote kwani yeye hajali huku kocha Jackson Mayanja na nahodha wake, Mussa Hassan wakisikia tambo za Kazimoto.

Kwa kuwa Mwanahiba anajua umuhimu wa Jeshi la Polisi, alikwenda kuripoti na kufunguliwa jalada namba SHY/RB/895/2016 na kupelekwa hospitali kutibiwa. Yasemekana askari walimfuata Kazimoto lakini mpaka nilipokuwa naandaa makala haya, hakukuwa na taarifa zozote kama alikamatwa au la.

Kwa kawaida wachezaji wa timu za kandanda, hasa Simba na Yanga hudhani wako juu ya sheria na kwamba wanaweza kufanya jambo lolote wakitegemea kutetewa na vilabu vyao.

Tumeona mara nyingi wachezaji wakianzisha vurumai viwanjani kwa kuwapiga waamuzi na kuvunja vitendea kazi vyao kama meza na mabango ya kuonesha mabadiliko ya wachezaji na muda wa nyongeza.

Nakumbuka shabiki wa Coastal Union aliyevunja vifaa vya wasimamizi wa mchezo lakini hakuna karipio lolote lililotolewa na chama cha kandanda cha wilaya au mkoa. Hata TFF haikutoa tamko kukemea jambo lile.

Husemwa mwana umleavyo ndivyo akuavyo. Hali hii ya wachezaji kujichukulia sheria mkononi haikuanza juzi wala jana. Imekuwapo kwa muda mrefu na kadhia hii imekuwa ikiangaliwa kwa macho tu bila wahusika kuchukuliwa hatua stahili.

Lazima wachezaji watambue na kuheshimu kazi za watu wengine. Waandishi wa habari za michezo wanapokwenda viwanjani huwa kazini kama wanavyokuwa wachezaji wanapokuwa mchezoni. Kazi ya waandishi ni kuandika matukio yote ya uwanjani.

Kama kuna mchezaji aliyecheza vizuri watamsifu na aliyeboronga wataeleza wazi alivyoboronga ili ajirekebishe au atafute sababu zilizomfanya kucheza chini ya kiwango chake.

Kazimoto angejiuliza ni kwa nini hana hakika ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha Simba mara kwa mara.

Tena basi yeye si mchezaji pekee asiyepangwa kuanza kwenye kikosi cha kwanza kwani wapo wengi kama yeye. Kwa nini aone nongwa kutopangwa?

Hilo peke yake lingetosha kumfanya ajiulize na kuongeza bidii mazoezini ili kumridhisha kocha ampange. Kwa hiyo anapoandikwa kuwa uwezo wake umepungua iwe changamoto kwake ya kujibidisha zaidi ili kurejesha kiwango chake.

Kama Mussa Hassan ‘Mgosi’ ambaye ni nahodha wa timu yake huwekwa benchi sembuse yeye? Kwani kumshambulia mwandishi ndio kocha wake atampanga hata kama anaona hafai kumwanzisha mchezoni?

Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited (MCL) Bakari Machumu ameeleza wazi kuwa endapo Kazimoto aliona kaandikwa vibaya, angepeleka malalamiko yake kwa uongozi wa gazeti husika na kutaka aombwe radhi.

Labda kama Kazimoto asingeridhika na uamuzi wa MCL, basi angeenda mahakamani kudai ‘haki’ kwa ‘kuchafuliwa jina lake.’ Badala yake alijitwalia sheria mkononi na hiyo yaonesha hulka (mwenendo au tabia ya mtu inayojionesha katika matendo) yake.

Wakati tukiliachia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi kuhusu tukio hilo la kufedhehesha, ni wajibu wa TFF kuchukua hatua sahihi kuwaadhibu wachezaji wanaopiga waandishi wanapokuwa wakifanya kazi zao. Ukimya unawapa vichwa wachezaji wa aina ya Kazimoto.

Wakati hayo yakiendelea, si chama cha kandanda mkoani Shinyanga wala Shirikisho la Kandanda Nchini (TFF) lililotoa tamko kukemea kitendo hicho. Ukimya huu wa nini wakati wacheza kandanda wanageuka mabondia?
marobarnabas@yahoo.com
0715/0784 33 40 96