Samatta atemwa Stars

14Mar 2024
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Samatta atemwa Stars

​​​​​​​ALIYEKUWA Nahodha wa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), Mbwana Samatta, ameachwa katika kikosi cha wachezaji 23 kilichoitwa kwa ajili ya kujiandaa na mechi mbili za kimataifa dhidi ya Bulgaria na Mongolia, imefahamika.

Mbwana Samatta.

Nyota mwingine aliyeachwa katika kikosi hicho ni golikipa, Beno Kakolanya.

Hata hivyo, mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize na beki wa kati wa Simba, Kennedy Juma, wamerejea katika kikosi hicho.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco' amesema timu hiyo inatarajia kuingia kambini Jumapili ili kuanza maandalizi ya michezo hiyo miwili ya kirafiki.

Morocco amesema wachezaji walioitwa katika kikosi hicho ni mchanganyiko wa vijana na nyota wenye uzoefu wa kuitumikia timu hiyo.

Amesema kikosi hicho kitaondoka nchini Machi 18, mwaka huu na kuanza safari ya kuelekea Azerbaijan ambapo michezo hiyo miwili ya kirafiki inayotambuliwa na Kalenda ya FIFA itachezwa.

"Tutakuwa na mechi mbili za kirafiki, tutacheza Machi 22 na Machi 25, mwaka huu dhidi ya Bulgaria na Mongolia, baada ya hapo wachezaji watarejea nchini haraka kwa ajili ya majukumu mengine.

Tumechanganya baadhi ya wachezaji ili kuwapa nafasi vijana na sura mpya kwa lengo la kutengeneza timu imara ijayo,” amesema Morocco.

Kikosi kamili cha Stars ni  makipa; Aishi Manula (Simba), Aboutwalib Mshery (Yanga) na Kwesi Kawawa (Syrianska FC, Sweden) wakati mabeki ni pamoja na Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca wote kutoka Yanga, Lusajo Mwaikenda (Azam FC), Haji Mnoga (Aldershot Town,  England, Mohammed Hussein, Kennedy Juma (Simba) Novatus Miroshi (Shakhtar Donestsk- Ukraine na Miano Danilo wa Villena CF ya Hispania.

Viungo ni Feisal Salum 'Fei Toto', Yahya Zaydi (Azam FC), Mudathir Yahya (Yanga),Morice Michael (RFK Novi Sad, Serbia),Himid Mao (Telaea El Gaish SC, Misri) na Tarryn Allarakhia kutoka Wealdstone ya England.

Washambuliaji ni Mzize, Saimon Msuva (Alnajmah FC, Saudi Arabia), Kibu Denis (Simba), Abdul Suleiman 'Sopu' (Azam FC), Ben Starkie (Ilstone Town- England) na Charles M'mombwa anayecheza soka la kulipwa huko Australia.