TGNP,Wadau wataka ongezeko wanawake katika uongozi  

07Mar 2024
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
TGNP,Wadau wataka ongezeko wanawake katika uongozi  

Wadau wa maendeleo ya wanawake wametaka pawepo utashi wa kisiasa na dhamira ya kweli kwa viongozi wa vyama vya siasa kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi ndani na nje ya vyama hasa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, mwaka huu na uchaguzi mkuu, mwakani.
 

Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi akisoma hotuba ya pamoja ya wadau hao wametaka kuwekwa mifumo rasmi kuwawezesha wanawake kisiasa na kiuchumi.

 

Wadau pia waliibua tatizo la umiliki wa rasilimali mbalimbali hasa ardhi ya kuwa bado ni shida kwa wanawake kutokana na mila na tamaduni za jamii zinazompa nafasi zaidi mwanamume katika kumiliki ardhi jambo ambalo alisema linarudisha nyuma maendeleo ya mwanamke kiuchumi.

“Umiliki wa ardhi kwa wanaume ni asilimia 75 ukilinganisha na asilimia 27 kwa wanawake. Wanawake wenye umiliki wa ardhi wengi wao wanatumia kwa kulima mashamba madogo madogo kwa kuzalisha mazao ya chakula kwa ajili ya familia,” alisema.

Tatizo la upatikanaji wa huduma bora za kijamii alitaja kuwa bado ni kikwazo kingine katika kukuza maendeleo ya wanawake akitolea mfano ukosefu wa huduma ya majisafi na salama inawaongezea wanawake na wasichana mlundikano wa majukumu na kushindwa kushiriki katika shughuli nyingine za kukuza uchumi za siasa hususan uongozi wa kisiasa.

Tatizo la upatikanaji wa huduma bora za kijamii alitaja kuwa bado ni kikwazo kingine katika kukuza maendeleo ya wanawake akitolea mfano ukosefu wa huduma ya maji safi na salama inawaongezea wanawake na wasichana mlundikano wa majukumu ambapo wanashindwa kushiriki katika shughuli nyingine za kukuza uchumi za siasa hususan uongozi wa kisiasa.

“Sera ya maji ya mwaka 2003 imetamka kwamba maji yapatikane ndani ya umbali wa mita 300 kwa mjini na 400 kwa vijijini lakini hali hii haijaweza kufikiwa bado wanawake wanatumia umbali mrefu na muda mrefu kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani” alisema Liundi.

Sambamba na hilo upatikanaji wa nishati nao ni kikwazo kikubwa kwa wanawake ikielezwa kuwa asilimia 85 ya kaya nchini zinategemea kuni kama chanzo cha muhimu cha nishati kwa ajili ya matumizi ya nyumbani hali inayombebesha mzigo wa majukumu mwanamke yasiyo na ujira.