Benchikha akatisha kozi kuja kuwakabili Al Ahly

14Mar 2024
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Benchikha akatisha kozi kuja kuwakabili Al Ahly

KOCHA Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha, ameamua kukatisha masomo yake na kurejea nchini kuanza mikakati ya kuikabili Al Ahly kwenye mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

KOCHA Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha.

Taarifa za uhakika zilizoifikia Nipashe zinasema Benchikha aliondoka nchini kuelekea Algeria siku chache zilizopita kwa ajili ya kuhudhuria kozi ya juu ya ukocha, lakini  baada ya kutangazwa droo ya robo fainali ameamua kukatisha kozi hiyo na kurejea nchini.

Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo ameiambia Nipashe kuwa kocha huyo anatarajiwa kurejea nchini siku yoyote kuanzia leo na tayari ametoa maombi kwa uongozi kuipeleka timu hiyo Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi katika kipindi ambacho ligi itasimama kupisha mechi za kirafiki za kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulimwenguni (FIFA).

“Kocha atarejea mapema kuendelea na majukumu yake, katika michuano hii ya kimataifa Benchikha hana masihara tayari tumeshamfahamu mpinzani wetu na ameweka mikakati yake kuelekea mchezo huo.

"Moja ya mikakati yake ni kutumia kipindi cha michezo ya kimataifa kwa timu za taifa katika kalenda ya FIFA, ameomba kambi Zanzibar lakini  ametaka kuwapo kwa michezo ya kirafiki kabla ya kuwakabili Al Ahly," amesema kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Simba kwa mara nyingine itaumana na mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika katika michezo miwili ya hatua ya robo fainali kuwania kutinga nusu fainali.

Katika michezo hiyo, Simba ambayo juzi ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 3-1 kwenye ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida Fountai Gate, itaanzia nyumbani kati ya Machi 29 na 30 kabla ya kwenda kurudiana nao kati ya Aprili 5 na 6 jijini Cairo.