Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugezi wa TWCC, Mwajuma HAmza, amesema tuzo hizo zinalenga kuonesha mchango wa mwanamke mjasiriamali katika kukuza uchumi wa nchi na kuchochea maendeleo ya jamii.
"Wanawake ni nguzo muhimu sana katika maendeleo ya jamii yoyote na kwamba wanawake wana uwezo wa kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda na biashara endapo tu wataendelea kuaminiwa na kupewa nafasi ya kufanya hivyo," amesema Mwajuma.
Aidha, amesema mchakato wa wa upatikanaji wa washindi wa tuzo umeanza tangu Februari 20 hivyo TWCC wanaendelea kuwahimiza wanawake wajasiriamali kuendelea kujisajili kwa kujaza fomu inayopatikana kwenye ofisi za chama hicho katika mikoa yote.
"Mwaka huu TWCC imetoa nafasi kwa wananchi kupendekeza wanawake vinara kwenye biashara na hasa wale wanaokidhi vigezo vilivyowekwa ili waweze kuingizwa kwenye mchakato wa tuzo hizi," amesema Mwajuma.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa, kwa mwaka huu kuna vipengele 20 vitakavyoshindaniwa vikiwemo sekta ya kilimo, uzalishaji, madini, usafirishaji, biashara ya kuuza nje ya nchi, huduma za kifedha, ujenzi, afya, utalii, uhandisi, mawasiliano, sanaa, teknolojia ya habari, uvuvi, usimamizi wa hafla, huduma za chakula (mama lishe) pamoja na ufugaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi ya TWCC, Mercy Sila, ameshukuru serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ambapo wanawake wengi wameweza kuanzisha biashara na viwanda vidogo vidogo ambavyo vimewaongezea kipato.
"Kipekee tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mazingira mazuri ya biashara, lakini pia niwashukuru wadau wetu wote ambao wameendelea kujitokeza kudhamini tuzo hizi ambapo zawadi nzuri zitatolewa kwa washindi na kupata fursa ya kutembelewa na Chama kwenye shughuli zao," amesema Mercy.
Tuzo hizo zitatolewa jijini Dar es Salaam ambapo kunatarajiwa kuwepo na mgeni rasmi kutoka Serikalini ambaye atakabidhi tuzo hizo kwa washindi watakaotangazwa.