Simba Queens yaipangia mikakati Yanga Princess

31Dec 2023
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Simba Queens yaipangia mikakati Yanga Princess

BAADA ya kufanikiwa kuvuna pointi tatu kwenye mchezo wao uliopita dhidi ya Baobab Queens, Kocha Mkuu wa Simba Queens, Juma Mgunda, ameweka wazi kuwa sasa wameanza mikakati ya kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo wao ujao dhidi ya watani zao Yanga Princess, utakaochezwa Januari 3.

Kocha Mkuu wa Simba Queens, Juma Mgunda.

Simba juzi iliibuka na ushindi mnono wa mabao 5-2 dhidi ya Baobab Queens ikiwa ni mchezo wa raundi ya pili ya 2 ya Wanawake Tanzania uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Baada ya kukamilika kwa dakika 90, Kocha Mgunda alisema wamemaliza mchezo na Baobab Queens salama na hakukuwa na majeraha makubwa sana na kuwapongeza wachezaji wake kuendelea kupata alama tatu muhimu.

Hata hivyo, alisema licha ya ushindi huo mnono bado ameona mapungufu na ameanza kufanyia kazi mazoezini ili kuhakikisha wanaimarisha ubora wao kabla ya mchezo unaofuata.

“Kwangu kila mechi inakuwa na mipango yake, tumemaliza mchezo na Baobab Queens, mikakati inayofuata ni juu ya mchezo unaofuata dhidi ya Yanga, huu utakuwa na mipango yake mingine na tayari tunaenda kuianza mazoezini, yapo mapungufu madogo niliyoyaona, naenda kuyafanyia kazi," alisema Mgunda na kuongeza,

"Hii ni Derby, lazima tujipange vizuri, tunarudi kwenye uwanja wa mazoezi kwa lengo la kuhakikisha tunapata pointi tatu kwenye kila mechi ili kufikia malengo yetu msimu huu,” alisema Mgunda.

Kwa upande wake, Nahodha wa Simba, Vivian Corazone alisema Ligi imekuwa ngumu lakini wanaendelea kujiandaa kwa kila mchezo kuhakikisha wanapata alama tatu kwenye kila mchezo ili kufikia malengo yao ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Alisema baada ya ushindi wa juzi nguvu zao wanazielekeza katika mechi ya 'Derby' dhidi ya Yanga Princess.

“Ligi imekuwa ngumu na timu zote zimejiandaa vizuri, tunarudi uwanja wa mazoezi kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Yanga, lengo letu kuu ni kuchukua pointi zote tatu dhidi ya watani wetu,” alisema Vivian.