Tusijitoe soko la forodha EAC, changamoto zijadiliwe

31Aug 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tusijitoe soko la forodha EAC, changamoto zijadiliwe

SERIKALI imeshauriwa kujitoa kwenye soko la pamoja la forodha la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),kutokana na kupungua kwa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.

Ushauri huo ulitolewa juzi na Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwa kutumia taarifa ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), iliyoonyesha kupungua kwa mizigo inayosafirisha. Kwa mwaka 2015/16, Tazara ilijiwekea lengo la kusafirisha mizigo tani 200,000, lakini kutokana na wafanyabiashara wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kukimbia bandari hiyo, ilisafirisha tani 128,105.

Kamati hiyo imeeleza kuwa kwa sasa wafanyabiashara wengi wamehamia kwenye bandari za Beira ya Msumbiji na Mombasa, Kenya.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Selemani Kakoso, alisema Tanzania kwa sasa haifaidiki kwa kuwa kwenye soko hilo la pamoja inafanya kazi ya kukusanya kodi kwa nchi hizo.

Alisema wakati mizigo kwenye bandari ya Dar es Salaam ikipungua kwa kasi, kwenye bandari nyingine kama ya Beira nchini Msumbiji, mizigo imeongezeka kwa sababu hawatekelezi inavyotakiwa suala hilo la soko la pamoja.

Alisema Tanzania ikijitoa kwenye soko hilo, mizigo kwenye bandari ya Dar es Salaam itaongezeka kwa sababu wafanyabiashara waliokimbia watarudi.

Suala la kupungua kwa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam lilishatolewa maelezo na Serikali, akiwamo Rais John Magufuli kwamba wafanyabiashara wengi waliokimbia ni waliokuwa wakikwepa kulipa kodi na kwamba pamoja na hali hiyo, makusanyo ya kodi yameongezeka.

Kamati hiyo ya Bunge inawajibika kushauri pale inapoona kuna mambo hayaendi sawa kama la Tazara kusafirisha mizigo kidogo kinyume cha lengo lake, lakini haikuwa vizuri kushauri Tanzania ijitoe katika soko la pamoja la forodha la EAC kutokana na sababu hiyo ambayo inaweza kujadiliwa na mamlaka husika katika jumuiya.

Kujiondoa maana yake ni kwamba tutakuwa tumejiondoa katika uanachama wa EAC na athari zake ni kubwa kuliko faida.

Wakati huu ambao EAC inakaribia kuanza kutekeleza hatua ya kuwa na sarafu moja, sio vizuri kuzungumzia kujitoa, bali tuzungumzie changamoto zinazojitokeza na kuzitafutia ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo.

Sisi tunaona kwamba mihemuko na uamuzi wa kukurupuka kujitoa katika soko la pamoja la forodha haufai kwa kuwa EAC ilianzishwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi zote wanachama.

Sote tunakumbuka athari za kiuchumi kwa Tanzania, Kenya na Uganda ambazo zilikuwa wanachama wa jumuiya hiyo iliyovunjika mwaka 1977.

Mwaka 2013 wabunge walicharuka na kutaka Tanzania ijiondoe katika EAC kwa madai kuwa baadhi ya nchi zilikuwa zinaitenga, lakini busara za Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, zilisaidia alipolihutubia Bunge na kutangaza kwamba Tanzania itakuwa ya mwisho kujiondoa.

Tutaonekana watu wa ajabu kuzungumzia kujitoa katika mtangamano wa EAC wakati nchi zote duniani zikihangaika kuanzisha jumuiya mbalimbali za ushirikiano kwa ajili ya kupata fursa za maendeleo pamoja na kukabiliana na vitisho kama ugaidi.

Tanzania kuwa mwanachama wa EAC imepata mafanikio mengi, mojawapo ni fursa ya kupata mradi wa bomba la mafuta litakalojengwa kutoka Uganda hadi Tanga na kutoa ajira kwa takribani watu 10,000.

Tunaishauri Serikali kukutana na kamati hiyo ya Bunge na kuipa majibu ya kuridhisha kuhusiana na suala hilo, huku ikiendelea kuweka mazingira bora katika bandari ya Dar es Salaam ili kuwavutia wafanyabiashara zaidi wapitishe mizigo yao.