Hadi jana mchana, idadi ya waliofariki dunia walifikia wanane baada ya wengine watatu kufariki dunia wakiwa hospitalini wakipatiwa matibabu.
Baadhi ya wazazi kisiwani hapo, wakiwa na mfadhaiko, walisema juzi kuwa hawaelewi chanzo cha tatizo hilo ambalo limewakumba watoto wengye umri mdogo ambao asubuhi na mapema walianza kutapika na kutetemeka na baada ya muda mfupi, watatu kati ya hao wakafariki dunia ndipo uamuzi wa kuwapeleka hospitalini ukachukuliwa.
Malimu Juma Mati alisema hawajui chanzo cha tatizo hilo na wamepatwa na mshangao kwa kuwa waliokumbwa na ugonjwa huo na wengine kufa ni watoto wenye umri mdogo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Abdalla Hussein Mussa, aliwataja watoto waliofariki dunia kuwa ni Arshad Haji Haji (miaka miwili), Faridat Fumu Khamis (kichanga cha miezi mitatu) na Kazima Makame Haji (miaka minne) wote wakazi wa Kisiwa Panza.
Aliwataja waliolazwa kuwa ni Aviwe Khamis Khalfan (miaka miwili), Abubakar Makame (mwaka mmoja na nusu) Azikar Haji Haji (6), Suleiman Haji Hamad (12), Samira Haji Hamad (12), Fatma Suleiman Hamad (11) na Sahira Khamis Makame miaka miwili.
Wengine ni Biabu Abdalla Juma (37), Mati Vuai Mohamed (8), Fakih Vuai Mohamed (6) na Hulaiafa Ame Othman (18) wote wakazi wa Kisiwa Panza ambao wote wanaendelea na matibabu.
Kutokana na tukio hilo, Kamanda Khamis aliwataka wakazi wa Kisiwa Panza na maeneo jirani kuwa watulivu wakati huu ambao uchunguzi unafanyika ili kujua chanzo cha tukio hilo.
Kaimu Daktari Mfawidhi wa Hospitali ya Abdallah Mzee, Mohamed Faki Salehe, alisema walipokea wagonjwa 33, watano wamefariki dunia na wengine walifariki kijijini na kufanya jumla ya wanane.
“Idara ya Kinga Wilaya ya Mkoani imefunga kambi katika eneo la Kisiwa Panza ili kutoa matibabu pale pale, wamesema uchunguzi wa awali wamegundua vimelea vya bakteria vinavyosababisha matatizo, ila uchunguzi zaidi wanafanya kwenye maabara kubwa,” alisema.