Wakuu wa Mikoa watakiwa kuhamasisha wananchi kutumia usafiri wa treni

06Mar 2024
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Wakuu wa Mikoa watakiwa kuhamasisha wananchi kutumia usafiri wa treni

NAIBU Waziri Wizara ya Uchukuzi, David Kihenzile, amewataka wakuu wa Mikoa kuwahamasisha wananchi kutumia usafiri wa treni katika kusafirisha mizigo ili kuondokana na tatizo la usafiri huo kusafiri ikiwa tupu pindi itakapoanza safari zake.

NAIBU Waziri Wizara ya Uchukuzi, David Kihenzile.

Hayo yamebainishwa leo katika ufunguzi wa kongamano la siku mbili la uwekezaji katika sekta ya reli linalofanyika mkoani Mwanza, ambapo amesema hatua hiyo itachochea ukuaji wa sekta zingine na taifa kujiongezea mapato mara dufu.

Amesema utekelezaji wa reli ya kisasa inayotumia Umeme imeiweka Tanzania kwenye viwango vya kimataifa vya usafirishaji kwa kutumia reli ya kisasa inayotumia umeme na kuhifadhi mazingira.

" Hapa tumekutana kujadili fursa zilizopo pia kuiambia dunia nini tunafanya na tupo wapi tulikuwa na tatizo la uharibifu wa mazingira lakini reli hii inakwenda kukabiliana na tatizo ilo, wawekezaji wajitokeze kwa wingi na wawekeze kwenye reli" amesema Kihenzile

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli nchini, Masanja Kadogosa amesema serikali imejipanga kujenga zaidi ya kilomita 4700 za reli ya kisasa kwa lengo la kukuza uchumi na kila mwananchi aweze kuwa na maendeleo.

Amesema reli hiyo siyo pambo bali ni fursa kwa wananchi kwani afrika inaunganishwa na reli, ndege na meli hivyo tunapaswa kuboresha miundombinu ya kiuchukuzi nchini ili kwenda na sambamba na fursa hizo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amesema kuboreshwa kwa bandari ya Dar es salaam itachangia kuongezeka kwa kiwango kikubwa cha mizigo kushushwa na kusafirishwa kupitia reli hiyo ya kisasa ambapo Mwanza wamebahatika kwani ndio mwisho wa reli hiyo hivyo ni lazima wajipange kuchangamkia fursa hiyo.

"Kama mizigo hii yote itakuja Mwanza, je sisi tutapakia nini kwenye treni yetu kurudi kwenye bandari ya Dar es salaam, tumejipanga kuhamasisha kilimo chenye tija Mwanza, ufugaji wa kisasa na usindikaji wa samaki na madini ili tuingie kwenye mzunguko wa kibiashara" amesisitiza Makalla.