Haki za punda zinavyokiukwa nchini

25Feb 2024
Thobias Mwanakatwe
DODOMA
Nipashe Jumapili
Haki za punda zinavyokiukwa nchini

SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali la Inades Formation Tanzania (IFTz) linalojishughulisha na maendeleo ya kijamii, kiuchumi na ustawi wa kijamii limeiomba serikali kuingiza mnyama punda katika mtaala wa masomo ya ustawi wa wanyama.

Limesema hatua hiyo itasaidia wataalamu wanaohitimu vyuo vya afya na tiba ya mifugo kuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa mnyama huyo.

Daktari wa Afya na Tiba ya Wanyama wa shirika hilo, Dk. Charles Bukula, akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari mjini hapa, amesema mtaala wa Tanzania haujamzungumzia punda kama ilivyo kwa wanyama wengine kama farasi.

Amesema hali hiyo ni dosari kwa ustawi wa punda kwa kuwa inasababisha mnyama huyo akose haki za msingi ikiwamo matibabu.

Amesema kukosekana wataalamu wa mnyama punda kunasababisha changamoto nyingi, ikiwamo kutokaguliwa nyama ya punda anapochinjwa. Hivyo, ikitokea mtumiaji amepata madhara hawezi kupata msaada wowote.

Amesema kuwa serikali pamoja na wadau wa ustawi wa wanyama wanapaswa kupitia upya kanuni za ustawi wa wanyama ili punda kujumuishwa kama mnyama anyayeonekana kuwa haarini kutoweka.

"Ifike wakati jamii imthamini punda kama inavyothamini wanyama wengine kwa kumpatia matibabu, lishe bora na kutosababishiwa maumivu yasiyo ya lazima, mfano kupigwa ovyo wakiamini kuwa punda haumii," amesema.

Dk. Bukula amesema katika kuendelea kumthamini punda, serikali itenge mwezi Mei kuadhimisha siku ya punda duniani ambayo itakuwa inaadhimishwa kila mwaka kama wanavyoadhimisha siku ya ugonjwa wa kichaa duniani kwa lengo kutoa hamasa kubwa kwa punda kupewa thamani kama wanyama wengine.

Ameongeza kuwa shirika la IFTz linatambua kuwa kama punda akistawi, jamii itamtumia kwa muda muda mrefu na kupata kipato pale anapotumika katika shughuli za usafirshaji mizigo.

Amesema punda kama ilivyo kwa wanyama wengine, anazo haki ambazo ni pamoja na haki ya kutopata njaa, kiu au udhoofu wa mwili, haki ya kupewa chakula bora na maji ya kunywa, haki ya kuwa huru dhidi ya hofu na msongo wa mawazo na haki ya kutosumbuliwa kifikra.

Nyingine ni haki ya kuwa huru dhidi ya usumbufu wa mwili wake, haki ya kuwa huru dhidi ya maumivu, majeraha na magonjwa na pia ana haki ya kukingwa dhidi ya maradhi, majeraha au maumivu.

Shirika la IFTz linaendesha mradi wa kuboresha maisha ya jamii kupitia ustawi wa mnyama punda  kwa ufadhili wa Shirika la Brooke East Africa, mradi ambao unaendeshwa katika mikoa ya Dodoma, Iringa na Singida.

Malengo mahususi ya mradi huo ni kubadilisha na kuboresha ustawi wa punda wanaofanya kazi katika jamii, kuwasaidia katika kustawi na kuendeleza ustahimilivu zaidi, kuongeza vishawishi ili kusaidia kuingizwa kwa mahitaji ya punda katka sera na desturi ikiwa ni pamoja na maandalizi ya maafa na dharura.

Malengo mengine ni kutengeneza mifumo thabiti ya afya ya wanyama inayokidhi mahitaji ya haraka na ya baadaye kwa punda wanaofanya kazi.