NHIF kuja na mfumo wa alama za vidole kuepusha udanganyifu

07Mar 2024
Maulid Mmbaga
Dar es Salaam
Nipashe
NHIF kuja na mfumo wa alama za vidole kuepusha udanganyifu

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Benard Konga, amesema wanatarajia siku chache zijazo kuja na mfumo maalumu wa alama za vidole na kutumia neno la siri katika kuthibitisha wanachama wa mfuko huo ili kukomesha udanganyifu.

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Benard Konga.

Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam Konga amesema wamebaini kwamba kuna udanganyifu unafanywa na baadhi ya wanachama kwa kutumia kadi moja kutibu watu hadi wanne wa familia moja, na kwamba kutokana na hilo wameweka waangalizi katika kila kituo cha kutolea huduma za afya.

 

Amesema katika hilo hawatarudi nyuma na wataimarisha udhibiti ili kuhakikisha fedha za mfuko zinatumika kwa wanachama halali, akibainisha kwamba kwa yoyote atakaebainika kufanya udanyanyifu kadi yake itafunguiwa.

 

“Hatuna mjadala kwenye hilo vinginevyo kwenye asilimia nane tutatibu asilimia 15, kwenye hilo hatupepesi macho tuko wakali tunasimamia, tuko katika vituo vyote vya Dar es Salaam na mikoa mingine. Kama mtoto wako ulimkatia bima akiwa na miaka mitatu sasa ana 15 sura imebadilika usisubiri akaumwa, njoo ofisini tukubadilishie tukupe kadi mpya inayoendana na uhalisia,” amesema Konga.

 

“Tukigundua kwamba picha iliyoko kwenye kadi na ya mtoto uliekuja naye sio yenyewe hiyo kadi tutaishika na mengi yatafuta nyuma yake, lakini gharama zote ziliziko kwenye kadi familia lazima ilipe, na tunaenda mbali tunazuia familia zima ili Baba uje, tukicheza juu ya hilo huu mfuko utakuwa shamba la bibi,” amesisitiza Konga.

 

Aidha, ameeleza kuwa mtumishi yoyote atakaye bainika kwenda kinyume atachukuliwa hatua, na kwamba haiwezekani kadi moja ya Sh 50,400 ikatibu watoto wanne kwenye familia, akisisitiza kwamba suala hilo haliwezekani.

 

Hata hivyo, Konga amebainisha kwamba wamefanya tafiti 596 na kufanikiwa kuokoa takribani Sh. Milioni 200, na kuchukua hatua za kusitisha mikataba 42, kubaini wanataaluma 178 waliofanya udanganyifu ambao tayari wamewaripoti kwenye mamlaka zao.

 

“Pia tumefungua mashtaka yanayohusu wanachama 68 juu ya matumizi mabaya ya kadi, na jumla ya kadi 5,468 zimeshitishiwa huduma kutokana na kuwa na viashiria kwamba zinahusika na udanganyifu, pia kuna taarifa inasambaa kwamba watumishi 147 wamejihusisha na udanganyifu, lakini kati yao 27 ndio wa mfuko.

 

“Wamechukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma, 16 wamefukuzwa kazi, watano wamepewa onyo, wawili wameshushwa mshahara na wanne wameshushwa vyeo, lakini pia kuna waajiri binafsi pia ambao wamesitishiwa mikabama yao,” amesema Konga.