Katika mechi mbili ambazo ameiongoza timu hiyo tangu kuchukua nafasi ya Roberto Oliviera 'Robertinho', Simba imeruhusu bao moja pekee kwenye kipigo cha bao 1-0 nyumbani kwa Wydad Casablanca kwenye mchezo wa Ligi ya mabingwa Afrika, lakini iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar juzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Benchikha amewapongeza wachezaji wake hasa safu ya ulinzi kwa kuonyesha mabadiliko makubwa ya kiuchezaji.
Akizungumza jana siku moja baada ya mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar, Benchikha alisema ameridhishwa kuona timu yake haijaruhusu goli kwenye mchezo wa juzi na kwamba walikuwa na nafasi ya kupata ushindi mkubwa zaidi lakini wameangushwa na uwanja ambao haukuwa rafiki na kuwanyima nafasi ya kucheza soka safi lakini hata hivyo amefurahishwa na kile wachezaji wake walichokifanya.
Alieleza kuwa Kagera ni timu nzuri na walitoa ushindani mkubwa lakini wao walikuwa bora katika kila eneo ikiwemo safu ya ulinzi ambayo hawajaruhusu wapinzani wao kupata bao na kufanikiwa kuibuka na ushindi huo.
“Tulicheza vizuri sana.., nawapongeza wachezaji wangu, tulimiliki sehemu kubwa ya mchezo lakini uwanja haukuwa rafiki na kutunyima kucheza soka safi, Kagera ni timu nzuri wanacheza soka safi na walitupa ushindani mkubwa ingawa sisi tulikuwa bora ndio maana tumepata ushindi,” alisema Benchikha.
Aliongeza kuwa ameridhishwa na jinsi safu yake ya ulinzi kuwa makini na anaimani kubwa kwenye mchezo dhidi ya Wydad Casablanca watafanya vizuri na kuibuka na ushindi ambao kwao ni muhimu.
“Baada ya mechi hii tunaenda kucheza mechi ya ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca, kwetu ni fainali kwa sababu tunahitaji ushindi, tunarudi uwanja wa mazoezi kujiimarisha zaidi,” alisema Benchikha.
Aidha, aliwataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi Jumanne kushuhudia na kuisapoti timu yao kwenye mchezo dhidi ya Wydad Casablanca na amewahakikishia wamejiandaa vya kutosha kwa ajili ya mchezo huo muhimu.
"Mpira ni mashabiki, kwetu wa nafasi kubwa sana katika kutusaidia kufanya vizuri, tunaomba wajitokeze kwa wingi na tutaonyesha soka safi zaidi ya lile tulilolionyesha Morocco, tunaka ushindi tu," alisema Benchikha.
Simba inahitaji ushindi pekee kwenye mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa ili kufufua matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.










