Kiwanda kilichopewa leseni na serikali kuzalisha mabati, kimebainika kinauza majokofu, vigae, PVC na bodi za dari (ceiling boards).
Kutokana na kadhia hiyo, waziri huyo ameagiza taasisi za serikali kupita kwenye viwanda vyote nchini vinavyozalisha mabati na bidhaa nyingine kukagua kama bidhaa zinazozalishwa na viwanda nchini zinakidhi viwango.
Taasisi zilizopewa maagizo hayo ni Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Shirika la Viwango Tansania (TBS) na Wakala wa Vipimo (WMA).
Waziri Kijaji ametoa maagizo hayo jijini Dodoma alipozuru kwenye viwanda vya kuzalisha mabati vya ALAF na Herosean Enterprises inayozalisha mabati ya DRAGON ikiwa ni utekelezaji maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia alishaagiza kuwa viongozi wanapaswa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na viwanda nchini, zinazingatia ubora.
Waziri huyo akiwa kwenye kiwanda cha Herosean Enterprises, alibaini kuwapo bidhaa zingine ambazo hazihusiani na malengo halisi ya leseni iliyotolewa na BRELA.
"Leo (juzi) nimetembelea viwanda hivi viwili lakini cha kusikitisha hiki kiwanda cha kuzalisha mabati ya DRAGON kinajihusisha na biashara ya kuuza bidhaa nyingine ikiwamo friji, PVC, vigae na ceiling boards (bodi za dari).
"Nimewataka wanioneshe vielelezo vya usajili wa bidhaa hizo tofauti na bidhaa za mabati kiwandani hapa, sikupata majibu sahihi.
"Ninaziagiza taasisi zinazohusika na hili suala zilishughulikie ili kupata ukweli wake," aliagiza Waziri Kijaji aliyefuatana maofisa kadhaa toka wizara yake.
Vilevile, Waziri Kijaji ameagiza wamiliki wa viwanda vinavyozalisha bidhaa za mabati nchini, kuuza bidhaa hiyo kwa bei rafiki ili kunufaisha wanunuzi kwa makundi yote.
"Jambo lingine ninalotaka kuwaambia watanzania kwa bidhaa nilizotembelea leo, ukilinganisha na nchi zingine, mabati yetu Tanzania bei yetu iko chini kuliko nchi yoyote ile ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo niwatake msisikilize kelele za mtaani, endeleeni kujenga kwa wingi na sisi serikali tunaendelea kutekeleza miradi yetu," amesema Dk. Kijaji.
Ofisa Huduma kwa Wateja Kiwanda cha Mabati ya ALAF, Herry Jailos, ameshukuru serikali kwa kufanya ziara na kubaini changamoto zinazowakabili ikiwamo ukosefu wa masoko kutokana na wazalishaji bidhaa hizo kuwa wengi nchini.
Kiwanda kubainika kuwa na bidhaa ambazo hakina leseni ya uzalishaji wake si tukio jipya nchini. Novemba 3, mwaka jana, serikali ilibaini kuwa kiwanda cha kampuni ya Toco & Company Limited kilikuwa kinazalisha mifuko ya plastiki iliyopigwa na serikali ilihali kina leseni ya kuzalisha mifuko ya plastiki yenye ubora unaotakiwa.
Vilevile, ilibaini wakati wa ukaguzi kiwandani huko, Mbezi Juu, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, kwamba kiwanda cha kampuni hiyo iliyosajiliwa nchini Oktoba 19, 2019, kilikuwa na mabango nje ya kiwanda yanayoonesha kinazalisha mabati ilhali usajili wake ni wa kuzalisha mifuko kwa ajili ya vifungashio visivyoharibu mazingira.
Juni Mosi, 2019, serikali ilianza kutekeleza rasmi marufuku ya kuzalisha, kusambaza na kutumia mifuko ya plastiki.