Amewataka kutumia nafasi hiyo kukemea ukatili huo ili kulinda utu wa mtoto husika.
Ametoa marufuku hiyo kwenye Kongamano la Mwaka la Muunganiko wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali mkoani Shinyanga, lililolenga kutafakari mafanikio na utekelezaji wa shughuli za kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa mwaka 2023.
Amesema mtindo wa maisha ya kisasa umewaathiri wazazi wengi na hata kusahau malezi bora ya watoto wao, huku wengine wakikuta mtoto wa jirani akifanyiwa ukatili hawakemei kitendo hicho bali wanafurahi na kuanza kurekodi video kwa kutumia simu zao na kuirusha kwenye mitandao ya kijamii.
“Kurekodi video hizo pia ni sehemu ya ukatili acheni, hebu rudini zama za zamani tuwe na malezi bora ya watoto, pamoja na kumchukulia mtoto wa jirani ni mtoto wako, ukimkuta anafanyiwa ukatili kemea ikishindikana chukua hatua za kisheria,” amesema Samizi.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuunga mkono mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kufanya nayo kazi ya kupinga ukatili wa kijinsia zikiwamo mimba na ndoa za utotoni ili jamii ibaki kuwa salama na kwamba shirika lolote litakapopata changamoto wasisite kuwasiliana naye ili waitatue.
Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Aisha Omary, amesema mashirika yasiyo ya kiserikali yamesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ukatili ndani ya jamii zikiwamo mimba na ndoa za utotoni na kwamba kwa mwaka jana hakuna ndoa hata moja ya utotoni ambayo ilifungwa wilayani hapa.
Mwakilishi wa dawati la jinsia kutoka Jeshi la Polisi Shinyanga, Takelove Ayo, amesema mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa yakifanya kazi kubwa na hata kuisaidia polisi katika kesi za ukatili ambapo zinakwenda kwenye dawati hilo zikiwa zimekamilika.
Naye Mwenyeki wa muunganiko wa mashirika hayo, Jonathan Manyama, amesema umoja huo ulianzishwa mwaka 2021 na sasa kuna wanachama 36 na lengo lake ni kuunganisha nguvu na kuwa na sauti ya pamoja katika mapambano ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Amesema: “Mkoa wa Shinyanga tulikuwa wa kwanza kwenye masuala ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto lakini sasa hivi ukatili umepungua na tupo nafasi ya 10 siyo namba moja tena”.









